Kwa hatua lilipofikia bifu zito kati ya mastaa mashosti wa zamani, Wema
Isaac Sepetu ‘Madam’ na Kajala Masanja ‘Kay’, imebainika kwamba hakuna
ambaye yupo tayari kumzika mwenzake.
Kwa mujibu wa chanzo makini ambacho ni mtu wa karibu wa waigizaji hao,
mtafaruku huo umechukua sura mpya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya
Madam kuanika ubaya aliotendewa na Kajala aliyewahi kumlipia faini ya
shilingi milioni 13 na kumuepusha na kifungo cha miaka 7 jela, Machi 25,
2013.
“Hali ni tete, Madam ameibua bifu upya alipofunguka kupitia kipindi
chake cha In My Shoes kinachorushwa na Runinga ya EATV, hapo ndipo
ilipodhihirika kwamba wawili hao hawawezi kuzikana wala kusameheana.
“Wafuasi wa Kajala hawakufurahishwa na maneno ya Wema ambayo walidai
yalikuwa na lengo la kumvua nguo mwenzake, yale matumaini ya kusameheana
hayapo tena, ni bifu hadi wanakwenda kaburini,” kilisema chanzo hicho.
Kwenye kipindi hicho, mbali na mambo mengine, Wema alieleza kuwa Kajala
hakuwahi kuwa rafiki yake lakini alijitolea kumlipia faini kumuepusha na
kifungo kutokana na kuguswa na kuingiwa na moyo wa huruma kama msanii
mwenzake.
“Sikuwahi kuwa na urafiki na Kajala, kilichonifanya niwe karibu naye ni
mwanaye ambaye alikuwa akinipenda na kutaka kukutana na mimi...,”
alisema Madam.
Kupitia kipindi hicho, Wema pia alizungumzia kiini cha ugomvi wao ambapo
alianika kinagaubaga kwamba alichukizwa na suala la Kajala kumsaliti
kwa kutembea na mchumba wake aitwaye CK (yule kigogo aliyesumbua mjini
kwa kutapanya fedha).“Kajala hana fadhila, huwezi amini mtu ambaye
niliamua kujitolea kwa moyo wangu kumlipia Sh. milioni 13 huyohuyo aje
kutembea na mchumba wangu, huku ni kukosa ubinadamu kulikopitiliza,”
alisema Wema.
Saa chache baada ya Wema kufunguka, wafuasi wa Kajala mitandaoni
walimjia juu Wema kwa kumwambia kuwa hana busara na ndiyo maana ameamua
kutamka maneno hayo waliyoyaita kuwa ‘ni ya aibu’.
“Wema hana busara, mtu mwenye busara zake hawezi kuzungumza hadharani
mambo ya kuibiana mabwana, ni ujinga tu. Unazungumza ili iweje?”
aliandika mfuasi wa Kajala mtandaoni.
Jitihada za kumpata Kajala aweze kuzungumzia mashambulizi hayo ya Wema
hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokelewa lakini shosti
yake wa karibu alisema Kajala amechukizwa na maneno hayo ya Wema na
kamwe hatakuja kukaa naye meza moja, achilia mbali kumzika.
“Kajala hakufurahishwa na maneno ya Wema, hali ni mbaya, amesema kamwe
hawezi kukaa na Wema meza moja maana amekuwa mtu wa kumdhalilisha kila
kukicha, alianza kwa kumwambia ana nuksi na sasa amemdhalilisha katika
kipindi chake, kamwe hatamsamehe na hayuko tayari kumzika wala kuzikwa
na Wema,” alisema shosti huyo.
Baada ya kipindi hicho kuruka hewani, baadaye mwanahabari wetu alimvutia
waya Wema ambaye alizidi kusimamia msimamo wake kuwa kamwe hawezi
kumsamehe Kajala kwa kuwa hakuonesha ubinadamu kwa kitendo cha
kumkwapulia bwanaa’ke.
“Mengi nimeyasema kwenye kipindi changu, najuta kumfadhili Kajala hivyo
hata akifa mimi pia siwezi kuhusika chochote maana hana fadhila na hata
yeye asipokuja kwangu sawa tu,” alisema Madam.
Msanii mwenye taito kubwa Bongo Movies ambaye hakupenda jina lake
lichorwe gazetini, aliwaomba mama wa wawili hao kutumia busara za kiutu
uzima kumaliza bifu hilo.
“Haya mambo ni ya wanawake, mama zao wanatakiwa kukutana na kulijadili
ili waweze kulimaliza tatizo hili sugu,” alisema msanii huyo.
Jitihada za kuwatafuta wazazi wa wasanii hao ili kusikia wanazungumziaje
bifu hilo, hazikuzaa matunda kwani simu ya mama Wema, Mariam Sepetu
iliita bila kupokelewa huku mama Kajala akikosekana hewani.
Kabla ya kuachiwa huru kwa faini, Kajala alihukumiwa kwenda jela miaka 7
au kulipa faini ya shilingi milioni 13 kwa kesi ya kuuza nyumba
iliyowekwa kizuizini na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) baada ya mumewe, Faraji Agustino kukumbwa na tuhuma za
kutakatisha fedha haramu.
-GPL
No comments:
Post a Comment