17 February 2015

WAZIRI MKUU KUFUNGUA MKUTANO WA KIKANDA JUU YA UKUAJI NA MAISHA YA BAADAE YA MIJI YA AFRIKA



 
Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo Endelevu (UONGOZI Institute) imeandaa  mkutano  wa kikanda  utakaokutanisha viongozi na watunga sera  kutoka  nchi  za Afrika mashariki kuzungumzia changamoto za ukuaji wa miji na kushughulikia hali ya baadaye ya miji ya Afrika.

Mkutano huu uliopewa jina la, ‘Maisha ya baadae ya nchi za Afrika Mashariki: Jinsi gani tunataka kuishi mwaka 2050’, utafanyika katika hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, Kilimanjaro Hotel tarehe 19 na 20 Februari ambapo Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Mizengo Pinda (Mb), atakuwa mgeni rasmi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa UONGOZI Institute, Prof. Joseph Semboja alisema kwamba jukwaa hilo linalenga kuangalia na kujadili changamoto na fursa mbalimbali zinazoletwa na ukuaji wa miji  Afrika Mashariki na jinsi gani viongozi wa Afrika wanaweza kukabiliana nazo kwa pamoja. 

“Kuna uwiano mkubwa wa ongezeko la watu Afrika (na duniani kwa ujumla) wanaoishi mijini na kupelekea msongamano na shinikizo la nyumba, ajira na huduma za kijamii. Ni kwa matokeo haya jukwaa hili limelenga kujadili namna ya kutatua changamoto hizo na kufikiria miji ambayo itatimiza matakwa yetu,” alisema Prof. Semboja. 

Kwa mujibu wa chapisho la UN-Habitat  ‘Hali ya miji ya Afrika 2014’ , “Afrika Mashariki inashika nafasi ya chini katika miji inayokua duniani lakini ndiyo kanda inayoongoza katika kasi ya ukuaji wa miji yake hivi sasa.  Ifikapo mwishoni mwa muongo huu wa sasa idadi ya wakazi waishio mijini itaongezeka kwa asilimia 50 na jumla ya idadi ya wakazi wa mijini ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa kuwa mara tano ya 2010.
Hivyo basi, ukanda wa Afrika Mashariki utakumbwa na changamoto zitakazotokana na ongezeko kubwa la  idadi ya watu mijini; ongezeko kubwa la madai mapya na ya ziada kwa ajili ya utoaji wa nyumba za kutosha na kwa gharama nafuu na huduma mijini, na pengine muhimu zaidi, fursa ya kuzalisha kipato mijini.”

“Ni dhahiri kwamba ukuaji wa miji na maendeleo mijini ni matokeo chanya ya maendeleo ya binadamu na ukuaji wa kiuchumi kama tunaweza kuyakabili kiusahihi. Na hii ndiyo maana nzima ya mkutano huu…Kutuweka katika njia sahihi kwa kutambua vipaumbele vya juu na vitu  muhimu kwa ajili ya maendeleo," aliongeza Prof. Semboja. 
Washiriki wa kongamano hili watatoka: Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan ya Kusini, Tanzania na  Uganda. Waalikwa watakuwa wawakilishi wa ngazi za juu kutoka serikalini, mashirika ya kikanda na kimataifa, miji mikubwa, wasomi, sekta binafsi na asasi za kiraia.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname