Waziri Mkuu Mizengo Pinda amedai kuwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari walioshiriki sherehe za miaka 38 ya CCM mjini Songea, wakiwa
wamevalia sare, ni watoto wa wanachama wa chama hicho tawala, kauli
ambayo imekosolewa na watu wa kada mbalimbali.
Sherehe hizo zilifanyika Jumapili ya Februari 1 kwenye Uwanja wa
Majimaji mjini Songea, zikishirikisha makundi mbalimbali, wakiwamo
wanafunzi hao wa shule za msingi na sekondari ambao walivalia sare za
CCM na kucheza gwaride na halaiki, ambayo kwa kawaida huchukua muda
mrefu kujifunza na kuielewa.
Lakini akijibu swali la mbunge wa viti maalum (Chadema, Susan Lyimo,
mtendaji huyo mkuu wa Serikali alitetea ushiriki wa watoto hao wapatao
500 kwenye sherehe hizo akisema kuwa ni sehemu ya mfumo wa wanachama wa
CCM.
“Susan, utafikiri tulikuwa pamoja. Nilijua tu swali hili lazima
litaulizwa. Ila mtoto wa nyoka ni nyoka. Chama hiki kina mfumo wake
ambao umeshuka mpaka kwenye ngazi ya kitu kinaitwa chipukizi,” alisema
akijibu swali la mbunge huyo aliyetaka kujua sababu za CCM kutumia
watoto kwenye shughuli zake za siasa wakati ina wanachama wapatao
milioni 10 kote nchini.
“Chipukizi hawa ni watoto ambao wamezaliwa kutokana na wazazi wana-CCM,
ndiyo maana chama kiliwatumia. Sherehe ilikuwa nzuri na ilipendeza sana.
Kwa kuwa hawajafikia umri wa kuingia katika masuala ya siasa, halina
madhara lile rafiki yangu, pia bado ni wadogo mno na walikuwa
wanafurahia gwaride na kuvaa sare tu.”
Lyimo hakuridhishwa na jibu hilo la Waziri Pinda, akisema hakutakiwa
kutoa majibu ya aina hiyo na kwamba katika mkusanyiko huo, kulikuwa na
watoto wazazi wao si wanachama wa CCM.
“Lengo la watoto hawa ni kusoma na si kufanya siasa. Iweje mfanye mambo
kwa double standard (ndumilakuwili)?” alihoji na baadaye Pinda alitaka
suala hilo lisiendelee kujadiliwa.
“Naheshimu maelezo ya Susan, lakini kiacheni chama kiendelee na
utaratibu wake. Mfumo wake ndiyo huo, ndiyo ulivyo na sidhani kama kuna
haja ya kuendelea kubishana katika suala hili,” alisema Pinda ambaye
ofisi yake inasimamia elimu ya msingi na sekondari.
Kitendo hicho cha zaidi ya wanafunzi 500 kushiriki sherehe hizo kwa
kuimba nyimbo mbalimbali za CCM, kucheza halaiki na gwaride kimekosolewa
na wasomi na wanasiasa nchini, wakisema wanafunzi wanaweza
kushirikishwa kwenye shughuli za kitaifa tu, si za vyama vya siasa.
Kabla ya nchi kuruhusu tena siasa za vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya
tisini, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walikuwa wakitumiwa
kwenye shughuli za chama tawala na za Serikali, lakini imekuwa ni nadra
sana kuonekana kwenye mikutano ya kisiasa tangu uhuru wa kidemokrasia
ulipoanza.
Lakini ili kufanikisha sherehe hizo za CCM ambazo zilifanyika Jumapili
kutokana na siku ya kuzaliwa chama hicho (Februari 5) kuwa katikati ya
wiki, maofisa wa elimu ya sekondari wa Manispaa ya Songea waliwaandikia
barua wakuu wa shule zilizopo karibu na Uwanja wa Majimaji, wakiwataka
kuhudhuria pamoja na walimu na wanafunzi ambao waliagizwa kuvaa sare.
Majibu hayo hayakuridhisha wabunge wengine na baada ya kipindi cha
maswali ya papo kwa papo ambacho Waziri Pinda alikianzisha ili kujibu
hoja mbalimbali za utendaji wa Serikali, mbunge wa Muhambwe
(NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliomba mwongozo wa Spika juu ya suala
hilo.
Mkosamali alisema kitendo cha kuwatumia wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari katika sherehe hizo ni sawa na kuwalazimisha kukishabikia
chama ambacho hawakipendi.
“Kuna barua zinaonyesha jinsi wanafunzi walivyolazimishwa kuvaa sare za
chama na kuhudhuria sherehe hizo. Jambo hili si sawa kwa sababu
linawalazimisha wanafunzi kuwa wanachama wa chama ambacho hawakipendi,”
alisema Mkosamali.
Hata hivyo, Spika Makinda hakutoa nafasi kwa upande wa Serikali kujibu na badala yake alisema kuwa litatolewa ufafanuzi baadaye.
Credit Mwananchi

No comments:
Post a Comment