17 February 2015

HUZUNI:AUMWA NA NYOKA, ATOKWA MAGAMBA

KWELI duniani hujafa hujaumbika! Mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Kondo Athuman, mkazi wa Pugu Mnadani, Dar es Salaam amejikuta akiishi kwenye mazingira magumu kutokana na magamba kumtoka mwilini na kukatika vidole baada ya kumuua nyoka.  
Kondo Athuman akionyesha mguu unaotoka magamba.
CHANZO CHAKE
Akisimulia kwa huzuni, Kondo alisema mwaka 2006 alisafiri na mkewe kwenda mkoani Morogoro ambapo walipata shamba na kuendesha shughuli za kilimo cha mahindi na ufuta.
Alisema siku moja akiwa ametoka shambani alijipumzisha nyumbani kwake lakini ile anaingia ndani akamuona nyoka mkubwa na alijitahidi kumuua lakini kabla ya kumuua akakimbia, akashangaa kumuona wa pili akiingia na kufanikiwa kumuua.
ALIMUUA NYOKA, AKAMFUKIA, ASUBUHI AKAKUTA MTI
Akifafanua zaidi Kondo alisema baada ya kumuua nyoka wa  pili akiwa na mkewe waliendelea kumsaka yule wa kwanza ambaye aliingia chini ya kabati na kufanikiwa kumkata kichwa.
Baada ya kuwaua nyoka hao aliwatoa nje na kuchimba shimo kisha kuwafukia lakini cha ajabu alipoamka asubuhi na kwenda kuangalia alipowafukia, alikuta shimo likiwa wazi huku kukiwa kumepandwa mti.
KUISHIWA NGUVU NA KUTOKWA MAGAMBA
“Mara baada ya kuwaua wale nyoka nilianza kusikia baridi na kuishiwa nguvu  ambapo zilipita siku tatu nikaanza kutokwa magamba yanayofanana na wale nyoka huku nikitokwa na vidonda vikubwa mguuni na vidoleni kisha mikono ikawa inagoma kukunjuka. 

VIDOLE VIKAANZA KUKATIKA
“Niliendelea kuumwa mpaka vidole vingine vikakatika kutokana na vidonda. Kweli nateseka ambapo baada ya kuzidiwa tuliamua kurudi nyumbani Dar ambapo nilienda katika hospitali mbalimbali na kupimwa vipimo vyote ambapo nilionekana sina ugonjwa wa ukoma wala mwingine wowote.
“Nikaanza kutafuta dawa za kienyeji kwa waganga. Mganga mmoja alinieleza kwamba wale nyoka hawakuwa wa kawaida bali walitumwa na yote hayo yalitokana na wivu kwani wazee wa pale Morogoro walikasirika walipoona tunawapita kimaendeleo kwa kuwa nilikuwa na bidii ya kufanya kazi na kuvuma mavuno mengi,” alisema Kondo.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname