Same. Katika hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, Dk Michael Kadege limekutwa likipeperusha bendera katika eneo la Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na kuzua tafrani kati ya mkuu huyo na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela.
Gari hilo likiwa na Bendera ya Taifa, lilionekana
saa nne asubuhi likiwa limeegeshwa katika eneo la Mamba Myamba katika
Jimbo la Same Mashariki huku Dk Kadege akiwa kwenye mgahawa.
Kitendo cha gari hilo kuonekana likipeperusha
bendera kilimfanya Kilango kulifuata akidhani ni la Mkuu wa Wilaya ya
Same, ndipo akakuta ni la Mbozi.
“Hili gari siyo la Same na kawaida mkuu wa wilaya
nyingine haruhusiwi kupeperusha bendera kwenye eneo ambalo siyo lake,
huyu amekuja kwenye mambo yake ya siasa, anapeperusha bendera ili
wananchi wamwone kuwa yuko juu na hii ni hujuma kwenye jimbo langu,”
alilalamika Kilango.
Alisema Dk Kadege ni miongoni mwa watu wanaotaka
kugombea ubunge Jimbo la Same Mashariki lakini ni vyema akasubiri muda
ukifika ajitokeze hadharani badala ya kujenga mpasuko kwa CCM katika
jimbo hilo.
“Huyu amekuja kwa ajili ya vikao vya ndani, mwaka
2005 tuligombea wote kwenye kura za maoni nikamshinda nikiwa na kura 389
yeye 46 akawa mtu wa nne, mwaka 2010 mimi nilipata kura 7,900 na yeye
alipata 2,200 sasa ameanza, sikatai lakini asubiri muda wake,” alisema
Kilango.
Kwa upande wake, Dk Kadege alisema hakuwa na
taarifa kuwa gari lake linapeperusha bendera kwa kuwa yeye hahusiki
kuweka bendera, akataka dereva wake aeleze sababu za kupeperusha bendera
kwenye eneo lisiloruhusiwa.
Dk Kadege alisema yeye yuko likizo na alikwenda
nyumbani kwao Same kupumzika na hafanyi shughuli zozote za kisiasa
katika jimbo hilo kama inavyodaiwa na Kilango.
Dereva wa mkuu huyo wa wilaya ambaye alikataa
kutaja jina lake, alipohojiwa sababu za kupeperusha bendera katika eneo
lisiloruhusiwa alisema alikuwa akifanya usafi wa gari na alipohojiwa
zaidi alidai siyo msemaji wa mkuu wa wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi alisema
kutokana na sheria, utaratibu na miongozo ya wakuu wa wilaya, kiongozi
huyo wa wilaya haruhusiwi kupeperusha bendera katika eneo ambalo siyo
lake.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa
namba 19 ya Mwaka 1997 na Sheria ya Serikali za Mitaa namba Saba na Nane
ya mwaka 1982, mkuu wa wilaya ni msimamizi wa shughuli za kimaendeleo
na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika wilaya yake tu.
Kapufi alisema atawasiliana na Dk Kadege kama
anafahamu utaratibu na miongozo waliyopewa wakati wa kuanza kazi ili
ajue kama alikusudia kufanya hivyo au kama alipitiwa.
Chanzo Gazeti la Mwananchi
Chanzo Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment