17 September 2014

Mwanamke ajirusha kwenye bwawa la Mamba

Mwanamke mwenye umri wa miaka 65 mjini Bangkok, Thailand, amefariki baada ya kujirusha katika bwawa lenye Mamba katika shamba la kutunza na kuhifadhi wanyama hao karibu na mji huo.
Walioshuhudia kitendo hicho wanasema kuwa walimuona mwanamke huyo, Wanpen Inyai, akijirusha katika bwawa lenye Mamba katika kituo cha kuwatunza wanyama hao cha Samut Prakarn, siku ya Ijumaa.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa jarida la The Bangkok Post. Wafanyakazi wa kituo hicho walikosa kumuokoa mama huyo.
Polisi wanasema kuwa walifahamishwa na familia ya mama huyo kwamba alionekana mwenye afya duni na mwenye kusongwa na mawazo kabla ya kifo chake.

Kituo hicho kina zaidi ya Mamba 100,000 katika mabwawa yake
Vituo vya watalii nchini humo vinasemekana kukosa mikakati ya usalama.
Polisi walithibitisha kifo cha Bi Wanpen Jumanne mchana.
Kwa mujibu wa ripoti, Bi Wanpen alivua viatu vyake kabla ya kujirusha ndani ya bwawa hilo, ambalo linasemekana kuwa na kina cha mita tatu.
Wafanyakazi walijaribu kutumia vijiti virefu kuwafukuza Mamba hao kwa lengo la kuwazuia wanyama hao kumshambulia mwanamke huyo.
Mapema siku hiyo, familia ya Wanpen, ilijaribu kutoa taarifa ya kupotea kwake la lengo la kumtafuta ingawa walifahamishwa kusubiri kwa saa 24.
Kifo chake kinafanana na kisa kimoja kilichomkumba mwanamke aliyejiua mwaka 2002 kwa njia hiyo hiyo katika kituo cha kuwatunza Mamba.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname