MOJA ya tatizo kubwa linalowasumbua wasanii wetu,
hasa hawa wa muziki wa kizazi kipya, ni ukosefu wa usimamizi makini wa
kazi zao za sanaa, au kama wazungu wanavyosema, Management.
Wenyewe, hasa chipukizi wanaotaka kutoka, utawasikia wanasema, nina
kipaji lakini sina meneja. Ingawa wanaposema meneja maana yake ni
msimamizi wa kazi zao, lakini kwao huwa na maana pana zaidi, kwamba mtu
huyo, ndiye awe bosi wake, amsaidie hela ya studio, kazi ikitoka
aipeleke redioni kisha awe ndiye msimamizi na mpangaji wa kila kitu
chake.
Mikataba wanayoingia na mameneja hawa, huwaonyesha wao kama
waajiriwa. Baada ya hapo ni kufuata amri zao, ndiyo maana unaona wasanii
wanakejeliwa hadi kuwekwa mitandaoni eti wanawaomba misamaha mameneja
wao. Inatisha!
Ukweli mmoja ambao wasanii wetu wanashindwa kuelewa ni kwamba wao
ndiyo mabosi, wao ndiyo hasa wanapaswa kunyenyekewa. Meneja hawezi
kuingiza hela kama msanii hapati shoo, hauzi kazi zake wala hapati
matangazo. Kazi ya meneja ni kutafuta kazi, akishapata anarudi kwa bosi
wake na kuweka mezani mazungumzo ya masilahi. Ni wajibu wa msanii
kukubali au kukataa kutegemea na jinsi anavyojichukulia.
Lakini huku ni kinyume chake, meneja anazungumza kila kitu kuhusu
kazi na masilahi, msanii wetu anaambiwa tu panda jukwaani, malipo yako
haya hapa!Nimegundua kwa nini wasanii wetu wengi wanaendelea kuwa kama
walivyo baada ya kuongea na mmoja kati ya mameneja wa msanii Nasibu
Abdul ‘Diamond’ anayeitwa Babu Tale.
Kama tunavyojua, juzikati dogo alikutana na msala kule Ujerumani,
baada ya kuchelewa kuingia ukumbini kwenye shoo yake na mashabiki, wengi
wao wakiwa ni raia wa Afrika Mashariki, walipolianzisha na kusababisha
uharibifu mkubwa wa mali. Ilikuwa ni halali yao kufanya fujo, kwa sababu
licha ya kukata tiketi na kuingia ukumbini saa nne usiku, Diamond
alitokea ukumbini saa kumi usiku!
Sasa nikampigia ili kusikia anasemaje juu ya tukio hilo, hasa baada
ya kuwepo kwa habari kwamba promota aliyemualika Diamond huko Ulaya
(Tunaambiwa Mnigeria flan mjanjamjanja) alipaswa kulipa hasara
iliyopatikana pamoja na kijana wetu.
Nikiri pia kwamba nimeanza kumsikia siku nyingi Babu Tale, kipindi
kile cha ujio wa Tip Top Connection, ingawa sijawahi kufanya naye
kazi.Aliniambia hivi: “Kipromosheni hii ni nzuri sana kwa sababu
itamtangaza sana, kiasi cha watu kutaka kujua hivi Diamond ni nani, na
kazi zake ni zipi.”
Sijasomea biashara na matangazo, kwa hiyo sina uhakika na uhalali wa
kauli hiyo, lakini kwa uzoefu wangu katika uandishi, maneno haya yana
maana zaidi kuliko Babu Tale anavyotaka watu waelewe.
Kama
ningekuwa yeye, kwa maana ya kiongozi wa Diamond, ningependa kujua nini
kilitokea na sababu za kutokea kwake. Mkataba wa awali ulimpasa kupanda
jukwaani saa sita, kwa nini alikubali apandishwe saa kumi?
Meneja unashangiliaje vurugu zilizosababishwa na msanii wako,
ukiamini kwamba zinamtangaza? Mtu asiyejua kilichotokea anayemhitaji
Diamond, hawezi kuamini kuwa haheshimu mikataba, ni mwenye kuchelewa
kwenye shughuli hadi kusababisha maafa?
Kama meneja anaamini msanii kutangazika vizuri kwa mambo mabaya,
tunashindwa vipi kuamini kuwa wao ndiyo waratibu wa skendo za mara kwa
mara zinazowakumba wasanii wao?
Wasanii wetu kadiri wanavyokua kimuziki na kiakili, wanapaswa pia
kuangalia aina ya watu wanaofanya nao kazi kulingana na levo waliyopo.
Kama skendo zinamtangaza msanii, hiyo bado inaweza kuwa siri ya ndani,
lakini mbele ya hadhara, ni lazima meneja asimame na kulaani kuwa
kitendo kama vurugu kwenye shoo, kimemharibia sana msanii wake na
atakuwa makini zaidi katika siku zijazo ili asifanye kazi na watu kama
hao, angalau kwa kuzuga!
No comments:
Post a Comment