UTAFITI
mbalimbali uliokwishafanywa unaonyesha kuwa magonjwa mengi ya saratani
(cancer) yanatokana na vyakula tunavyokula kila siku katika maisha yetu.
Katika siku za hivi karibuni, ongezeko la magonjwa haya limekuwa kubwa
kwa sababau vyakula vinavyosababisha magonjwa hayo, ndivyo vinavyoliwa
sana kuliko vile vinavyozuia.
Wiki
iliyopita tuliwaorodheshea baadhi ya vyakula vinavyoaminika kusaidia
kuzuia magonjwa ya kansa ambapo wiki hii tunawaletea orodha ya vyakula
vinavyoaminika kuongoza kwa kuwa chanzo cha magonjwa hayo hatari:
VYAKULA VYA KUKAANGA
Vyakula
vingi vinavyotayarishwa kwa kukaangwa kwenye mafuta yenye moto mkali
huwa na madhara kiafya na miongoni ma madhara hayo ni pamoja na
kusababisha kansa ya kwenye mfuko wa uzazi. Vyakula hivyo ni pamoja na
chips na vyakula vingine vinavyopikwa kwa kukaangwa kwenye mafuta.
VYAKULA VYENYE CHUMVI NYINGI
Vyakula
vyenye chumvi nyingi vimebainika navyo kusababisha kansa. Vile vile
inaelezwa kuwa chumvi huwa kama chakula kwa bakteria wa kansa tumboni.
Kansa ya tumbo inadaiwa kuua watu wengi nchini Japan kutokana na jamii
hiyo kupenda sana vyakula vyenye chumvi nyingi. Miongoni mwa vyakula
vyenye chumvi nyingi ni vile vya kusindika, kama vile nyama za makopo,
maharage, n.k
SUKARI
Matumizi
mabaya ya sukari yanaelezwa kusababisha kansa. Kama tujuavyo, kuna aina
mbalimbali za sukari lakini sukari hatari zaidi ni zile zinazowekwa
kwenye vinywaji mbalimbali, zikiwemo soda, juisi za ladha ya matunda
ambazo huwa na kiwango kingi cha ‘fructose’ ambayo inaelezwa kusababisha
saratani ya kongosho.
Vile
vile sukari kwa ujumla wake hairuhusiwi kutumiwa na mtu ambaye tayari
amegundulika kuwa na kansa kwa sababu chakula cha chembechembe za
saratani mara nyingi huwa ni sukari. Kwa matumizi mengine ya kawaida,
sukari inatakiwa kutumiwa kwa kiwango kidogo sana katika vinywaji au
vyakula tunavyotumia, tofauti na baadhai ya watu wanavyoweka sukari
nyingi ili kupata utamu zaidi.
NYAMA ILIYOIVA SANA
Upikaji
wa nyama kwa muda mrefu na kwenye moto mkali (high temperatures)
husababisha aina fulani ya kemikali inayojulikana kitaalamu kama
‘heterocyclic aromatic amines’. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na
Chuo Kikuu cha Utah (University of Utah), umeonesha kwamba watu
wanaopenda kula nyama zilizoiva sana, wako hatarini zaidi kupatwa na
saratani ya njia ya haja kubwa (Rectal Cancer). Hivyo inashauriwa
unapopika nyama, usipike kwenye moto mkali na kuiva kupita kiasi.
POMBE
Unywaji
wa pombe kupita kiasi nao unaelezwa kusababisha aina nyingi ya
saratani, kwa wake kwa waume. Aina ya saratani zinazodaiwa kusababishwa
na pombe ni pamoja na satarani ya mdomo, ini, utumbo na koromeo, ambazo
ndizo zinazoua watu wengi hivi sasa nchini Marekani.
NYAMA NA MAFUTA
Utafiti
uliofanywa na Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, umegundua kwamba
watu wanaopenda kula nyama kila siku wako hatarini kupatwa na saratani
ya utumbo kuliko wale wanaokula mara moja moja. Pia baadhi ya mafuta ya
wanyama na yale yanayowekwa kwenye ‘baga’ au ‘cheese’ huweza kusababisha
kansa.
Vile
vile ulaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa kuchanganya na nyama
zilizosindikwa au kuhifadhiwa kwa matumizi ya muda mrefu husababisha
saratani pia. Vyakula hivyo ni pamoja na ‘soseji’ ambazo hupendwa na
watu wengi. Pia mikate ya nyama ‘hot dogs’ nayo ni chanzo cha magonjwa
ya saratani.
VYAKULA VYA UNGA MWEUPE
Vyakula
vyote vinavyopikwa kutokana na unga uliokobolewa na kuondolewa
virutubisho vyake vyote na kuwa mweupe, vinaelezwa kuchangia magonjwa ya
saratani kwa kiasi kikubwa. Vyakula hivyo ni pamoja na ‘donati’
(doughnuts), maandazi, mkate mweupe, n.k
Mwisho,
licha ya kuepuka ulaji wa vyakula vilivyotajwa hapo juu, unatakiwa
kuzingatia ulaji wa vyakula asilia vitokanavyo na mimea, mboga za majani
na matunda kwa wingi kila siku. Utaona kwamba adui mkubwa wa afya zetu
ni vyakula vyote vya kusindika na vile vya kutengenezwa viwandani au
vile ambavyo wakati wa utayarisjaji wake huondolewa virutubisho vyake
vya asili.
No comments:
Post a Comment