Karume amtembelea Mansour kituo cha Polisi
Aliyewahi kuwa Waziri wa SMZ, Mansour Yusuph Himid ambaye alikamatwa na
silaha mbili za moto na risasi 412, nyumbani kwake Chukwani hivi
karibuni.
Zanzibar. Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani
Abeid Karume jana alifika Kituo cha Polisi Madema kumjulia hali shemeji
yake, aliyewahi kuwa Waziri wa SMZ, Mansour Yusuph Himid ambaye
alikamatwa na silaha mbili za moto na risasi 412, nyumbani kwake
Chukwani hivi karibuni.
Karume alifika katika kituo hicho ambacho ni Makao Makuu ya Polisi Mkoa
wa Mjini Magharibi saa 5.30 asubuhi na kumjulia hali Himid ambaye
amewekwa mahabusu akisubiri uchunguzi wa polisi dhidi ya tuhuma
zinazomkabili.
Habari za uhakika kutoka ndani ya polisi zinadai kuwa Rais Karume
alizungumza na shemeji yake kwa muda usiopungua dakika tano na kumtaka
kuwa mstahimilivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na utaratibu wake.
Viongozi wengine waliofika katika kituo hicho ambacho kimeimarishwa
ulinzi tangu alipofikishwa juzi, ni pamoja na wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kutoka CUF; Hija Hassan Hija (Kiwani), Saleh Nassor Juma
(Wawi), Hassan Hamad Omar (Kojani ) na Naibu Waziri wa Maji, Nishati,
Makazi na Ardhi, Haji Mwadini Makame ambao walimpa mkono wa pole 6.30
mchana.
“Mansour anastahili pongezi na siyo kupewa pole, inashangaza mambo ya
ulinzi na usalama ni ya Muungano kwa nini upande mmoja uruhusiwe
kumiliki silaha na upande mwingine uzuiwe, ndiyo maana tunasema Zanzibar
haitendewi haki,” alisema Hija muda mfupi baada ya kutoka kituoni.
Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuendelea na operesheni ya
kuwasaka viongozi wengine wanaomiliki silaha na kuwafikisha katika
vyombo vya sheria kwa vile tukio hilo limewafunza mambo mengi na kutaka
haki itendeke.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi
alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na matokeo yake
ndiyo yatakayoamua wapi pa kufunguliwa mashtaka kati ya Zanzibar au
Tanzania Bara.
“Kwa mujibu wa sheria za Zanzibar, hairuhusiwi raia yeyote kumiliki bastola,” alisema.
Himid alipekuliwa nyumbani kwake juzi baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za kiintelejensia kuwa anamiliki silaha za moto.
Taarifa kutoka katika eneo la tukio zinaeleza kuwa kazi ya upekuzi wa
nyumba mbili zilizopo katika eneo moja ilifanywa kwa kutumia mashine
maalumu.
Chanzo: Mwananchi |
No comments:
Post a Comment