Alexander Msowoya (35), ambaye ni mkazi wa Chang’ombe, jijini Dar es
Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni akikabiliwa na
shtaka la kumteka nyara askari wa kike wa usalama barabarani.
Akiwa
anaendesha gari, mshtakiwa huyo anadaiwa kumteka Kostebo Ester katikati
ya maeneo ya Tameke na Chang’ombe kabla ya kukamatwa maeneo ya katikati
ya Mabibo na Ubungo baada ya msako mkali wa polisi waliokuwa wakitumia
redio za upepo.
Hati
ya mashtaka iliyosomwa mbele ya hakimu Mwanaidi Ngoda ilidai kuwa Julai
11, mwaka huu, saa 9:00 alasiri, eneo la kati ya Temeke na Chang’ombe,
mshtakiwa alimteka nyara askari polisi Konstebo Ester, alipotakiwa
kuonyesha leseni yake.
Ilidaiwa
kuwa Afande Ester alimkamata mshtakiwa huyo akiwa anaendesha gari lenye
namba za usajili T 495 BKJ na kumtaka aonyeshe leseni yake, lakini
hakufanya hivyo.
Baada
ya hapo, ikadaiwa kuwa trafiki huyo wa kike akamwamuru dereva huyo
aliyekuwa anaendesha gari aina ya Rav4 ya rangi ya bluu kuweka gari lake
pembeni, lakini alikaidi kwa kudai ana haraka.
Kutokana
na hali hiyo, ilidaiwa kuwa askari aliingia ndani ya gari kwa kupitia
kwenye mlango wa nyuma na kuamuru waende kwenye kituo cha polisi
Chang’ombe.
Hata
hivyo, ilidaiwa kuwa badala ya kuelekea alikoelekezwa, mshtakiwa
alianza kwenda anakokujua yeye, hivyo kukiuka amri halali ya polisi na
kitendo hicho kuhesabika kama ni utekaji nyara.
Awali,
kabla ya kesi hiyo kusomwa, askari polisi mmoja alimwambia mwandishi wa
habari hizi kuwa kilichomuokoa afande Ester ni redio ya mawasiliano
aliyokuwa nayo, ambayo kwa kiasi kikubwa ilifanikisha kujua walipo na
wanakoelekea.
Hivyo, walikuwa wakifanya mawasiliano na askari wengine waliokuwa maeneo mbalimbali gari linapopita na ikasaidia kukamatwa.
“Afande amepumzika nyumbani kwake. Kwa sasa hali yake si nzuri ana presha kutokana na tukio hili,” alisema askari mmoja wa kiume mahakamani hapo, ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Hata
hivyo, alidokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kesi hiyo ikapelekwa kwenye
mahakama za juu kutokana na uzito wake, kwani ni ya utekaji nyara.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo na kupelekwa rumande. Kesi hiyo imepangwa kuendelea tena Julai 27, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment