TIFU! Ni dhahiri kuwa sasa, staa wa filamu za
Kibongo, Rose Ndauka na Rais wa Bendi ya Mashujaa Musica, Charles
Gabriel ‘Chaz Baba’ wapo kwenye bifu zito.Habari kutoka kwa chanzo chetu
zinasema kuwa, chanzo cha bifu hilo ni fedha, ambapo Rose alikodisha
gari la Chaz Baba kwa ajili ya matumizi yake lakini akalirudisha likiwa
limeharibika na kumuomba Chaz alitengeneze kisha angemlipa fedha zake,
lakini hakufanya hivyo.
“Alikodi gari kwa Chaz, lakini aliporudisha lilikuwa bovu, akamuomba
Chaz alitengeze angemlipa, baada ya hapo akaingia mitini. Chaz
alikasirika sana, maana hata Rose alipopigiwa simu alikuwa hapokei.
“Imefikia hatua Chaz ametoa kiapo kibaya, amesema hata akifa, maiti yake
isizikwe mpaka Rose alipe fedha zake kwanza,” kilitiririka chanzo
hicho.
Akizungumzia ishu hiyo, Chaz alisema, kitu alichokifanya Rose si kizuri na kamwe hawezi kumsamehe mpaka amlipe fedha zake.
Huyu hapa anafafanua zaidi: “Unajua Rose alikuja kwangu na kukodi
gari yangu aina ya Toyota Noah, akarudisha likiwa halitamaniki kabisa,
nilipomwuliza akasema walipata ajali, nikamtaka akalitengeneze, akasema
hana pesa kwa hiyo nitengeneze atanilipa.
“Tangu siku hiyo sijaona simu yake wala meseji, hata nikimpigia
hapokei. Nimeingia hasara ya kwenda kutengeneza kwa shilingi laki tano,
pesa yangu inaniuma, nataka anilipe.
“Hata kama nikifa leo, maiti yangu isizikwe mpaka Rose alipe haki
yangu kwanza. Akitangulia yeye utaratibu utakuwa hivyo sitokubali azikwe
hadi ndugu zake wanilipe fedha zangu,” alisema Chaz Baba.
Baada ya
kupata habari hiyo Risasi Jumamosi lilimhoji Rose kulikoni ameshindwa
kulipa deni la watu hadi mdai anatoa kiapo kibaya kama kile, akaruka
vikali.
“Ni kweli kabisa mimi nilikodi gari ya Chaz nikawa natembelea na
ilivyokuja kuharibika nililitengeneza mimi na kwenda kumkabidhi lakini
hakuridhika na namna lilivyotengenezwa ndiyo maana anasema ananidai
lakini mimi sijui hilo deni,” alisema Rose.
No comments:
Post a Comment