16 July 2014

MAKAVU LIVE: LAZIMA UKAE...HIVI CHID BENZ HUU NI USHAMBA AU JELA INAKUITA?!SHTUKA....

Rashid Makwilo ‘Chid Benz’.
KWAKO,
Rashid Makwilo ‘Chid Benz’. Naamini utakuwa mzima wa afya njema, kama ndivyo unajisikiaje ukiwa mzima wakati kuna wenzako wanalia na afya zao si nzuri kwa sababu yako?


Lengo la kukuandikia barua hii ni kukuweka sawa ingawa nakumbuka mara kadhaa, waandishi mbalimbali wenye nia njema na wewe waliwahi kuandika makala za kukuweka sawa.

Matukio yako ya kupiga watu kila siku si ya kufumbiwa macho kabisa. Tena ingekuwa bora ungekuwa unagombana na wanaume wenzako, lakini wewe unaowaonea watoto wa kike!

Kama una nguvu kwa nini usiombe pambano na Francis Cheka akuonyeshe kazi? Wewe si bondia? Ukorofi huchafua status ya mtu. Inawezekana unajiona mjanja lakini kumbe unafanya mambo ya kijinga. 

Hivi juzi tu, ulimshushia kipondo Aisha Kibuye, ambaye inaelezwa ni shabiki wako. Ulimpiga hadi ukasababisha akawa anazimia kila wakati. Sitaki kuzungumzia hilo sana maana ni jambo lililofikishwa mbele ya mahakama. 

Lakini nikuulize, raha yako ya kupiga wenzako ni nini? Juzi tena, umemfuata mwanamuziki mwenzako, Ray C nyumbani kwake na kumpiga.
Hao nimewatolea mfano maana ni matukio yaliyoripotiwa, si ajabu huko mtaani una matukio kibao ya kupiga watu. Hivi ni ushamba au jela inakuita? 

Kila kukicha unaleta vurugu na wasanii wenzako. Umegombana na wengi kwenye kumbi mbalimbali za starehe. Ni nini unatafuta ndugu? Inatakiwa ujichunguze upya na ubadilike kabla makubwa hayajakukuta! 

Sijajua kinachokusumbua ni nini! Ni utoto? Wewe si mtoto, maana una zaidi ya miaka 18, tena zaidi ya miaka 25! Utoto wako upo wapi?
Tuseme labda ushamba! Lakini nikifikiria ushamba, pia sikupati maana wewe ni mtoto wa mjini, tena uliyezaliwa jijini Dar es Salaam, eneo la wajanja wa mji – Ilala. Ushamba wako unatokea wapi? 

Inawezekana ni ugeni wa ustaa, labda hukutarajia kuwa msanii na ukajulikana, kwa hiyo umefura kichwa na unajiona unaweza kupigana au kumpiga yeyote kwa sababu wewe ni staa. Acha kujidanganya! 

Hakuna aliye juu ya sheria. Amini maneno yangu na ni vyema kama utayafanyia kazi mapema, vinginevyo utaja nikumbuka ukiwa nyuma ya nondo. Jela si nzuri ndugu, kuwa makini.
Usanii siyo ugomvi. Zinduka ndugu, dunia imebadilika. Magonjwa mengi, watu wanatembea na maradhi yao, utakuja mpiga mtu ngumi moja, anaanguka na kukata kauli, anafariki - utakuwa mgeni wa nani? 

Kama ni wa kusikia utasikia, kama ni sikio la kufa, basi baki na tabia yako ya hovyo ila siku yakikikuta utakumbuka. Ni bora nimekuambia, kuliko kukuacha ukazidi kupotea!
Wenye lugha yao wanasema: “Asiyefunzwa na mamaye, ulimwengu utamfunza!” kazi kwako.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname