06 July 2014

HUYU NDIYE SHEIKH ALIYELIPULIWA KWA BOMU ARUSHA

Sheikh wa Msikiti wa Qiblatan, Sood Ally Sood (37), uliopo Kilombero jijini Arusha amelipuliwa na bomu la kurusha kwa mkono akiwa nyumbani kwake wakati wakila daku hapa akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mt. Meru, alijeruhiwa miguuni na mapajani.
Shekhe Muhaji Hussein Kifea alijeruhiwa miguu na mapajani akiwa kitandani baada ya kutibiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo akiwajulia hali majeruhi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha, SACP Liberatus Sabas akiwajulia hali mashekhe hao.
 

Sheikh wa Msikiti wa Qiblatan,Sood Ally Sood (37) uliopo Kilombero jijini hapa amejeruhiwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono alipokuwa akila daku nyumbani usiku wa kuamkia jana.
Pamoja na Sheikh Sood, mtu mwingine aliyekuwa nyumbani kwake,aliyetajwa kwa jina la Muhaji Kifea (38) mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam pia amejeruhiwa katika tukio hilo na wote wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa matibabu.



Sheikh alijeruhiwa miguu yake yote na mapajani huku Kifea akipata majeraha makubwa miguuni na kupoteza baadhi ya vidole vya miguu yote.



Akizungumza hospitalini hapo, Sheikh, Sood alisema tukio hilo lilitokea nyumbani kwake eneo la Majengo ya chini, usiku wa kuamkia jana saa 5:00 wakati yeye pamoja na mgeni wake walikuwa wakila chakula sebuleni.



“Nikiwa sijui hili wala lile nilishtushwa na mlipuko ulioambatana na vyuma mbalimbali vilivyokuwa vikiruka hewani ambapo bomu hilo linaelezwa kuwa ni guruneti lililorushwa kupitia dirishani baada ya watu wasiofahamika kufanikiwa kuvunja kioo cha dirisha la chumba tulichokuwamo,” alisema Sheikh Sood.



Alidai anawajua waliotekeleza shambulio hilo kwa sababu amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu anaowafahamu na tayari alikuwa ametoa taarifa kwa vyombo vya dola.



Alisema kuwa siku tatu kabla ya tukio hilo alikoswakoswa kupigwa risasi na watu wasiofahamika wakati akitoka msikitini na akatoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha kuhusu tukio hilo. Sood anasema kuna baadhi ya vijana anawatuhumu juu ya matukio hayo.



Sheikh huyo ambaye ni Kiongozi wa dhehebu la Answar sun Kanda ya Kaskazini amekuwa akitofautiana na waumini wenzake kutokana na msimamo wake wa kutokukubaliana na baadhi ya waumini wenye msimamo mkali wa msikiti huo.



Mkuu wa Mkoa wa Arusha,  Magesa Mulongo alikemea matukio ya mabomu yanayolitikisa Jiji la Arusha katika siku za karibuni na kuviagiza vyombo dola kufanya uchunguzi wa kina kubaini wahusika wote ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.



“Uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hili limetekelezwa na watu walio karibu na Sheikh. Polisi wanaendelea na uchunguzi kwa sababu baadhi ya watu wanaotajwa kuhusika kwenye tukio hili pia ni miongoni mwa watuhumiwa kwenye matukio mengine ya milipuko ya bomu Arusha,” alisema Mulongo.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatusi Sabasi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa majeruhi wanaendelea vyema huku polisi wakiendelea na uchunguzi wa kina kuwabaini wahusika.



Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alielezea kusikitishwa na matukio ya milipuko ya mabomu Arusha na kuliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwakamata wahusika bila kujali vyeo, nyadhifa, dini, itikadi wala rangi zao.



“Arusha tunapita katika kipindi kigumu sana. Kwanza tulishuhudia mlipuko wa bomu kanisani, ikafuatiwa na lile la mkutano wa hadhara wa Chadema, kabla ya mwingine kulipuka kwenye baa na sasa nyumbani kwa Sheikh,” alisema Lema.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname