BAADA ya kuzikosa tuzo za MTV Africa na BET, hatimaye
mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, usiku wa kuamkia jana
Jumapili ametwaa tuzo mbili kupitia African Music Magazine Awards au
AFRIMMA zilizotolewa huko Texas, Marekani.
Diamond ametwaa tuzo mbili za Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki na ya Wimbo Bora wa Kushirikiana.
Baada ya kutwaa tuzo hizo, Diamond amerudisha
shukrani zake kwa Rais Jakaya Kikwete akisema ndiye aliyempa nguvu ya
kufanya muziki kwa ari kutokana na mchango wake kwa sanaa nchini.
“Nakushukuru sana Rais Kikwete kwa mchango wako,
kijana wako nimefanya maajabu, lakini hii yote imetokana na mchango wako
kwa wasanii nchini, baada ya kiongozi wetu kuonyesha kuijali kazi yetu
na sisi imetupa moyo wa kufanya makubwa zaidi,” alisema.
Tuzo nyingine ya Diamond ni ile ya Wimbo Bora wa
Kushirikiana ambao ni ‘Number One remix’ alioufanya na Davido wa
Nigeria. Hata hivyo nyota huyo alisema ushindani uliopo sasa umemsaidia
kwa kiasi kikubwa kufika alipo na anaamini kwamba imetokana na michango
ya watu wengi.
“Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mama, familia,
uongozi wangu, kipenzi changu, vyombo vya habari bila kuwasahau
mashabiki wangu kwani siku zote wamekuwa wakiniunga mkono kwenye shida
na raha na pia wasanii wote wa ndani na nje ya Tanzania kwani changamoto
tunazopeana ndizo zilizotufikisha tulipo,” alisema Diamond.
Naye Meneja wa Diamond, Babu Tale aliyeambatana
naye Marekani alisema tuzo hizo ni ushindi mkubwa kwa Tanzania kwani
wamewapita wasanii waliokuwa wakiogopwa.
“Hii inadhihirisha tunaweza na tutafika mbali,
tumewashinda Mafikizolo, 2Face na wengine wengi. Tupo mbali na ni hatua
nzuri kwa muziki wa Tanzania,’’ alisema Babu Tale.
Nyimbo zilizokuwa zikiwania tuzo ya ‘kolabo’ bora
ni Single ya T Pain na 2 Face –’Rainbow’, ‘Khona’ ya Uhuru na Mafikizolo
wa Afrika Kusini, ‘Surulere remix’ ya Dk. Sid wa Nigeria, Mkenya Amani
ft. Waganda Radio na Weasel ‘Kiboko Changu’ J. Martins ft. Dj Arafat
‘Touching Body’ na Rebees na Wizkid ‘Slow Down’ Tuzo ya msanii bora wa
kiume Afrika Mashariki ilikuwa inawaniwa pia na Ben Pol kutoka Tanzania,
Bebe Cool wa Uganda, Wyre wa Kenya, Navio wa Uganda na Jackie Gosee wa
Ethiopia.
Mtanzania mwingine Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ au
Jide ameshinda tuzo ya msanii bora wa kike Afrika Mashariki aliyokuwa
anashindania na Rema wa Uganda, Aster Aweke wa Ethiopia, Avril wa Kenya,
Victoria Kimani wa Kenya na Irene Ntale wa Uganda.
Tuzo ya Mtayarishaji Bora wa video imekwenda kwa
Ogopa Dj’s walioitengeneza video ya kwanza ya ‘My Number 1’ ya Diamond
Platnumz. Tuzo hizi zilikuwa zinawaniwa na wasanii wa nchi 17
No comments:
Post a Comment