Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Mutungi.
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema
haitambui kuondolewa kwa kipengele cha ukomo wa uongozi uliofanywa na Chadema
bila kufuata idhini ya mkutano mkuu wa chama hicho.
Mwaka 2006, Katiba ya Chadema ilifanya marekebisho
yaliyoruhusu wanachama kugombea uongozi bila ukomo wakati awali, waliruhusiwa
kugombea kwa vipindi viwili vya miaka mitano.
Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, inasema kipengele hicho katika Ibara ya
6.3.2 (C) kiliondolewa kwenye katiba bila idhini na mkutano mkuu wa chama
hicho. Mutungi alisema baada
ya kupitia muhtasari wa kikao cha mkutano mkuu wa
mwaka 2006 suala la kuondoa kipengele cha ukomo wa uongozi halikuonyesha
kujadiliwa katika mkutano huo.Hata hivyo, akizungumza kwa simu jana, Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kipengele hicho kiliondolewa kwa
vikao vya chama ambavyo ni wilaya na mkoa.
“Mjadala kuhusu ukomo wa uongozi ulishamalizika na
haujadiliwi tena, ulishapitishwa na vikao halali vya chama, mkutano mkuu
ulipitisha yale yaliyoamuliwa na vikao vya chini,” alisema Dk Slaa.
Hata hivyo, Jaji Mutungi alisema: “Chadema wamefanya
mabadiliko bila kufuata katiba”
Alishauri waitishe mkutano rasmi na halali kwa mujibu wa
katiba ya chama hicho ili waweze kurekebisha kasoro zilizopo.Alisema kama chama
hicho hakitarekebisha kasoro hiyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haiwezi
kuitambua ibara hiyo.Alisema ingawa hoja hiyo iliwasilishwa na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba ambaye sasa si mwanachama
wake, bado hoja hiyo ni muhimu na inahitaji kufanyiwa kazi.
“Ni vizuri mkaifanyia kazi hoja hiyo bila kujali kwamba
aliyeiwasilisha si mwanachama tena wa Chadema,” alisema katika barua hiyo
No comments:
Post a Comment