UNASHANGAA mashabiki wa Simba wakiwa wako kimya pindi mpira
unapokuwa miguuni mwa Kevin Yondani wa Yanga katika mechi ya Taifa
Stars? Unashangaa mashabiki wa Yanga nao wakiwa kimya pindi mpira
unapokuwa kwa Amri Kiemba wa Simba katika mechi ya Stars? Basi wala
usishangae sana.
Hata Brazil ipo vivyo hivyo. Jana Alhamisi
kulikuwa na pambano kati ya Brazil na Croatia. Hali hiyo ilitazamiwa
kuwepo pindi mambo yanapokuwa magumu kwa upande wa Brazil. Nilikuwa
nimekaa kijiwe kimoja cha jioni chenye mashabiki wa nchi mbalimbali na
nikapata simulizi.
China Keya, kiungo wa zamani wa Pan Afrika ambaye
anaishi hapa amenisimulia mambo yanavyokwenda ovyo pindi maisha ya timu
ya taifa ya Brazil yanapokuwa magumu uwanjani, hasa timu yao inapocheza
katika Jiji la Sao Paulo.
“Timu ya taifa ya Brazil inakuwa katika wakati
mgumu pindi inapocheza soka hapa Sao Paulo. Mashabiki wa soka wa Sao
Paulo hawana uvumilivu hata kidogo. Mechi ikifika dakika ya 20 bila ya
bao, wanaanza kuwazomea taratibu wachezaji wao,” anasema China. “Lakini
pia mashabiki wa hapa wakati mwingine wanawashangilia wachezaji kutokana
na timu wanazochezea. Kwa mfano, kama kipa akikaa Julio Cesar na timu
haifanyi vizuri basi wanaanza kulitaja jina la kipa Rogerio Ceni. Kila
Cesar akigusa mpira wanalitaja jina la Ceni.”
“Ceni ni kipa wa Sao Paulo, timu inapocheza katika
Jiji la Sao Paulo ndiyo wanamkumbusha kocha kwamba Ceni ndiye
anayepaswa kukaa langoni na si kipa mwingine yeyote. Maisha ya Brazil
jijini Sao Paulo ni magumu.
“Wakati mwingine mpira akiugusa Neymar wanazomea
na kulitaja jina la Lucas Moura (wa PSG). Ni kwa sababu Lucas amezaliwa
eneo hili hili la Sao Paulo. Neymar amezaliwa Sao Paulo lakini yeye
anatoka kitongoji cha Santos ambacho kipo kando kidogo.
“Fred naye aliwahi kufunga bao katika mechi ya
kirafiki na kwenda upande wa mashabiki wa timu pinzani ndani ya Brazil
huku akiwaonyesha ishara ya sikio kuwasikiliza kama wanaweza kunyamaza
na kelele zao za kumzomea.” Anamaliza China.
Hapa simulizi zinazidi kunoga zaidi. Majuzi Neymar
alilazimika kuongea na vyombo vya habari vya Brazil kuwasihi raia wa
Brazil kuacha kushangilia wachezaji kutokana na timu wanazochezea.
Kuelekea katika mechi yao ya jana dhidi ya
Croatia, ungeweza kuona ni kwa kiasi gani Wabrazili wanaipenda timu yao.
Mazungumzo yote yalikuwa ni namna ya kuifunga Croatia.
Biashara kubwa zaidi kwa sasa ni jezi namba 10 ya
Neymar, rangi za kuchora bendera ya Brazil usoni, tarumbeta zao ambazo
hazina kelele sana kama Vuvuzela.
Unadhani Waingereza wanaipenda na kuipamba sana
timu yao? Hapana. Hawawazidi Wabrazili. Tatizo kubwa la Tanzania na
ukanda wa Afrika Mashariki ni kupokea taarifa nyingi kutoka katika
vyombo vya Uingereza. Lakini Wabrazil ni kiboko!
Timu inapokwenda kula chakula cha mchana kituo
maarufu cha Televisheni cha hapa, Global Sports kinaweka tukio hilo
laivu. Timu ikiwa inatoka katika korido ya hoteli kupanda katika basi
kwa ajili ya kwenda mazoezini tukio hilo linawekwa laivu katika
televisheni
No comments:
Post a Comment