Kama hujui, wanaume ni wambea zaidi ya wanawake, tofauti ni kwamba wao hawasutani hadharani!
Katika
jamii yoyote mtu mwenye tabia ya umbea huchukiwa, hutengwa na hata
wakati mwingine hupigwa kwa kuonekana kuwa ni chanzo cha migogoro na
huku viongozi wa dini wakimwona mtu wa aina hiyo kuwa ni mtenda dhambi.
Watu wanaopenda tabia ya umbea huenda wakawa wamepata mtetezi. Ripoti
iliyotolewa hivi karibuni kuhusu tabia ya watu kupenda kutumia muda
mwingi kusema mambo ya watu wengine, inasema tabia ya umbea ina manufaa
kiafya.
Ripoti hiyo iliyotolewa na watafiti kutoka chuo kikuu cha Rhode Island
cha Marekani, inasema kuwa watu wanaonufaika zaidi za tabia hiyo ni wale
wanaopenda kuongea mambo mabaya wa watu wengine kuliko wenzao
wanaopenda kuzungumza kuhusu mambo mazuri.
Wataalamu hao wamebaini kuwa iwapo mtu atatumia dakika 20 kuzungumzia
mambo mabaya ya watu wengine, anaweza kuimarisha afya yake kwa kupunguza
msongo wa mawazo, woga na mashaka kwa asilimia 96 kwa muda wa masaa
manne mfululizo.
Hata hivyo, wamebainisha kuwa mtu akitumia muda huo huo kuzungumza mambo
mazuri ya watu wengine, atapunguza msongo wa mawazo kwa asilimia 72
ikimaanisha kuwa watu wenye kuzungumza mambo mabaya ndio wenye kunufaika
zaidi.
Watafiti hao, wakifafanua hali hiyo wameelezwa kuwa mtu anapoongea
habari nzuri zinazowahusu watu wengine huuchochea ubongo kutaka
kujiunganisha na mtu anayezungumzwa, wakati yule anayezungumza habari
mbaya huwa kinyume chake.
Mtu anayezungumza habari mbaya anatabia ya kutokuhifadhi alichokisema,
bali huendelea na mambo yake kama kawaida, wakati anayezungumza habari
nzuri hukaa nazo moyoni kwa kipindi cha muda fulani.
Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Lusajo
Kajula anasema binadamu wote huongea kuhusu watu wengine, lakini umbea
ni zaidi ya maongezi.
Lusajo anasema asili ya mwanadamu ni kuzungumza japokuwa wakati mwingine
hujikuta akiishia kutoa mifano halisi ya maisha ya watu wengine na
hivyo kuingia katika mgogoro wakati mtu aliyesemwa anaposikia.
“Umbea ni kawaida na hauzuiliki, tatizo ni yaliyomo ndani ya umbea
ambayo mara nyingi hutegemea na mawazo mtu aliyonayo. Kama ana mawazo
hasi, ataongea mambo mabaya,” anasema Kajula.
Hata hivyo, Kajula anapingana na dhana iliyopo miongoni mwa watu kuwa
mwanamke ndiyo anayependa zaidi tabia ya kuzungumza mambo ya watu
wengine kuliko mwanaume.
“Kuna tafiti nyingi zinazoonyesha kuwa wanaume ni wambea zaidi kuliko
wanawake, ila wao hawasutani na pia hawawezi kujieleza vizuri kama
wanawake,” anasema Kajula na kuongeza kuwa kwa kawaida tabia ya kuongea
mambo mazuri yanayowahusu watu wengine hukusudia kukuza heshima ya mtu
anaezungumziwa.
Mwanasaikolojia na mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Nguvu ya Umbea’, Maria
Konnikova anasema hakuna mtu anaeweza kuukwepa umbea na kushauri kuwa
mtu asihangaike kutaka kuwazuia wambea kusema wayatakayo.
Anasema wataalamu mbalimbali wa masuala ya saikolojia wamebaini kuwa
umbea ni njia muhimu katika kuleta umoja na mshikamano katika jamii
kwani kwa kufanya hivyo husaidia kueneza taarifa ambazo wanajamii
wasingeweza kuzifahamu.
“Pia imebainika kuwa umbea ni zana nzuri ya kuifundisha jamii mtu gani
anafaa kuwa rafiki na yupi anastahili kuepukwa,” anasema Konnikova.
Mwanasaikolojia Homer Simpson wakati fulani aliwahi kusema: “Kama
hatutakiwi kula nyama kwanini wanyama waliumbwa kwa nyama? Kama kila mtu
anafahamu kuwa umbea ni mbaya kwa nini anasema? Jibu ni rahisi; katika
ubongo wetu kuna sehemu inayopenda umbea.”
Anasema kila mtu ananufaika na mambo mazuri yanayosemwa juu yake
anapoyasikia. “Wapi ungependa kufanya kazi, sehemu ambayo watu
wanakusema vibaya au vizuri?”anahoji Simpson.
Mchungaji wa Kanisa la Free Pentekosti Tanzania (FPCT) Njia Panda ya
Himo, Kilimanjaro, Elisante Ngailo, akizungumzia utafiti huo anasema
watu wanaotumia muda mwingi kuzungumza mambo mabaya yanayowahusu watu
wengine husema tu bila kufiria.
“Watu wa aina hii hawaumizi kichwa kufiri sana, wao husema mambo
walioyasikia au kuyaona, kisha kuendelea na maisha yao,” anasema Ngailo.
Anaongeza: “Lakini hawa watafiti wanataka kutuambia kwamba sasa tuwaseme
sana watu kusudi tupunguze msongo wa mawazo? Hili haliwezekani” anasema
Ngailo.
Kwa maoni yake si sahihi kwa watu kuwasema watu wengine vibaya na kwamba
tafiti kama hizi hazijengi jamii kwa kuwa tabia ya umbea inapingwa na
makundi mbalimbali ya watu.
Maoni ya watu mbalimbali
Roda Mgimwa mkazi wa Vingunguti anasema matokeo ya utafiti uliofanywa
kuhusu tabia ya umbea anakubaliana nao kwasababu watu wa aina hiyo
hawana hofu ya jambo wanalolizungumza.
“Wakati mwingine unaweza kumsikia mtu anasema umbea kuhusu mtu fulani
ndani ya daladala bila kujua iwapo yule anayesemwa ana ndugu yake hapo
au la. Kwa namna hii watu hawa hawawezi kusumbuliwa na msongo wa
mawazo,” anasema Roda.
Elia Mwamwaja mkazi wa Kongowe anasema matokeo ya utafiti huo yanaweza
kuwapa nguvu wambea kuwasema vibaya watu wengi zaidi hasa kila wakati
wanapohisi wanamsongo wa mawazo.
“Sasa kuna watu watatumia umbea kama dawa, wakihisi wanamsongo wa mawazo
watakuwa wanaanza kusema mambo mabaya hata kama sio ya kweli,” anasema
Mwamwaja.
Hata hivyo, Mwamwaja anatoa angalizo: “Kwa mtu ambaye hakuwa na tabia ya
umbea hawezi kuianza tabia hiyo leo kwasababu tu amesikia wanaofanya
hivyo wanaweza kupunguza msongo wa mawazo.”
No comments:
Post a Comment