Mfumo huo wa ununuaji wa stika zinazobandikwa
katika makasha ya kazi zinazoandaliwa na wasanii hao hutolewa na Mamlaka
ya Mapato Tanzania TRA ambayo imethibitisha jambo hilo, huku ikieleza
kuwa wanauza kwa pauni kwa sababu mtengenezaji wa stika hizo akaunti
yake ipo mwenye pauni, siyo shilingi.
Wakizungumza na MWANANCHI kwa nyakati tofauti wasambazaji wa
kazi hizo, wasanii na uongozi wa sanaa nchini walisema tangu kuanza
rasmi kwa mfumo huoJulai 2013, kumekuwa na hali ya sintofahamu kutokana
na stika hizo kuwa adimu na zinapopatikana kuuziwa kwa fedha za nje
kinyume na makubaliano ya serikali na wasanii juu ya mfumo huo.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff),
Simon Mwakifamba alisema stika hizo kuuzwa kwa pauni ni changamoto mpya
inayoukumba mfumo wa urasimishaji wa kazi za wasanii na kupoteza maana
nzima ya zoezi hilo.
“Limekuwa ni tatizo kubwa linalowakwaza wasanii
nchini hasa wasambazaji wa kazi hizo kutokana na gharama kubwa
wanayotumia sambamba na kukosa stika kwa wakati mwafaka,” alisema na
kuongeza;
“Mtu umeshajipanga kutoa kazi ziku mbili kabla,
ukienda TRA unaambiwa stika zimekwisha wakati tayari umeshachukua
mkopo benki yaani unakuwa umeongeza matatizo mengine juu.”
Mwakifamba alitoa wito kwa serikali kupitia Wizara
ya Viwanda na Biashara kuhakikisha inarekebisha mfumo huo uliopo sasa
ambao umeonekana kuwa kero kwa wasanii.
“Naona kutumia pauni ni kuongeza gharama kubwa ambayo isingeweza kufikiwa iwapo stika hizi zingeuzwa kwa fedha ya Tanzania.
“Kwa mujibu wa kiongozi wetu sidhani kama haya
ndiyo yalikuwa makubaliano yetu. Stika moja tunanunua kwa shilingi 14,
lakini unalipa kwa pauni na si shilingi ya Tanzania, hata hivyo
tunauziwa kuanzia stika 100 na si chini ya hapo.”
Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba
alisema, “Kubwa zaidi tunalolalamikia sisi kama wasambazaji na wasanii
ni kuuziwa stika hizi kwa fedha isiyo yetu, kwa nini iwe hivi, pauni
kila siku inabadilika mara inapanda mara inashuka.”
Novemba alisema, “Wasanii wa muziki wanalalamika
kuhusu hilo hasa wa muziki wa Injili. Wasanii wa muziki wa kizazi kipya
wameamua kukacha kabisa albamu kutokana na ukweli kwamba hawauzi, lakini
hata waliofurahia urasimishaji bado utata unakuja kwenye stika yaani
hakuna afadhali tulidhani tutapata haki, lakini sasa mambo ndivyo
sivyo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Five Effect, kampuni
inayojishughulisha na usambazaji wa kazi za wasanii, William Mtitu naye
alisema, “Kuna uhaba wa stika hata hivyo tunanunua kwa pauni, wasanii
tuliamua kusambaza kazi zetu wenyewe kutokana na tatizo la kutoendelea
na Mhindi anatunyanyasa siyo siri akinunua kazi yako humdai tena
anaitumia atakavyo.
Kigogo TRA ahamaki
Katika hali ya kushangaza Mkurugenzi wa Huduma na
Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard
Kayombo, alikana tuhuma hizo na kudai kwamba si kweli bali wasanii
wanauziwa stika hizo kwa shilingi za Tanzania.
“Taarifa hizo hazina ukweli wowote, stika zote
zinazouzwa hapa TRA zinauzwa kwa mfumo wa fedha za Tanzania na si fedha
za kigeni, hatujawahi kuwauzia wasanii stika kwa fedha za Uingereza
(pauni), waambie hao wanaosema hivyo wakuonyeshe risiti walizolipia kwa
pauni.”
Kauli ya wasambazaji
Uongozi wa Kampuni ya Steps Entertainment ambao
ndio wasambazaji wa kazi za wasanii walipotakiwa kuonyesha risiti ambazo
walilipia stika hizo kwa pauni badala ya shilingi ulisema, “Ni jambo la
kushangaza kama TRA wenyewe wanatulipisha kwa pauni kisha wanakana
haiwezekani, risiti tunazo ila zungumza na Afisa Utafiti Mwandamizi wa
TRA.”
TRA yathibitisha
Ofisa Utafiti Mwandamizi wa TRA, Ephraim Mdee
alithibitisha matumizi ya pauni ya Uingereza katika ununuzi wa stika za
wasanii na kutoa maelezo ya kwa nini mamlaka hiyo iliamua kutumia pauni
badala ya fedha za Tanzania.
“Ni kweli wasanii wanauziwa stika kwa pauni ya
Uingereza. Tulifanya hivi tukiwa na makusudi maalum kwa kawaida stika
hizi tunazinunua kutoka kampuni ya M/S Hague Cheque Security na stempu
moja inatengenezwa kwa pauni 0.00285,” alisema na kuongeza;
“Lakini gharama hii ukiigawanya kwa shilingi ya
Tanzania unapata shilingi 7 na hii unazidisha mara mbili na kupata
shilingi 14. Tuliamua kutumia pauni kutokana na tatizo la kupanda na
kushuka kwa fedha hiyo hata hivyo mtengenezaji akaunti yake ipo kwenye
pauni,” alisema Mdee.
Mdee alisema kuhusu suala la kutokuwepo stika kwa
wakati, ni tatizo lililojitokeza siku za awali baada ya kuanzishwa mfumo
huo. “Nadhani hicho ni kitu cha kawaida, inawezekana mteja akaja na
kununua nyingi.”
Wizara
Waziri wa Biashara na Viwanda, Abdallah Kigoda
alishangazwa na taarifa hizo huku akisisitiza kwamba hayakuwa
makubaliano yaliyopitishwa na bunge.“ Hili ni jambo nyeti na wizara yangu inaanza kulishughulikia haraka sana. Nakiri kwamba Wizara ya Fedha inapaswa kuangalia suala hili kwa umakini zaidi kwani wizara yangu haijalipitisha hilo na ninashangazwa kwa nini wasanii wanunue stika hizi kwa pauni?” alihoji Kigoda.
credit: Mwananchi
No comments:
Post a Comment