07 January 2014

HUYU NDIYE KAJALA MASANJA...MFAHAMU HISTORIA YAKE NA FAMILIA YAKE

HII ni safu mpya ambayo itakuwa ikizungumzia juu ya maisha ya kweli ya mtu yeyote maarufu. Itatokana na mahojiano ya ana kwa ana!

Kwa kuanzia, tunaye nyota wa filamu za hapa nyumbani, Kajala Masanja, ambaye kabla ya kujiingiza kwenye sanaa hiyo aliwahi kuishi kinyumba na mmiliki wa studio ya Bongo Records, Paul Matheas, maarufu kama P.Funk na kujaaliwa kupata mtoto mmoja aitwaye Paula.

Katika safu hii, Kajala ambaye amewahi kukutwa na misukosuko lukuki ikiwemo kuhukumiwa kifungo jela, anaelezea mambo mengi kuhusiana na maisha yake ambayo hakuwahi kuyaelezea kokote kule au katika chombo chochote cha habari.

“Nilizaliwa mwaka 1983 katika familia ya mzee Masanja na walijaaliwa kuwa na watoto wawili tu, mimi na mdogo wangu, Dorice. Sisi tuna tofauti kubwa sana ya umri kati yetu kwa vile tulipishana sana kuzaliwa. Wakati nikizaliwa, wazazi wangu ambao wote ni askari polisi, walikuwa wakifanya kazi na kuishi kituo cha Oysterbay jijini Dar es Salaam.
“Kutokana na kukaa muda mrefu utotoni nikiwa peke yangu, matokeo yake nilijikuta nikiishi kwa kudekezwa sana. Nilipofikisha umri wa miaka sita, nilipata shauku ya kuanza shule kwani nilikuwa nafurahi sana kuwaona watoto wenzangu wakipita pale wakienda na kurudi shuleni.

“Baada ya kuandikishwa Shule ya Msingi Mbuyuni, siku ya kwanza niliyotakiwa kwenda niliamka asubuhi na mapema na dada aliyekuwa akinilea alinivalisha nguo za shule na kunitaka sasa kusubiri chai kabla ya kunipeleka shuleni.


“Wakati dada akiipua chai ili animiminie kwenye kikombe, kwa bahati mbaya ilinimwagikia mapajani na kuniunguza sehemu kubwa ya mapaja yangu. Ikabidi wazazi wangu wafuatwe kituoni hasa kwa kuwa hakukuwa mbali na nyumbani, ambao walifika na kunipeleka hospitalini. Ndoto ya kusoma ikaishia hapohapo!


“Nilipofika hospitali, walinipa dawa na kila siku nilikuwa nikienda kuosha kidonda, hamu ya shule ikaniishia, nikawa mtu wa kulala tu, maana hata kutembea nilikuwa siwezi, kwani nilipohitaji kutembea nilibebwa na kufanyiwa kila kitu hadi nilipopata nafuu.


“Hali yangu iliendelea kuimarika hadi nilipopona kabisa na kuanza kwenda shuleni, ambako nilikutana na watoto wenzangu ambao tukajikuta tukijenga urafiki. Nilikuwa mpole mno, sikuwa mtu wa kuongea kabisa na mara nyingi watoto wenzangu wakorofi walipenda sana kunichokoza.


“Wakati huo nikisoma, mwalimu wangu wa darasa alikuwa Mama Salma Kikwete ambaye sasa ni first lady na nilikaa dawati moja na watoto wa Rais Kikwete, Ridhiwan na Miraji na kwa kweli walikuwa ni marafiki zangu wakubwa sana.


“Nakumbuka nilipofika darasa la sita, kuna msichana mmoja alipanga kunipiga yeye na marafiki zake kwa madai kuwa mimi nimemchukulia mchumba wake, maana kipindi hicho ni wadogo na kutokana na upole wangu niliwaambia mimi sijafanya hivyo wakaniambia kesho yake lazima wanipige, maana enzi hizo tukitaka kupigana, lazima iwe Ijumaa.


“Siku hiyo ilipofika, mama alikuja kuniamsha asubuhi kwa ajili ya kwenda shuleni, nikajifanya nimebanwa na tumbo, siwezi kuamka wala kutembea, akanitafutia dawa na kunipa ninywe kisha akaniambia nilale. Nilishukuru sana kwani siku hiyo niliepuka kipigo.


“Ilipofika Jumatatu nikaendelea na mambo yangu kama kawaida wala hawakunisemesha tena, lakini nilikuwa muoga sana, nilijua wakati wowote wanaweza kunivizia na kunipiga, lakini haikutokea ingawa hata mimi rafiki zangu walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kujibu mashambulizi.


“Niliendelea kusoma shuleni hapo kwa amani mpaka nilipomaliza darasa la saba. Wakati huo nilikuwa na rafiki yangu mmoja wa kiume ambaye kila siku jioni alikuwa akipita nyumbani. Baba yangu akamshtukia, siku moja alichukua manati yake aliyokuwa akiitumia kuwapigia kunguru, alipopita akampiga nayo!
“Kufuatia kitendo hicho, rafiki yangu yule hakupita tena nyumbani na akatokea kunichukia sana kwa ajili ya kitendo alichofanyiwa, wakati wa kuanza sekondari ulipofika, nilipelekwa Songea katika shule ya masista kwa hofu kuwa nikisoma mjini nitaharibika kimaadili.

“Nilipoanza masomo shuleni hapo, nilikuwa mpweke sana maana sikuwahi kukaa mbali na wazazi wangu, halafu kulikuwa na baridi sana kitendo kilichosababisha nisiwe naoga kabisa na kujikuta nikipata ukurutu kwa uoga wa kuoga maji ya baridi.”

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname