20 December 2013

OKWI APOKELEWA KAMA MFALME NA MASHABIKI WA YANGA..!!POLISI WATUMIKA KUTULIZA MZUKA WA WANA JANGWANI


 Mashabiki wa Yanga wakiwa na bashasha wakati wakimsubiri Emmanuel Okwi.
 Baadhi ya mashabiki wa Yanga wakiuza jezi zenye jina la Okwi.
 Okwi wa tatu kulia akiwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, leo.
 Mashabiki wa Yanga wakiwa katika mstari kumsubiri Okwi.
 Mashabiki wa Yanga.
 Okwi akiwasili.
 Okwi akisindikizwa na askari pamoja na mashabiki kuelekea katika gari lake.
 Okwi akitabasamu baada kupata mapokezi makubwa.
 Mashabiki wakimlaki Okwi.
 Shabiki wa Yanga, Steven akiwa na Okwi.
 Mashabiki wakisukuma gari alilopanda Okwi.

DAR ES SALAAM, Tanzania

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, aliyesaini mkataba wa kuichezea Yanga kwa miaka miwili na nusu, leo ametua kwa kishindo na kulakiwa na mamia ya wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo.

Okwi aliyewahi kuichezea Simba kwa mafanikio makubwa kabla ya kujiunga na Etoile du Sahel ya Tunisia, Januari mwaka huu, aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam majira ya saa 10 jioni.
.
Baada ya kupokewa na viongozi wa Yanga na kuzua hekaheka hasa wakati nyota huyo anatoka uwanjani hapo kuelekea kupanda gari, alisema ametua Jangwani kikazi zaidi na usajili wake, litashughulikiwa na viongozi wa Yanga pamoja na Shirikisho la soka Uganda (Fufa).

Kuhusu Simba, Okwi alisema anaiheshimu kwa sababu alifanya nao kazi vizuri, wamemlea, lakini kwa sasa yeye ni mali ya Yanga na kuongeza kuwa yu fiti kucheza mechi ya kesho kama akipangwa.

“Nimekuja Yanga kufanya kazi, suala la usajili wangu litashughulikiwa na viongozi wa pande zote. Naiheshimu Simba, nimefanya nao kazi vizuri, wamenilea na kuniheshimu, ila sasa ni mali ya Yanga” alisema Okwi.  
Akizungumzia ujio wa Okwi, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema wamefanikisha usajili huo wa kihistoria baada ya kukamilisha taratibu muhimu ikiwemo kupata hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC).

Usajiliwa kwa Okwi, unaifanya Yanga kufunga idadi ya nyota watano wa kigeni wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni, akiungana na Mganda mwenzake Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Didier Kavumbagu.

Kizuguto amewasihi wanachama, wapenzi na washabiki kuwapa ushirikiano wachezaji wote wa zamani na wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili.

Nyota wengine waliosajiliwa hivi karibuni katika kuimarisha kikosi cha Yanga kuelekea raundi ya pili ya Ligi Kuu na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni Juma  Kaseja (huru) na Hassan Dilunga kutoka Ruvu Shooting.

Okwi alitua SC Villa akitokea Etoile du Sahel ya Tunisia ambayo Januari mwaka huu ilimnunua kutoka Simba kwa dola za Kimarekani 300,000, lakini akiamua kuachana na klabu hiyo na kurejea kwao Uganda, kwa madai hakulipwa mishahara kwa miezi mitatu.

Kuna habari kuwa, Etoile hadi sasa haijailipa Simba SC fedha zake za kumnunua nyota huyo ambaye sakata lake lipo Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Baada ya Okwi kutocheza kwa miezi sita, Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa) lilimpigania aruhusiwe kuichezea SC Villa ya huko kunusuru kiwango chake.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname