Msanii wa Uganda, Moses Ssali aka Bebe Cool ameshinda kesi
iliyohusu tukio la kufyatuliwa risasi na polisi miaka mitatu iliyopita,
hivyo mahakama kuu ya Uganda imeamua alipwe kiasi cha pesa za Uganda
zenye thamani ya zaidi ya shilingi za Tanzania milioni 257.
Awali Bebe Cool alifungua mashitaka akidai zaidi ya milioni 533 za Tanzania, kufuatia kujeruhiwa sehemu ya mguu wake.
Bebe Cool alidai kiasi hicho cha pesa kama fidia ya kipato
alichopoteza katika kipindi cha miezi 9 hadi 12 wakati akiuguza majeraha
ya risasi.
Msanii huyo aliiambia mahakama kuu ya Uganda kuwa alikuwa amepata
dili ya kufanya matangazo na MTN na Century Bottling Co Ltd, makampuni
ambayo yangemlipa kiasi kikubwa cha pesa. Na kuongeza kuwa alikuwa
katika maandalizi ya kurekodi nyimbo 16 kwa ajili ya album yake ambayo
ingemuingizia mkwanja mrefu.
Hata hivyo, Bebe Cool alishindwa kuwasilisha vielelezo mahakamani
kuonesha hasara hiyo, hivyo mahakama ikaamua alipwe milioni 257 badala
ya milioni 533 alizodai.
Bebe Cool alipigwa risasi January 29 mwaka 2010 na polisi
anayejulikana kwa jina la Anthony Achikan muda mfupi baada ya kupiga
show kwenye jukwaa moja na R.Kelly jijini Kampala.
Bebe Cool na kundi lake walikuwa barabarani na magari yao mida ya saa
tisa usiku wakielekea Nakumatt, ambapo walikutana na polisi
aliyewasimamisha.
Yalitokea majibishano ya muda mrefu kati ya Polisi huyo na Bebe Cool,
ndipo polisi huyo alifyatua risasi zilizomjeruhi mwimbaji huyo.
Polisi huyo alikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya usalama ambapo alifunguliwa mashitaka kwa kufanya jaribio la kuua.
Polisi huyo alikutwa na hatia na hadi sasa anaendelea kutumikia kifungo cha miaka 9 jela.
No comments:
Post a Comment