01 December 2013

MSAFARA WA MWENYEKITI UVCCM WAWEKEWA MAGOGO


Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) taifa, Sadifa Juma Khamis (MB) Polisi mkoani Pwani inachunguza kundi la watu linalodaiwa kuweka magogo barabarani kuzuia msafara wa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) taifa, Sadifa Juma Khamis (MB) katika eneo la Tondoroni, wilayani Kisarawe, mkoani humo. 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema atazungumzia suala hilo baada ya  kupata  taarifa kamili. 
Kwa mujibu  wa watu walioshuhudia tukio hilo, kundi hilo liliweka magogo hayo jana usiku katika barabara ya kati ya eneo la Mpuyani katika njia panda ya barabara iendayo vijijini kuingia barabara kuu ya Morogoro. 
Mashuhuda wa tukio hilo walisema katika nyakati tofauti kundi hilo lilianza kuzuia msafara huo kwa kutaka kushinikiza dai la mgogoro wa mipaka kati ya eneo la Jeshi la Wananchi wa Ulinzi Tanzania (JWTZ) na makazi ya watu katika eneo la Tondoroni, wilayani humo. 
Watu hao ambao idadi yao haikuweza kufahamika walidaiwa kutishia kuchoma moto magari ya msafara huo wa mwenyekiti wakati alipotaka kushuka na kuzungumza nao na kuamua kujisalimisha kwa kuingia ndani ya gari  na kurudi Kisarawe. 
Mwenyekiti  huyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Tanzania Visiwani mapema akiwahutubia  wananchi wa Kisarawe aliwataka kudumisha amani kwa  kukiweka Chama Cha Mapinduzi madarakani. “Amani ikivurugika hakuna atakayekuwa salama, hata askari  nao  hawatokuwa salama”. 
Akiongea na viongozi wa CCM na UVCCM  katika jengo la ofisi za CCM wilaya, aliwataka wanachama hao kuvunja makundi ya kampeni kwa kuwa hayana tija kwa sasa, isipokuwa wakati wa kampeni za uchaguzi. 
Alisema kuwa Muungano wa Tanzania ni muhimu hivyo changamoto zilizomo ndani yake zitafutiwe muafaka kwa njia ya amani. 
Alisema kuna  baadhi ya watu wakorofi ambao wanadai muungano uvunjwe hasa kutoka Pemba wakidai kuwa kisiwa hicho ni chao wakati  visiwa hivyo vya Pemba na Zanzibar havina wenyewe na watu walioko huko wametokana  na  biashara ya utumwa na wengi wao walitoka upande wa Tanzania Bara wa makabila mbalimbali. 
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo alimsimika mwandishi wa siku nyingi, Abubakar Mlawa kuwa kamanda wa UVCCM wilayani humo na wengine 15  wakiwamo madiwani  kuwa makamanda wa UVCCM wa kata zao.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname