Mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari (CHADEMA), amesema Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya chama hicho, Bw. Godbless Lema yupo katika hatari ya kubambikiwa kesi.
Alisema ipo mipango inayosukwa ili kumhusisha Bw. Lema na milipuko ya mabomu katika mikutano ya chama hicho, eneo la Soweto na ule wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, mkoani humo.
Bw. Nassari aliyasema hayo bungeni Mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na kuongeza kuwa ni wajibu wa Serikali kusimamia haki badala ya kuwabambikia kesi wanasiasa kwa lengo la kudhoofisha vyama vya upinzani.
Alisema kwa mara kadhaa, amewahi kutembelea magereza na kujionea vijana wengi wakiwa ndani bila hatia na kutolea mfano wa kijana ambaye alikamatwa na kuwekwa mahabusu akihusishwa na ulipuaji wa bomu Soweto na Olasiti.
"Huyu kijana yupo tayari kutoa ushahidi...alikamatwa Arusha na kupelekwa Mwanza, baadaye alihamishiwa mkoani Shinyanga ambako aliminywa sehemu zake za siri na kuvunjwa mguu ili amtaje Lema kuwa alihusika na matukio hayo," alisema.
Bw. Nassari alimtaka Bw. Pinda kutoa ufafanuzi juu ya Serikali kuwabambikizia watu kesi ili kuvidhoofisha vyama vya upinzani badala ya kusimamia upatikanaji wa haki kwa raia wake.
Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema si nia ya Serikali kutaka kuwabambikizia watu kesi ambapo mambo yaliyotokea Soweto na Olasiti si madogo na yeye hana taarifa za suala hilo.
Alisema Serikali inaendelea na uchunguzi ili kuwabaini watu waliohusika na milipuko hiyo na
kama kuna Mbunge anayejua kila kitu ni vyema akatoa taarifa hizo ili ziweze kupelekwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
"Kwa kweli siwezi kujibu swali hilo...Mheshimiwa Nassari anajua kila kitu na mimi sina taarifa lakini si nia ya Serikali kuwabambikizia watu kesi ni vyema uandike maelezo yako kwa maandishi ili niwape wahusika ambao ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi wachunguze," alisema.
Kwa upande wake, Bw. Lema alisema amekuwa na wasiwasi juu ya suala hilo kwani yeye hausiki na jambo hilo na mhusika yupo ambaye alilazimishwa ili amtaje yeye.
No comments:
Post a Comment