BEKI wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani ‘Vidic’, ameibua maswali
mengi kwa mashabiki wa Simba na Yanga baada ya kuvua jezi yake namba
tano na kuwatupia mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi ambao nao
waliichanachana na kugawana vipande.
Lakini kabla ya kutupa jezi hiyo, aliwaonyeshea
ishara ya pesa kwa kuchezesha mikono yake ndipo utata ulipozidi. Yondani
aliibua maswali hayo ni baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa
mchezo huo, Ramadhani Ibada ‘Kibo’, kutokana na kumwonyesha kadi ya
njano kwa mara ya pili.
Alipokuwa anatoka nje, ndipo Yondani alipofanya
tukio hilo kwa kuwarushia mashabiki wa Simba jezi ya Yanga. Mashabiki
wale waliichukua na baada ya muda mchache, waliichanachana vipande
vidogo.
Mmoja wa mashabiki wa Simba, Hassan Timbwa,
alisema: “Hakuna jinsi, ilikuwa lazima tuichane kwa sababu kwetu hakuna
mvaaji, sisi Simba rangi zetu ni nyekundu na nyeupe, si nyingine.”
Yondani hakuwa wazi kufunguka juu ya mkasa huo na
kuondoka kimya kimya. Katika mechi hiyo ya Nani Mtani Jembe, Simba
ilishinda mabao 3-1.
No comments:
Post a Comment