Siku chache tu zilizopita tulihoji mpango wa Bunge kuwapeleka
wabunge nje ya nchi mara kwa mara kufanya kile kinachoitwa ziara za
kikazi na mafunzo. Tulisema ziara hizo hazina tija kwa taifa, isipokuwa
ni mkakati uliosukwa na Bunge kwa lengo la kuwanufaisha wabunge kifedha.
Tulihoji sababu za kufuja fedha za umma kuwapeleka wanasiasa katika
ziara hizo zenye gharama kubwa badala ya kupeleka wataalamu wetu walio
katika sekta muhimu zinazotoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa
nchi yetu.
Pamoja na kusisitiza kwamba ziara hizo zinazoitwa
za kikazi na mafunzo zimekuwa zikitumia mabilioni ya fedha za
walipakodi, tulihoji sababu za Kamati hizo kushindwa kufanya majumuisho
au kuonyesha jinsi gani wabunge wake na wananchi kwa jumla
walivyonufaika au watakavyonufaika na ziara hizo.
Tulisema Kamati hizo zilikuwa zikishindana kuona
ipi inafanya ziara nyingi zaidi kuliko nyingine au ipi inayowapeleka
wajumbe wake katika nchi zenye ‘neema’ zaidi kuliko nyingine. Bila
kumung’unya maneno, tulisema ziara hizo ni za kitalii na matanuzi zaidi
kuliko kitu kingine, kwa maana ya kutoleta tija kwa Bunge wala taifa.
Tulionyesha jinsi wajumbe wa Kamati nane za Bunge
walivyokuwa katika ziara mbalimbali ughaibuni kwa wakati mmoja.
Kichekesho cha karne ni pale tulipoambiwa kwamba Kamati ya Hesabu za
Serikali za Mitaa ilikuwa katika ziara ya Uingereza na Ireland eti
kujifunza masuala ya serikali za mitaa. Tuliuliza ni jinsi gani
mazingira ya Uingereza na Ireland yanafanana na ya Tanzania na kuhoji
kwa nini ziara hizo zisingefanyika katika nchi za Afrika zenye mazingira
yanayofanana na ya Tanzania? Wakati huo Kamati nyingine nyingi zilikuwa
nje ya nchi katika ziara kama hizo. Ndiyo maana tulisema siyo lazima
kuwa na shahada ya chuo kikuu kuweza kugundua kwamba ziara hizo
zinazoitwa za mafunzo na kikazi ni za ujanja ujanja na ubadhirifu wa
kupindukia.
Tumesema yote hayo kutokana na kashfa iliyolikumba
Bunge juzi kwa taarifa kwamba wabunge wengi wamekuwa wakichukua posho
za ziara hizo lakini wanakwepa kwenda, huku wakiweka fedha hizo
mifukoni. Huu ni wizi wa mchana kweupe na ni kosa la jinai, wala siyo
suala la kisiasa kama ambavyo wabunge wengi walivyotaka lionekane
walipokuwa wakilijadili bungeni juzi. Kashfa hiyo inawahusu wabunge
karibu wote na hii pia inahusu ziara zao mikoani, ambapo wengi
wanachukua posho bila kufanya ziara hizo.
Tunatarajia kwamba kashfa hii kubwa haitazimwa
hata kama Spika mwenyewe na uongozi wote wa Bunge utakuwa unahusika.
Tunamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), apanue
wigo kwa kukagua hesabu za Bunge na taasisi zinazosimamiwa na Kamati
mbalimbali za Bunge ili kuona kama fedha zilizotolewa kwa wabunge
kufanya ziara mbalimbali zilitumika kwa kazi hiyo.
Bunge hili la 10 limepoteza mwelekeo kwa wabunge
kujawa na tamaa za kujirundikia mali na kutaka utajiri wa haraka. Sasa
tunashuhudia wabunge wakidai na kupewa rushwa na mashirika
wanayoyasimamia, huku safari na ziara zao nyingi zikigharamiwa na
mashirika hayo. Uovu huo umewapofusha macho na kujaza kutu ndani ya
dhamira zao. Ndiyo maana hatuoni mabadiliko ya kweli katika hulka, kauli
na matendo yao. Badala yake tunashuhudia utapeli uliokithiri.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment