Cape Town. Baraza la
Jiji la Cape Town, limeidhinisha matumizi ya Rand72 milioni (Sh12.2
bilioni) kwa ajili ya mazishi ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson
Mandela.
Taarifa ya baraza hilo iliyotolewa jana ilisema bajeti hiyo ilipitishwa
katika kikao cha dharura na kwamba itasaidia kufanikisha shughuli zote
za maandalizi ya kumuaga Mandela katika mji huo.
Mbali na kupitisha bajeti hiyo, pia liliamua kuweka usafiri wa bure kwa
kutumia treni za mji huo – MyCiTi na mabasi marefu ya Golden Arrow
kuwafikisha watu katika maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya
kuonyeshwa shughuli za kuaga mwili.
Meya wa mji huo, Patricia de Lille alisema wameandaa pia mkakati maalumu
kwa watu watakaokuwa wanatembea kwa miguu ili kushiriki katika tukio
hilo muhimu na la kihistoria nchini humo.
Alisema taratibu za kuaga zitafanyika kesho na kwamba zitaendeshwa kwa
utaratibu maalumu na wa kipekee kwa sababu mji huo una historia ya
kipekee kwa kiongozi huyo aliyejitoa kudai uhuru.
“Kwa aibu yetu, mji huu ndimo lilimo gereza ambalo alitumikia kifungo cha miaka karibu yote 27,” alisema Lille na kuongeza:
“Lakini pia hapa ndipo alipotolea hutuba yake ya kwanza mara baada ya kuachiwa na kutaka iandikwe katiba mpya.”
“Kwa zawadi hii, tumemfanya Madiba kama sehemu inayoishi milele katika
Serikali na jiji hili. Madiba amechangia mengi ambayo hapa tunajivunia
leo hii.”
No comments:
Post a Comment