13 November 2013

UNAWEZA KUWA ULIMTENDEA MTU UBAYA MIAKA YA NYUMA NA UMESAHAU LAKINI YEYE HAJASAHAU NA ANAKUWINDA KULIPIZA KISASI!!

Kawaida yetu sisi kwenye leo tena tukimaliza tu kipindi ni lazima tukute wageni kibao waliokuja kutusalimia,kutuletea zawadi,kutueleza matatizo yao wengine wakiwa na dukuduku wanalotaka kutoa mioyoni mwao n.k
Leo mchana nimemaliza kipindi nikashuka chini lakini Gea akiwa amenitangulia kushuka.Kawaida tunaeneo huwa tunaweka viti tunapaita kijiweni hapo ndio tunakaaga na wageni wetu.
Nikamkuta Gea anaongea na mama aliyekuwa akilia kwa uchungu kilio kile cha kwikwi Gea akaniambia Dina msikilize huyu mama ana machungu yake tuone tutamsaidiaje kwenye kipindi
Mama akaanza kunisimulia kisa chake kilichonifanya nihisi naangalia movie.
(picha sio ya muhusika) Anasema miaka 12 iliyopita aliletwa Dar es salaam akitokea kijijini kwao kuja kufanya kazi za ndani.Alifika kwenye familia ya mama na baba waliojaaliwa kupata watoto wawili mdogo kabisa akiwa na mwezi mmoja.Anasema aliishi kwa furaha akafanya kazi zake na kulea watoto huku kukiwa hakuna tatizo kati yake na mama au baba mwenye nyumba.
Baada ya mwaka na miezi kadhaa kupita mtoto mdogo alishaanza kutembea na alikuwa akimpenda mno.Yeye amejaaliwa nywele nzuri tu za asili sasa kuna kipindi ilikuwa sikukuu mama akamwambia azitie dawa zitapendeza zaidi kweli akaweka dawa na nyweli zikawa nzuri tena ndefu zaidi.
Siku zikazidi kusogea mama akaanza kumbadilikia akawa mkali anamtreat vibaya kama vile kuna kitu ambacho yeye hakijui.Kila siku mama akawa ana kisirani nae mpaka akafika mahali akamfukuza nyumbani bila sababu yoyote.
Alimfukuza akijua hajui chochote hapa Dar es salaam wala namna ya kurudi kijijini kwao na wakati anafukuzwa baba mwenye nyumba hakuwepo.
Basi akatoka hapo nyumbani akaulizia stesheni ya treni ilipo maana anakumbuka alikuja kwa treni.Kufika stesheni hakuna treni siku hiyo akabaki anashangaa shangaa hapo na kilio juu hajui pa kuelekea wakati huo ni jioni wakatokea vijana wakajifanya wanataka kumsaidia wakamchukua kumbe walikuwa wahuni wakaishia kwenda kumbaka.
Baada ya kubakwa wakamtelekeza akiwa hajiwezi ndio kuna mama akamkuta katika hali mbaya akamchukua na kumsaidia.Akakaa kwa huyo mama akatibiwa majeraha akapona lakini ikabidi apime kama ameambukizwa magonjwa na mimba pia kama amepata.
Dada wa watu akapimwa akakuta ameambukizwa H.I.V  na mimba juu.
Anasema alilia sana na yule mama kumtia moyo kuwa ndio dunia.Baada ya kukaa pale mimba ikakua akaona bora arudi tu kijijini kwao basi akarudi kijijini akakakaa huko mpaka alipojifungua.Alijifungua salama mtoto wa kike na uzuri mtoto hakuambukizwa yupo salama mpaka leo amekuwa na anasoma shule yupo darasa la tano.
Dada anasema japo anaendelea na maisha yake na kujishughulisha na shughuli za upishi amekuwa na roho mchafu wa kulipa kisasi anamsumbua.Amekuwa akiishi na mawazo mabaya ya kuua kwa miaka mingi.Tukio alilofanyiwa linamtesa sana anasema kuna wakati anasahau kama ameathirika lakini ile hali ikimjia ya kumkumbusha kuwa anaishi na virusi vya ukimwi humfanya hapo hapo aanze kwenda hedhi.
Ni mara kadhaa ameshapanga mauaji ya huyo mama na watoto wake.Yeye anaishi mkoani alishakuja Dar es salaam mara mbili na kufika mpaka kwenye hiyo nyumba.
Kuna siku alishakuja akaingia mpaka ndani watoto walikuwa wenyewe akawatazama akawasalimia kutoka atokako alikuwa amepanga kuua lakini alipowaona wale watoto na akakumbuka aliwalea roho ya imani ikamuingia akaondoka.
Siku nyingine alishapanga kuchoma hiyo nyumba moto lakini akawaza je wakifa wasio walengwa je?Kumbuka anatoka mkoani kwa lengo hilo moja kulipa kisasi.
Anasema anataka huyo mama apate pigo na yeye asikie uchungu kuvurugiwa maisha yake.Wakati mwingine anawaza ajichome sindano atoe damu yake akimuona huyo mama amchome na kumuwekea hiyo damu na yeye apate H.I.V ana mawazo mengi mabaya kiukweli.
Akisimulia hayo yote analia kwa uchungu kwa nini alimtenda vile,kwa nini alimfukuza?alimkosea nini?kwa nini asingempandisha basi akarudi kwao.Ndio sasa anamtoto lakini mtoto ipo siku atamuuliza baba yupo wapi?yeye mwenyewe japo ana afya yake haumwi ipo siku atakufa mwanae atabaki na nani?
Anasema baada ya kuteseka na hicho kitu ndio akafunga safari kuja kukiongea ili asaidiwe kimawazo au vyovyote maana amekuwa akisikiliza leo tena watu wengi wanaongea yanayowasibu.
Nikamuuliza iwapo tukimtafuta huyo mama na familia yake yupo tayari kuwaona ana kwa ana na kumueleza matokea ya tendo alilowahi kumfanyia miaka 11 iliyopita?akasema hajui.
Mimi kwa kumsikiliza nimeona huyu mama anahitaji kusamehe ili aishi kwa amani.Pia akutane ana kwa ana na huyo mama amwambie kidonda alichosababisha kwenye maisha yake.Mama akubali makosa na amuombe msamaha kwa dhati.Pia asaidiwe uponyaji wa kiroho ili aweze kusamehe na kukubali yaliyotokea kwenye maisha yake na afungue ukurasa mpya.Na ikiwezekana apewe msaada wa kisaikolojia ili akili ikae sawa.
Kesho utamsikia katika leo tena ya clouds fm kuanzia saa nne asubuhi na utatupa mawazo yako ili kumsaidia.
Sijaweka jina,mkoa anaoishi,nyumba aliyoifanyia kazi hapa Dar kwa sababu maalum.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname