11 November 2013

MAMA MZAZI WA ZITTO KABWE AELEZEA JINSI ANAVYOKOSA RAHA NA MAISHA YA MWANAE


Kabwe Zitto akiwa na mama yake mzazi, Shida Salum.

Changamoto za hatari zilizomo katika mazingira ya safari ya kisiasa anamopitia Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe zinamtisha mama yake mzazi.
Mama wa Mbunge huyo kijana, Shida Salum, ameibuka na kusema alihangaika sana wakati wa malezi ya mwanawe huyo utotoni hata kuhatarisha maisha yake, wakati mtoto wake huyo alipoibwa siku moja na watu wenye silaha muda mfupi baada ya kumzaa Desemba 23, 1976.
“Sipendezwi kabisa na maisha kama mama wa mwanasiasa kutokana na changamoto nyingi ninazopata…maisha anayoishi Zitto yananipa uchungu wakati mwingine naweza kuacha kazi hapa nikarudi nyumbani kwa majonzi," anasema mama huyo. 
Akifafanua kuhusu mapambano yake na wezi, anasema alikatwa vidole kwa kisu wakati akinyang’anyana nao nguo alizomfunika mtoto huyo ambaye ni kati ya 10 aliojaliwa na Mungu.
Mama Zitto alisema hayo hivi karibuni Dar es Salaam katika mazungumzo mahsusi na mwandishi wa habari hizi.
Alisema anamshukuru Mungu kwa kumpa watoto, lakini kamwe hafurahii kuwa mama wa mwanasiasa kama Zitto.
Hata hivyo mbali na ulemavu wa vidole, mama huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata), alipata pia ulemavu wa mguu na mgongo akiwa kidato cha kwanza katika sekondari Kilakala, Morogoro.
Akisimulia changamoto anazopata kama mama wa mwanasiasa, anasema haikuwa rahisi katika malezi ya Zitto kutokana na kuonesha ushupavu na ujasiri tangu akiwa mdogo, hata hivyo anakiri kuwa kwa kiwango fulani, alichangia kumjengea ujasiri alionao sasa.
Na ili kukabiliana na changamoto alizonazo kisiasa, anasema kila anapopata fursa ya kusafiri ndani na nje ya nchi, humnunulia kijana wake vitabu vya masuala ya uongozi akiamini vitamjenga katika siasa na pia kuwa kiongozi mzuri kwa wananchi wanaomtegemea.
"Namnunulia vitabu hivyo, ili kumjenga kisiasa ili asione upinzani ni kupinga kila kitu, ajue kama kiongozi mbali na siasa ni nini wajibu wake kwa wapiga kura na pia kumjengea ujasiri ambao hata mimi unaanza kuniogofya sasa, maana amekuwa jasiri kupita kiasi," anasema Shida ambaye pia kitaaluma ni mwanahabari.
Shida alisomea fani hiyo kwa ngazi ya Stashahada katika kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ), ambacho kwa sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 
"Nilipata ulemavu wa vidole nikiwa mtu mzima, vilikatwa na wezi walionivamia nyumbani siku moja (Desemba 24) baada ya kumzaa Zitto. 
Wakati wakiiba nguo zilizokuwa kitandani bila kujua walibeba na mtoto wangu akiwa mchanga, nilijaribu kupambana nao wakanikata vidole kwa kisu," alisimulia mama huyo.  
Alisema: “Wezi hao walibeba nguo pamoja na mtoto ambaye ni Zitto…nililia sana nikiwasihi wamwache mtoto wangu, lakini walitoa kisu na kunikata vidole vya mkono wa kulia na kukimbia naye.”
Aliongeza kuwa, baada ya watu kusikia mayowe walifika kujua kilichotokea na alipowaeleza kuwa mtoto wake mchanga ameibwa, walizunguka kutafuta wezi hao  wakamkuta mtoto ametupwa chini ya mti pamoja na nguo.
"Mtoto walimkuta amewekwa chini pembeni ya mti wa msufi kwenye nguo na wezi wakiwa wamekimbia," alisema.
Kati ya watoto hao 10, mbali na Zitto mwingine wa kike, Ndabita Salum (22) kwa sasa yuko India akisomea Uhasibu, naye anapenda siasa akiwa ni mwanachama wa  CCM huku Zitto akiwa ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
"Sipendi siasa kwa sababu ina mambo mengi pamoja na kupoteza uhuru wa mtu, leo hii mtoto wangu yeyote kama ananiomba ushauri, siwezi kumshauri ajihusishe na siasa, ni hatari," anasema na kuongeza kuwa, siku zote amekuwa akiishi kwa hofu juu ya maisha ya mwanawe akiamini kuna wanaompenda na wasiopendezwa na ujasiri wake.
Shida ni mtoto wa pekee katika familia ya Salum Mohammed na Rukia Karavina wenyeji wa Mwanga, Kigoma Mjini alikozaliwa Julai 7, 1954 bila kuwa na ulemavu wowote.
Alisoma katika shule ya msingi Kigoma hadi darasa la nne na kwenda shule ya kati ya wasichana ya Urambo alikohitimu darasa la nane ambako alijiunga na kidato cha kwanza sekondari ya wasichana ya Kilakala.
"Nikiwa kidato cha kwanza niliugua homa kali nikarudishwa nyumbani, kumbe nilipooza, homa ile niliugua kwa miezi karibu mitatu na nilipopona nilikuwa nimepata ulemavu wa mgongo na mguu kidogo," alisema na kuongeza kuwa ilibidi kukubaliana na hali hiyo akarudi shuleni kuendelea na masomo hatimaye alihitimu kidato cha nne mwaka 1971.
Baada ya hapo alisema hakufanikiwa kuendelea na masomo ya juu badala yake alikwenda Chuo cha Serikali za Mitaa (sasa Mzumbe) na kupata Cheti cha Usimamizi wa Kodi za Serikali za Mitaa.
Alianzia kazi Kigoma akiwa mkusanya kodi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, aliolewa na kupata watoto hao 10.
Mwaka 1980 alipata kazi Wizara ya Fedha ya kukusanya mapato baada ya kupata Stashahada katika taaluma hiyo na amefanya kazi Kigoma, Mara, Kagera na Dar es Saalam ambako mwaka 1982 alijiunga Chawata.
Mwaka 1985 kupitia chama hicho alipata ufadhili na kusomea uandishi wa habari TSJ, lengo likiwa ni kusaidia kuandika habari za walemavu na changamoto zao, hata hivyo kazi hiyo hakuifanya hata mara moja.
"Mwaka 1996 niliomba kustaafu nikiwa Dar es Salaam, kwa sababu sheria ilikuwa hairuhusu walemavu kustaafishwa, nilirudi Kigoma na tulianzisha Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Serikali wilaya za Kigoma na Kasulu," alisema.
Ilipofika mwaka 2008 alirudi Dar es Salaam baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Walemavu nafasi ambayo anaishikilia mpaka sasa.
Akielezea changamoto za walemavu anasema anajitahidi kutetea mambo mbalimbali yanayokabili walemavu, ikiwa ni pamoja na watoto walemavu kupelekwa shule pamoja na watoto wasio walemavu.
"Mimi kama mjumbe wa Baraza la Katiba nashukuru karibu maoni mengi tuliyowasilisha yanayohusu walemavu yalipokewa na Tume na kuingizwa katika Rasimu, mambo ya elimu ya walemavu ni changamoto kubwa, kuna chuo kimoja tu cha walimu wa walemavu inabidi viongezwe kukidhi haja," alishauri.
Alitaja changamoto nyingine kwa walemavu kuwa ni kupata lugha ya alama kwa  wasioona na kusikia na pia kuondolewa kodi kwa vifaa vya walemavu vinavyoingizwa nchini, pamoja na miundombinu katika maeneo mbalimbali.
Source na zero blogspot

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname