*Dk. Bana: Tulitarajia kusikia busara, si kuzungumzia mtu
*Seif Khatib: Sitaki kuingizwa kwenye mbio za urais
KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, amemtaka Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, kujitambua na kufanya mambo yanayolingana na hadhi yake.
Pia amemtaka atumie muda wake kuwaeleza Watanzania sifa na uwezo wake, badala ya kupoteza muda kuzungumza na vyombo vya habari masuala yenye kumdhalilisha. Akizungumza na Rai jana Makamba alisema; “Nimesoma kwenye magazeti leo na kuona Sumaye akimsema mwenzake (Lowassa), binafsi sikupenda kabisa.
“Wale wanaosoma Biblia katika kitabu cha kwanza cha Timotheo, sura ya 3:1 imeandikwa: Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya Askofu, atamani kazi njema.
“Sasa na mimi nasema mtu akitaka kazi ya urais, basi atamani kazi njema. Hivyo wote wale wanaotamani urais wanatamani kazi njema. Sasa kuna sababu gani ya kusemana mbele ya vyombo vya habari?
“Watanzania wanataka uwaeleza sifa ulizonazo, lakini sidhani kama wanapenda au wanafurahia kuwaona viongozi wakubwa wakianza utamaduni wa kusemana kupitia vyombo vya habari.
“Pia mtu anayepaswa kujisifu ni yule anayetoka vitani, si yule anayekwenda, sasa Sumaye na Lowassa wameshakwenda vitani, kwa hiyo tunazijua kazi zao, uwezo na uhodari wao.
“Hawana sababu yoyote ile ya kulumbana, wasubiri muda ukifika wakachukue fomu, halafu sisi ndio tutaamua kutokana na tunavyowafahamu.
“Sumaye hana sifa ya kuzungumzia rushwa, tunakumbuka alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10, na katika kipindi cha uongozi wake rushwa ilikuwapo, labda atuambie alifanya nini kukabiliana nayo?
No comments:
Post a Comment