TAMKO LANGU KWA UMMA JUU YA UZUSHI UNAOENEZWA DHIDI YANGU.
Ndugu wanahabari,
Baada ya kumshukuru na
kumtukuza mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Natanguliza salamu zangu za
pole kwa familia ya marehemu mwanazuoni na mwanaharakati mwenzangu Dkt
Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya Haki siku chache zilizopita huko
Afrika ya kusini.
Ndugu zangu wanahabari,
Wengi mnanifahamu na
kuifahamu vema historia yangu katika utendaji kazi na utumishi wa umma
wa Watanzania. Nimekuwa nikiitumikia nchi yangu kwa kipindi kirefu
katika Nyanja na sekta mbali mbali kuanzia Darasani mpaka kwenye siasa.
Kwa msingi huo, mimi
Profesa Juma Kapuya, siku zote ninajikuta mwenye wajibu endelevu wa
kuendelea kulitumikia Taifa langu kila siku mpaka kufikia mwisho wa
Nguvu zangu.
Ndugu wanahabari,
Hivi karibuni nikiwa
huku jimboni kuendelea na shuhuli za utekelezaji wa ilani ya chama cha
mapinduzi kumezuka Tuhuma kadhaa zilizoelekezwa dhidi yamgu zikiasisiwa
na wanasiasa wenzangu wa ndani na nje ya chama changu ili kudhoofisha
juhudi na utendaji wangu wa kila siku.
Tuhuma hizo zisizokuwa
na kichwa wala miguu na pia kutokuwa na ukweli wowote, wamekuwa
wakizitoa kwa kumtumia msichana anayedai amefanyiwa vitendo visivyofaa
na mimi. Mimi simfahamu na sijui hizi shutuma zinatokea wapi.
Ndugu wanahabari,
Kwa tamko hili
ninapenda kuwaambia kuwa nimefedheheshwa sana na uwezo mdogo wa kisiasa
unaofanywa na hawa watu kwa kuwa dhamira yao haitatimia. Napenda
niwakumbushe ndugu zangu kwamba tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka
2015 na wapinzani wangu wameanza kunichafua ili nionekane sifai.
Ninapenda kuwaambia
watanzania na wananchi wa jimbo langu kuwa wanatakiwa wazipuuze taarifa
hizi kwa kuwa hazina ukweli wowote na kwamba ni za kutungwa zenye lengo
la kunidharirisha na kuniondolea heshima yangu niliyojijengea kwenye
jamii kwa kipindi kirefu sasa. Waswahili wanasema dawa ya mjinga ni
kumpuuza
Na hili
linajidhihirisha zaidi kwa habari hii kuandikwa na chombo kimoja tu cha
habari kinachotumiwa na chama kimoja cha siasa na baadhi ya wanasiasa wa
chama changu wasiokitakia heri chama chetu, naomba kuwashukuru na
kuwapongeza vyombo vingine vya habari kwa umakini wenu wa kuwa na
nauelewa wa kutoandika kitu bila kukifanyia uchunguzi na kubaini ukweli
ulivyo.
Chombo
hiki cha habari kiliwahi kuripoti mwaka jana kuwa kuna mitambo
imeingizwa nchini inayoweza kuandika ujumbe na kisha kuufanya uonekane
umetoka kwenye namba Fulani, kwa kipindi kile sikuwaelewa, lakini sasa
ninawaelewa na nimewaona kuwa wako sahihi na wao ndio waliouingiza
mtambo huu na sasa wameamua kuutumia dhidi yangu kwa kutengeneza meseji
na kuzihusianisha na mimi. Ninaamini ukweli utawaumbua muda si mrefu.
Ndugu wanahabari,
Nimeijenga heshima
yangu na familia yangu kwa jamii yangu kwa kipindi kirefu mno, kwa hivyo
siwezi kuruhusu heshima niliyoijenga kwa miongo kadhaa karibiwa na
kupotezwa na watu wachache tena kwa muda mfupi namna hii.
Hivyop basi nimechukua hatua za kisheria kuhakikisha heshima yangu inaendelea kulindwa na utu wangu unaheshimiwa.
Nimemwagiza
mwanasheria wangu afungue kesi na tayari amewashitaki watu wote
wanaohusika kwenye mpango huu na tayari wameshapokea taarifa ya kuitwa
mahakamani.
Nitaendelea
kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaoendelea kutaka
kujipatia umaarufu ama wa kisiasa au wowote ule kwa kutumia jina langu.
Hayo yote ni kwa
kuzingatia ukweli kwamba nchi yetu inaendeshwa kwa misingi ya kisheria
na kufuata na kuheshimu haki na wajibu wakila mmoja wetu.
Kwenye hilo ninawaambia ‘’janja yao nimeigundua, na hawatafanikiwa’’
Ninatoa Rai kwa yeyote
mwenye kuona hilo jambo lina ukweli alipeleke kwenye vyombo husika ili
lishuhulikiwe kwa mujibu wa sheria na sio kutumia vyombo vya habari
kuchafuana.
Mwisho ninasisitiza
kuwa nitaendelea kuilinda na kuitetea heshima yangu niliyojijengea kwa
jamii kwa muda mrefu sasa na sitaruhusukuiona ikiharibiwa na wajanja
wachache kwa maslahi yao binafsi.
Tuendelee kuijenga nchi yetu,
Mungu Ibariki Tanzania
Imetolewa leo tarehe 15.11.2013 nami
Prof. Juma A.Kapuya
Mbunge – urambo magharibi
S.L.P 45 Kaliua Tabora
Simu 0784993930
No comments:
Post a Comment