29 October 2013

UTAJIRI WA MAASKOFU: GWAJIMA TAJIRI NO.1....AWANUNULIA WACHUNGAJI WAKE 30 KILA MMOJA GARI,MABASI 20 KWA AJILI YA WAUMINI,ANAINGIIZA MILIONI 3 KWA SIKU..




UCHUNGUZI  wa kina uliofanywa na Gazeti la Uwazi kwa muda wa siku 30 umebaini kuwa Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar, Josephat Gwajima ndiye anayeongoza kwa utajiri wa viongozi wa imani ya Kikristo, hususan wa njia ya kilokole.
Gari la kifahari aina ya Hummer 2 analomiliki Mchungaji Gwajima.
Utafiti huo umefanywa kwa kutembelea makanisa makubwa ya kiroho ya jijini Dar es Salaam na kuomba kuzungumza na viongozi wake ambapo Gwajima alitoa ushirikiano kwa asilimia mia moja kuliko wengine.
MAKANISA YALIYOTEMBELEWA
Makanisa yaliyotembelewa na majina ya viongozi wake kwenye mabano ni pamoja na Full Gospel Bible Fellowship (Askofu Zachary Kakobe), Living Water Center ‘Makuti Kawe’ (Mtume Onesmo Ndegi), Kanisa la Maombezi ‘GRC’ (Lusekelo Anthony ‘Mzee wa Upako’), Mikocheni B Assemblies of God (Mama Rwakatare) na Kanisa la Efatha (Nabii na Mtume Josephat Mwingira).

Mabasi aliyonunua Gwajima kwa ajili ya waumini wake.
KWA NINI GWAJIMA NI NAMBA MOJA?
Anakuwa namba moja kwa sababu alianika mali zake na kipato chake kingine bila kushikwa na kigugumizi. Gwajima alisema anamiliki gari la kifahari aina ya Hummer 2 ambalo gharama ya manunuzi mpaka kufika Tanzania ni wastani wa shilingi milioni 250.

AWANUNULIA WACHUNGAJI MAGARI
Akizungumza na Uwazi hivi karibuni kwenye ofisi za kanisa lake, Kawe, Dar, Mchungaji Gwajima alisema hivi karibuni aliwanunulia wachungaji wake 30 magari ya kutembelea. Alisema fedha hizo alizitoa mfukoni mwake.





Baadhi ya magari aliyonunua Mchungaji Gwajima kwa ajili ya wachungaji wake.
Baadhi ya magari aliyoyakumbuka ni Subaru Forester (sokoni linauzwa shilingi milioni 17), Mitsubishi Pajero (shilingi milioni 16), Toyota Spacio new model (milioni 20) na Toyota Harrier Lexus (milioni 35).

ANAMILIKI JUMBA LA GHOROFA NNE
Mchungaji huyo alikwenda mbele zaidi kwa kuanika maisha yake ambapo alisema awali alikuwa akiishi kwenye  nyumba ya kupanga iliyopo Mbezi Beach, Dar lakini kwa sasa amehamia katika nyumba yake mpya ya ghorofa nne, mbili zikiwa hazijakamilika. Nyumba hiyo ipo Mbezi Beach.


ANA MABASI 20 KWA AJILI YA KUSAFIRISHIA WAUMINI WAKE
Gwajima: “Pia nimeweza kwa neema ya Mungu kununua mabasi ishirini. Haya ni kwa ajili ya kusafirishia waumini wa kanisa langu wakati wa kuja kwenye ibada na kurudi makwao.”

Alisema mabasi hayo ambayo hakuyataja majina na wala yenyewe hayajaandikwa majina mbele akidai ni ‘oda’ maalum, kila moja alilinunua kwa shilingi milioni 120.

SAFARI YA ULAYA NA MAREKANI KILA MWAKA HUMWINGIZIA SHILINGI MILIONI 192
Akizungumzia kipato, Gwajima alisema mbali na sadaka ambazo huendeleza kanisa, yeye mwenyewe kila mwaka huwa na safari ya Marekani kwenda kufundisha Injili  kama mwalimu.

“Pia nimekuwa nikijipatia fedha kutokana na kazi ya ualimu ambapo kila mwaka mara moja huwa nakwenda nchi za Ulaya na Marekani kufundisha kwa siku 60. Katika siku hizo huwa nalipwa dola za Marekani 2,000 kwa siku,” (kama shilingi milioni 3.2).
Kwa hesabu hiyo, kwa siku sitini Mchungaji Gwajima hukamata shilingi milioni 192 na kurudi nazo Tanzania.


ATAMBA KUWA NA WAUMINI WENGI KULIKO WENZAKE
Gwajima alisema kwa sasa kanisa lake limepanuka ambapo alitamba kuwapa Neno waumini wapatao 70,000 kwa siku hivyo yu mbioni kuanzisha makanisa  mengine  mikoa yote ya Tanzania.

Kiongozi huyo alifafanua kuwa amefanikiwa kuwa na waumini wengi kuliko makanisa mengine kutokana na huduma nzuri anayotoa kwa waumini na jamii kwa jumla.
“Nimefanikiwa kuwa na waumini wengi kuliko wengine kwa sababu nahubiri Neno tu, sirushiani maneno na makanisa mengine.
“Sisi (yeye na wachungaji wake) hatuna utamaduni wa kuwashambulia wachungaji wenzetu. Wao hata wakitusema vipi, sisi tunakaa kimya kwani kujibishana kunaleta mgawanyiko,” alisema Gwajima.


MZEE WA UPAKO
Uwazi lilifika kwa Mzee wa Upako, Ubungo Kibangu, Dar lakini ilikuwa ngumu kumuona, wasaidizi wake wakisema ana huduma ya kiroho.

Hata hivyo, kwa kutumia kumbukumbu za nyuma ambapo mtumishi huyo wa Mungu aliwahi kuhubiria waumini wake (ikaandikwa kwenye Uwazi) akitaja utajiri alionao na mahubiri hayo kurushwa na Channel Ten, alisema:
“Mimi ndiye Mzee wa Upako, nikitoka nje nakuta magari yangu sita, nachagua leo niendeshe hili au lile. Najiambia hapana hili nililiendesha jana, nachukua lingine.”

ATAJA MAGARI ALIYONAYO
Katika mahubiri hayo, Mzee wa Upako aliyataja magari hayo kuwa ni Mercedes Benz, Land Rover Discovery, Range Rover Sport, BMW X5, Ford Escape na Range Rover Vogue.

Aidha, mtumishi huyo wa Mungu aliendelea kutamba kuwa nyumbani mwake kuna viyoyozi  (AC) na kubainisha kwamba huwa akitoka kwenye gari lenye kiyoyozi anaingia katika nyumba yenye kiyoyozi.
Kiongozi huyo ana kanisa kubwa la ghorofa Ubungo Kibangu na mabasi makubwa matano ambayo hutumika kuwasafirishia waumini wake kutoka Barabara ya Mandela hadi kanisani kwake.

KWA WACHUNGAJI WENGINE, UWAZI LAAMBULIA PATUPU
Kwa wachungaji wengine wa kiroho, mwandishi wetu alipigwa danadana za nenda rudi, nenda rudi lakini kwa muda wote huo hakuweza kuonana na viongozi wake ili na wao wafungukie utajiri wao licha ya kwamba baadhi yao unajulikana.

Uwazi lilipenda kusikia kutoka kwenye vinywa vyao na si kwa kuambiwa na watu wengine au kuhisi.
Kwa Askofu Kakobe, nako hali ilikuwa hivyohivyo ingawa siku za nyuma aliwahi kunukuliwa akisema kwamba yeye siyo tajiri.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname