17 October 2013

REFA ALIYEPIGWA NA YANGA MWAKA JANA KUCHEZESHA PAMBANO LA WATANI JUMAPILI TAIFA

REFA aliyewahi kupigwa na wachezaji wa Yanga SC Machi mwaka jana timu hiyo ikifungwa 3-1 na Azam FC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Israel Nkongo Mujuni ndiye atakayepuliza filimbi katika mchezo wa timu hiyo dhidi ya watani wa jadi, Jumapili. 
Nkongo alipigwa na wachezaji wa Yanga baada ya kumtoa kwa kadi nyekundu beki Nadir Haroub 'Cannavaro' akiwa tayari amempa kadi nyekundu kiungo Haruna Niyonzima pia. 
Stefano Mwasyika aliyehamia Ruvu Shooting alimtupia ngumi ya ‘kibondia’ Nkongo na Nadir Haroub ‘Canavaro’ alionekana kuhusika katika vurugu hizo wote wakafungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Mashabiki wa Yanga SC walifanya vurugu kubwa na kuvunja viti Uwanja wa Taifa siku hiyo.

Refa Israel Nkongo akikimbia wachezaji wa Yanga baada ya kutoa kadi nyekundu ya pili kwa Cannavaro

Aliyekuwa kipa wa Yanga, Shaaban Kado akidaka mbele ya John Bocco wa Azam

Mashabiki wa Yanga waling'oa viti ili kumshambulia Nkongo

Nahodha Nsajigwa akizuiwa na Polisi asimsogelee refa baada ya Niyonzima kupewa kadi nyekundu

Vijana mashabiki wa Yanga wakipelekwa rumande kwa tuhuma za kuvunja viti na chini Nkongo akitoka uwanjani kwa msaada wa Polisi


Canavaro akitolewa nje huku huku akilia na kocha wake Papic akimtuliza.

Papic akiwatuliza wachezaji na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi

Canavaro akizuiwa na wenzake asimshushie kipondo refa huyo.

Polisi akiwa ameingia uwanjani ili kutuliza fujo hizo na kutoa ulinzi kwa refa huyo.

Mchezaji John Boko wa Azam FC akimtoka beki wa Yanga Haroub Nadir Canavaro.

Mashabiki wa Azam FC wakishangilia kwa furaha.

John Bocco akishangilia mara baada ya kuipatia timu yake bao la kwanza.

Timu zikiingia uwanjani tayari kwa kuanza mchezo huo.

Yamepita hayo na Nkongo amepewa tena mechi ya Yanga. Marefa wote wanne walioteuliwa kuchezesha mechi hiyo ya watani wa jadi, Simba na Yanga mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wanatambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) 
Mbali na Nkongo atakayepuliza filimbi, wengine ni Hamisi Chang’walu atakayeshika kibendera upande wa jukwaa kuu na Ferdinand Chacha atakayeshika kibendera upande wa pili, wakati mezani atakaa Orden Mbaga.
Waamuzi hao wote wanne, kwanza wana uzoefu wa kutosha kustahili kuitwa wa kimataifa na wote wana beji za FIFA na hii pia si mara ya kwanza kwao kuongoza mechi za watani na kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakijitahidi kufanya vizuri.
Nkongo, Chang’walu na Mbaga wote ni wa Dar es Salaam, wakati Chacha anatokea Bukoba. 
Katika mchezo huo namba 63, kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 5,000 ambako kuna viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648, wakati upande wa viti vya rangi ya bluu kiingilio ni Sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000, VIP C kiingilio ni sh. 15,000, VIP B itakuwa sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tu tiketi moja itapatikana kwa sh. 30,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni katika vituo mbalimbali.
Vituo hivyo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname