Mganga akamatwa na hirizi zenye chura wanaopumua akizitumia kuwauzia wahamiaji haramu wasiweze kukamatwa
katika Operesheni Kimbunga.
Kampeni ya kitaifa ya kuwaondoa
wahamiaji haramu nchini iliyopewa jina la “Operesheni Kimbunga”, imezidi kuibua
mambo mazito baada ya mganga wa kienyeji, kugundulika akitumia uchawi ili
kuwalinda wahamiaji hao wasikamatwe.
. Mganga
huyo aliyefahamika kwa jina la Bw. Bahalaye Gwenda (60), ameifanya kazi hiyo
tangu kuanza kwa operesheni hiyo kwa kuwalipisha wahamiaji haramu sh. 200,000
kila mmoja wasiweze
kukamatwa na vyombo vya dola vinavyofanya kazi
hiyo.
Tukio hilo la kustaajabisha, limetokea katika eneo
la Kigaga, Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma ambapo mganga huyo hutumia hirizi
ambazo ndani yake kuna dawa za kienyeji na vyura wanaopumua kuwauzia wahamiaji
hao.
Taarifa za mganga huyo,
ziliifikia Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo ambapo Mwenyekiti wa
kamati hiyo Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Venance Mwamotto, aliongoza kikosi kazi
cha wajumbe wa kamati, polisi hadi nyumbani kwa mganga.
Kamati hiyo ilipata malalamiko
hayo kutoka kwa wahamiaji ambao walikamatwa mbali ya kupewa dawa na mganga huyo
ambaye ni raia wa nchi jirani ya Burundi.
Mazingira ya kamati kufika
nyumbani kwa mganga huyo yalikuwa kama sinema
ambapo wajumbe wa kamati wakiwa na askari polisi, baada ya kukaribia nyumba
yake mganga akiwa ameshika mzizi mkononi na kibuyu kilichofungwa hirizi,
aliwapa ishara ya kutosogelea nyumba hiyo.
“Wakati tukiwa mbele yake
tukimfuata, alituambia tusisogelee nyumba yake kwani uchawi alionao una nguvu
kubwa hivyo unaweza kutudhuru, hatukumsikiliza tuliendelea kumfuata hivyo
alitupa vifaa vyake chini na kukimbilia ndani.
“Baadhi
yetu walikuwa waoga katika eneo husika wakiogopa
kudhurika, alipoingia ndani, alitokea mlango wa nyuma na kukimbia na sisi baada
ya kuingia ndani, tulichukua vifaa vyake kama
ushahidi,” alisema Bw. Mwamotto.
Aliongeza kuwa, kikosi kazi
alichokiongoza kiliamua kwenda nyumbani kwa mganga huyo kwa lengo la kumkamata
kutokana na malalamiko waliyopata kutoka kwa wateja wake ambao walidai kutumia
fedha nyingi kumpa mtaalamu huyo hivyo walitaka kurudishiwa fedha zao.
Alisema baada ya kuzipasua hirizi
walizozikuta, vibuyu na pembe, walikuta dawa za kienyeji pamoja na chura wazima
wanaopumua. Vitu vingine walivyovikuta ni vitambaa vyeusi, vyeupe, vyekundu na
vitu vingine vya ajabu.
Akizungumzia operesheni hiyo wilayani
humo, alisema wamefanikiwa kukamata sare za Jeshi la Burundi na kofia vilivyokuwa
vikitumika katika matukio mbalimbali ya uhalifu na wahamiaji haramu.“Tunaendelea na operesheni yetu kwa
kushirikiana na viongozi ili kuhakikisha wahamiaji wote haramu wanarejeshwa
nchini mwao tuweze kurudisha amani na usalama,” alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Issa Machibya, alisema
wahamiaji haramu wengi walikuwa wakijihusisha na matukio ya ujangili na
biashara ya silaha zikiwemo za kivita.
Alisema Mkoa huo pekee umewakamata
wahamiaji haramu 4,365 kutoka nchini Burundi katika awamu ya kwanza ya
operesheni iliyosambaa katika mikoa mbalimbali nchini na kuwataka wakazi wa
Kigoma, kushiriki kikamilifu katika vita hiyo.
Kwa mujibu wa kiongozi wa timu ya
Habari na Mawasiliano ya Operesheni Kimbunga, Zamaradi Kawawa, alisema katika
operesheni hiyo awamu ya pili iliyofanyika Mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera,
bunduki moja aina ya SMG, bastola moja, magobole 17 na risasi 115 zikiwemo za
bunduki aina ya SMG 102 na 13 za bastola vilikamatwa.
Wahamiaji haramu waliokamatwa wengi wao ni kutoka nchi za Burundi
ambapo raia wake 114 walikamatwa wakiishi nchini kinyume na sheria na raia 20
wa Rwanda ambao nao walikamatwa katika kipindi hicho
Majira.
No comments:
Post a Comment