Kikundi hicho ndio kilichokamatwa msituni na vifaa mbalimbali zikiwemo CD za mauaji ya Osama Bin Laden, Mauaji ya Idd Amini, Kuandaa Jeshi, Zindukeni Zanzibar, al Shabaab na Mogadishu Sniper.
CD na DVD walizokamatwa nazo wakizitumia kufanya mazoezi
Pia walikutwa na DVD player moja, mashine ya umeme wa jua wati 30, mapanga mawili, visu viwili, tochi moja, betri ya pikipiki, simu tano za viganjani, vyombo vya chakula, jiko la mkaa na jiko la mafuta ya taa.
Vingine ni taa ya chemli, baskeli tatu, ndoo nne za maji, unga wa mahindi kilo 50, mbaazi kiroba kimoja cha kilo 50, mahindi viroba vitatu vyenye uzito wa kilo 150, virago vya kulalia na mfuko wa kijani unaosadikika ni wa kijeshi wenye nembo ya nanga ya meli, yenye mistari kulia na kushoto na nyoka katikati.
Miongoni mwa masharti ya kujiunga na kikundi hicho, yametajwa kuwa ni pamoja na mwanachama kufarakana na familia yake, ili kuonesha utayari wa kutumikia kikundi hicho.
Mwandishi alifika katika kitongoji cha Mwambo, karibu na mlima wa Mwakyolongo uliokuwa ukitumika kwa ajili ya mafunzo hayo na kukutana na mtoa taarifa aliyefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Mtoa taarifa huyo alimtaja mmoja wa vijana (jina limehifadhiwa), ambaye aliachana na mke wake na mwingine ambaye alikataa maonyo ya wazazi wake, na kuwataka wazazi hao kama hawamruhusu ajiunge, bora wamwachie radhi.
Mtuhumiwa Said Mawazo, anadaiwa aligombana na familia yake baada ya kutakiwa na wazazi wake kuacha kushirikiana na watu hao ambapo aliwaambia afadhali atengane na familia yake na sio kuacha kikundi hicho.
Mama mlezi wa kijana huyo, Fatuma Abdalah, alimwambia mwandishi kwamba kijana wao alikataa kusikiliza ushauri wa mtu yeyote na alikuwa tayari kugombana na yeyote aliyejaribu kumzuia au aliyejaribu kuhoji jambo lolote kuhusu kikundi hicho.
“Mimi na baba yake tulijaribu kumkalisha na kumwambia asijihusishe na kikundi hicho, lakini majibu aliyotupa yalitushangaza na hata alidiriki kusema kuwa heri apewe radhi lakini hawezi kuacha kikundi hicho ambacho najua kilijificha kwenye kivuli cha dini,” alidai Fatuma.
Mama huyo alisema hawana namna zaidi ya kuachia sheria ichukue mkondo wake endapo watabainika kujihusisha na mafunzo ya kijeshi, kwani walikuwa wanahatarisha na kuvuruga usalama wa nchi, ingawa vijana hao hawakujua jambo lililokuwa limejificha nyuma yao.
Katika hatua nyingine, walimu wawili wa Shule ya Msimgi Likokona, katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, wameongezwa katika idadi ya watuhumiwa wa kikundi hicho.
Mwandishi alifika kijijini hapo na kuwakuta walimu hao wakiwa stendi ya basi wakienda katika Kituo cha Polisi Nanyumbu, ambako waliitwa kwa ajili ya mahojiano.
Ingawa walimu hao Cheka Salum na Abilah Seleman hawakutaka kuzungumza chohote walipokutana na gazeti hili wakiwa njiani kwenda kituo cha Polisi, lakini Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Salum Omary, alikiri kuwataarifu kuwa wanatakiwa Polisi.
Taarifa kutoka katika kituo hicho, zilibainisha kuwa walimu hao baada kufika kituoni hapo, walihojiwa kisha wakawekwa chini ya ulinzi ambapo Oktoba 12 mwaka huu, walisafirishwa kwenda Mtwara mjini kwa mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Zelothe Steven alipopigiwa simu, alisema polisi inaendelea na upelelezi na ukikamilika, atatoa taarifa kamili
No comments:
Post a Comment