17 October 2013

Kumekucha! Coastal Union yafukuza Kocha Mkuu

COASTAL Union ambayo ni miongoni mwa timu zilizosajili kwa gharama msimu huu, imemtimua Kocha Mkuu Mzanzibari, Hemed Morocco, kwa madai ya kutoridhishwa na kiwango cha uchezaji wa timu hiyo.
Timu hiyo ina pointi 11 sawa na Kagera Sugar wakiwa na tofauti ya mabao na inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Imeshacheza mechi nane, ikashinda mbili, kutoka suluhu tano na imepoteza mchezo mmoja dhidi ya timu dhaifu, Ashanti.
Ofisa Habari wa Coastal Union, Edo Kumwembe, aliliambia
Mwanaspoti kuwa uongozi wa klabu yake ambao ulikutana juzi Jumanne, umefikia azimio la kutomwongezea Morocco mkataba baada ya ule wa awali kumalizika tangu Septemba 31.
“Kwa sasa timu itakuwa chini ya Ally Mohamed ‘Kidi’ na ndiye atakayeiongoza kwenda Kagera, mpaka hapo atakapopatikana kocha mwingine, tunaangalia uwezekano wa kuchukua kocha kutoka nje ya nchi,” alisema Kumwembe.
Alisema wamefikia uamuzi wa kutomwongezea mkataba Morocco baada ya kutoridhishwa na viwango vya wachezaji wakati wanaamini usajili waliofanya ni mzuri.
Mwanaspoti linajua kwamba kocha huyo amenyimwa mkataba kutokana na staili yake ya kujilinda na kuogopa kushambulia akihofia kupoteza mchezo. Uongozi umetafsiri staili hiyo kama kuishiwa mbinu hasa kwa aina ya wachezaji waliosajiliwa.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname