03 October 2013

Haya ndiyo usiyoyajua kuhusu Miss Tanzania 2013; Happiness


 
WAKATI mshindi wa jumla wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2011 wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa) Shomari Kapombe akizaliwa mwaka 1994, katika kijiji cha Kishozi, Kagera alizaliwa mtoto wa kike ambaye hakudhaniwa iwapo siku moja angefika mbali kimtazamo, kiakili, kifikra na katika masuala ya ulimbwende.

Mtoto huyu alipewa jina la Biera lenye uhalisia wa kabila la Wahaya na baba yake ambaye alifariki baada ya yeye kutimiza umri wa mwaka mmoja. Alianza kulelewa na mama yake Amina Bukoko katika mji wa Tabora wakati huo mama yake akiwa na umri wa miaka 21 tu.

Huyu ni Happiness Watimanywa aliyetawazwa kuwa Miss Tanzania Septemba 21, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 19.
Mwanaspoti lilimtafuta mrembo huyu na kufanya mahojiano naye kama ifuatavyo...

Mwanaspoti: Wewe ni msomi na mrembo, unadhani urembo hasa ni nini?

Happiness: Kama unataka kuwa mrembo si lazima uvutie tu machoni mwa watu, kuna vitu vingi. Kwanza unapaswa kuwa mrembo wa umbo na sura hata hivyo uwe na vigezo vyote kwa kuitwa mrembo. Pili ni tabia, unapaswa kuwa mrembo wa roho na nafsi  (inner beauty) huwezi kuwa mrembo kisha ukafanya vitu vilivyo tofauti na urembo wako. Pia vilevile uweze kutambua udhaifu ulionao na kuurekebisha.

Mwanaspoti: Ni makosa gani ambayo unahisi yalifanywa na warembo waliowahi kutwaa taji la Miss Tanzania na umejipanga vipi kuyarekebisha na matarajio yako ni nini katika kuibadili sekta ya urembo nchini?

Happiness: Sidhani kama kuna makosa yaliyofanywa na warembo waliopita, ila kuna baadhi ya vitu ambavyo Watanzania wanasahau kwamba mrembo naye ni binadamu. Kuna vitu atavifanya ambavyo huenda vinaweza kuonekana kuwa na utofauti, ni kama binadamu wa aina nyingine. Lakini kikubwa ni kutekeleza masuala ya kijamii na yeye mwenyewe anavyoishi katika jamii. Kujijengea uwezo wa kufikiri ni nini utaifanyia jamii, si kuishia kuvaa taji ila ni zaidi ya ulimbwende.

Mwanaspoti: Umewahi kutembelea vivutio mbalimbali hapa nchini na je umejipanga vipi katika kuhamasisha utalii wa ndani?

Happiness: Nina mipango mingi na mizuri kuhusu hilo. Kwanza mimi nimekuwa mtalii mzuri na nilianza utalii wa ndani nikiwa mdogo kabla sijaingia katika masuala ya ulimbwende. Nimewahi kutembelea Mikumi, Serengeti, Manyara na nimewahi kufika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Nilikwea mlima huo mwaka 2011 na kufanikiwa kufika katika kilele cha Uhuru, nikiwa huko nilishuhudia mambo mengi sana na nilipata uzoefu mkubwa. Nimewahi kushuhudia mengi na Tanzania imebarikiwa vitu vingi. Nimeshawahi kuona simba anapanda mti nadhani ni uzoefu tosha, nimepanga kuhamasisha utalii wa ndani na kukaribisha wageni kutembelea nchi yetu.

Mwanaspoti: Ukiwa Miss Tanzania 2013, pia ulililetea sifa taifa kwa kuongoza katika somo la Uhasibu kati ya nchi 150, hebu tuambie ilikuwaje na vipi bado unaendelea na somo hilo?

Happiness: Nilikuwa nikilipenda somo la Uhasibu tangu nikiwa kidato cha kwanza licha ya kufanya vizuri katika somo la hisabati tangu shule ya msingi. Kwanza tulikuwa na mitihani ya IGCSE; mitihani hii tuliifanya kawaida sana ila kwa kuwa nilikuwa mdadisi sana hasa nisipomwelewa mwalimu wangu ilinisaidia kuweza kufanya vizuri. Hata hivyo alama zangu darasani zilikuwa ni kuanzia 90 mpaka 100 sikushuka chini ya hapo.
Nakumbuka niliitwa katika shule niliyokuwa nikisoma St Costantine International School, Arusha wakati wa mahafali ya kidato cha nne na kupewa habari hiyo njema, nilifurahi sana. Mtihani niliufanya mwaka 2009 na majibu nilipewa 2010. Lakini kidato cha tano na sita nilisoma masomo yaliyo nje ya mchepuo yaani Jiografia, Historia na Uhasibu, sikuhitaji masomo ya mchepuo

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname