Katika hali isiyo ya kawaida, mkazi wa Kijiji cha Lorwe Kata ya Nyahongo
Shirati, wilayani Rorya, mkoani Mara, Charles Warito (38), ambaye ni
shahidi wa mlalamikaji katika Kesi ya kudhuru mwili kwa kujeruhiwa
vibaya kwa kukatwa mkono na kusababisha ulemavu amefariki dunia, wakati
akitoa ushahidi.
Warito alikutwa na umauti huo akiwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya
ya Tarime mbele ya Jaji G. Ndika anayesikiliza kesi katika Wilaya za
Tarime na Rorya.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana mchana baada ya Mwanasheria wa
Serikali, Mayega na Mwendesha Mashitaka wa Polisi Inspekta George
Lutonja walimwita kuingia Kizimbani tayari kutoa ushahidi.
Shahidi huyo alianza kutoa ushahidi wake na alieleza kushambuliwa kwa
kukatwa mapanga na mtuhumiwa Kichohe Kichere ambaye ni mkazi wa Kijiji
cha Omoche Kata hiyo ya Nyahongo Shirati Januari 26, mwaka 2008 na
kutokana na majeraha aliyoyapata kwa kukatwa mkono na mwili wake ulianza
kupooza na kulemaa upande wa kulia ambao mkono ulikatwa
Alipoanza kujibu maswali kutoka kwa wakili wa mtuhumiwa mara alianza
kulegea na kuishiwa nguvu na kuanguka kizimbani na kuzimia hali
iliyofanya Mahakama hiyo Kusitisha Kusikiliza kesi na shahidi huyo
kukimbizwa Hospitali ya Wilaya kupatiwa matibabu na alifariki kabla ya
kupatiwa matibabu.
Mtuhumiwa katika kesi hiyo akiondoka haraka mahakamani hapo huku ndugu
wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina Otieno Rada alisema:
"Nimesikitishwa na kifo hiki cha ndugu yangu Charles Joseph kwani
majeraha hayo aliyoyapata ya kukatwa mkono na Kichere yalisababisha
alemae mkono na kuanza kupooza na yamechangia kifo chake."
Mwili wa marehemu Charles umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya Tarime
ukisubili kuchukuliwa na ndugu zake kutoka Kijiji cha Lorwe Kata ya
Nyahongo Shirati kwa maziko
No comments:
Post a Comment