Imeandikwa tarehe 29 Septemba 2013 By Eric Anthony, Kigoma
KAMPENI ya kitaifa ya kuondoa wahamiaji
haramu nchini iliyopewa jina la Operesheni Kimbunga, imefanikiwa
kusambaratisha kijiji cha wahamiaji haramu wa Burundi waliokuwa
wamejitengenezea dola yao nchini, kiasi cha
hata kutumia sarafu ya Burundi ilihali wakiwa Tanzania.
Aidha, watoto wao wanasoma shule kwa
mitaala ya Burundi, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha kwa lugha ya
Kifaransa wakiwa kijijini Nyamugali, Mvugwe wilayani Kasulu, Kigoma.
Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa
Kigoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa,
Issa Machibya katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake
mjini hapa.
Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya wakazi
wa mkoani Kigoma, wakiwemo wa Manispaa ya Kigoma Ujiji na wilaya za
Kasulu na Buhigwe, wamepongeza hatua hiyo.
Wameitaka serikali kutorudi nyuma katika
kuhakikisha inawaondoa nchini wahamiaji haramu ambao wametajwa kuwa
tishio kwa usalama wa nchi kutokana na kujihusisha na matukio ya
ujangili, biashara ya silaha zikiwemo za kivita, na matukio mengine.
Akizungumza mjini hapa, Machibya alisema
mbali ya kutumia faranga (fedha za Burundi) kwa matumizi yao ya kawaida
wakiwa nchini na kufundisha kwa mitaala ya nchi waliyotoka, wahamiaji
hao walipeperusha pia bendera ya nchi yao katika sehemu mbalimbali za
kijiji hicho.
“Lakini kwa sasa, wote wamekimbia na
kuziacha nyumba zao. Huwezi kuamini kama ni nyumba za wahamiaji haramu,
kwani walijijenga na kuishi watakavyo, tena bila ya hofu katika nchi ya
kigeni.
“Hebu tafakari, ni dharau gani unaishi
Tanzania, lakini hata pesa yao hutumii, badala yake unatumia
faranga.Tunashukuru tumewasambaratisha, na tutaendelea na operesheni hii
mpaka tuhakikishe Watanzania
wanaishi kwa amani katika ardhi yao,” alisema Machibya.
Inakadiriwa kuwa, idadi ya wahamiaji
haramu waliokuwa wanaishi kijijini hapo, lakini sasa wakiwa wamekimbia
mkono mrefu wa Operesheni Kimbunga, ni zaidi ya 600.
Mkoa wa Kigoma pekee umenasa wahamiaji
haramu 4,365 wa Burundi katika awamu ya kwanza ya operesheni hiyo
iliyosambaa katika mikoa mbalimbali nchini, lakini Machibya amewataka
Wana-Kigoma kushiriki kikamilifu
katika vita dhidi ya wahamiaji haramu hasa katika awamu hii ya pili na nyinginezo.
“Tatizo lililopo ni usiri. Wengi
wameshindwa kutoa ushirikiano, na kufanya wengi tuishi nao kana kwamba
ni Watanzania wenzetu… Watanzania waelewe hawa si watu wema, wangekuwa
wema wangefuata taratibu za kuishi nchini, lakini wamekuwa wakiishi kwa
ujanja ujanja mno. Mshona nguo za RC “Miongoni mwao ndimo walimo
mawakala wa silaha za kivita, mabomu ya kurusha kwa mkono na biashara
nyingine haramu.
Hatuwezi kukubaliana na hali hii,”
alisema Machibya na kutoa mfano unaoendelea kumshangaza hata yeye
mwenyewe kuwa, fundi maarufu aliyekuwa anashona nguo za baadhi ya Wakuu
wa Mkoa wa Kigoma, akiwemo
yeye mwenyewe na mtangulizi wake, John Simbakalia ni mtuhumiwa wa uhamiaji haramu.
“Ndiyo, hata kabla yangu ndiye aliyekuwa
anashona nguo za baadhi ya ma-RC (Wakuu wa Mkoa) hapa Kigoma,
Simbakalia ni miongoni mwao na mimi mwenyewe amenishonea suti
mbili…nikanogewa na kutaka kushona suti
nyingine, sasa nikiwa na kitambaa
changu, kila nikipita nakuta ofisi zimefungwa, zaidi ya mara nne
nimepita... kuuliza naambiwa ni wale wale, wameamua kujisalimisha kabla
ya kunaswa.
“Sasa mambo haya yanatokea hapa mjini,
si huyo tu, kuna wengi wanaendelea kusombwa…lakini kama Serikali ya
mkoa, tunasema wawe hapa mjini au mahali popote pale, operesheni hii
itawanasa na tunamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuunga mkono,”
alisema.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkuu wa Kambi
ya Wakimbizi ya Nyarugusu, wilayani Kasulu, Frederick Nisajile,
alipongeza kazi nzuri inayofanywa na serikali, huku akishauri mianya
mingine ya kuzalisha wahamiaji haramu au hata kugawa uraia kiholela kwa
wakimbizi ifungwe kwa sababu za kiusalama.
“Kwa idadi hii ya wahamiaji na
wakimbizi, usalama wa nchi uko hatarini. Kuna mengi ya kufanyiwa kazi
ili kuhakikisha nchi haiingiliwi,” alisema Nisajile ambaye amefanya kazi
na wakimbizi kwa takribani miongo miwili.
Mkazi mwingine wa mjini Kigoma, eneo la Burega ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutajwa jina, alisema,” Kigoma imevamiwa.
Mbaya zaidi watu wanafichiana siri,
lakini wahamiaji ni wengi, wakiwemo wafanyabiashara wakubwa. Nao wanaita
ndugu zao na kuzidi kuijaza nchi yetu, wakiishi bila kufuata taratibu.
Naipongeza serikali kwa kuanza
kukabiliana na wimbi hili la wahamiaji haramu.” Naye Kiongozi wa Timu ya
Habari na Mawasiliano ya Operesheni Kimbunga, Zamaradi Kawawa,
akizungumza kwa njia ya simu kutoka
Biharamulo, Kagera alisema anafarijika
kuona operesheni inang’ata kila sehemu, huku akiahidi kutoa taarifa ya
utekelezaji wa awamu ya pili ya operesheni inayoendelea kote nchini.
Operesheni Kimbunga ilianzishwa kwa
lengo la kukabiliana na vitendo vya uhalifu vilivyokithiri vikiwemo
ujambazi wa kutumia silaha, ujangili, utekaji wa magari na mauaji ya
kikatili pamoja na migogoro ya ardhi inayotokana na wafugaji kutoka nchi
jirani kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho.
Ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya
Kikwete alilolitoa Julai 29, 2013 akiwa katika ziara ya kikazi mkoani
Kagera, akitaka kufanyika kwa operesheni maalumu ya kuondoa uhalifu
katika mikoa ya Kagera, Kigoma na
Geita ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na kuwepo kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.
Operesheni Kimbunga inayoongozwa na
Brigedia Jenerali Mathew Sukambi ilianza Septemba 6, 2013, baada ya
kupita wiki mbili alizokuwa amezitoa Rais Kikwete kwa kuwataka wahamiaji
wanaoishi nchini bila kufuata sheria kuondoka kwa hiari yao au
kuhalalisha ukazi wao nchini.
source; HabariLeo
No comments:
Post a Comment