MTANDAO wa wauza madawa ya kulevya unazidi kupukutika Bongo kufuatia
madai ya kukamatwa kwa watu wanaodaiwa kujishughulisha na ubebaji
‘punda’ wa biashara hiyo haramu, Ijumaa Wikienda lina mtiririko wote.
Hivi karibuni, Video Queen wa Wimbo wa Masogange, Agnes Gerald
‘Masogange’ amedaiwa kunaswa nchini Afrika Kusini ‘Sauzi’ akiwa na kilo
mia moja na hamsini za unga unaoaminika ni sehemu ya madawa ya kulevya.
Ameshapanda kortini mara moja Ijumaa iliyopita.
Wakati Masogange
akisota Sauzi kwa madai hayo mazito, habari ya mjini kwa sasa ni ya
mtalaka wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ally Mohammed ’Z-Anto’, Sandra
Khan au Binti Kiziwi kudaiwa kutupwa jela miaka mitano kwa sakata la
‘unga’.
HABARI YA MJINI KWA SASA NI BINTI KIZIWI
Kuanzia Alhamisi
iliyopita, habari zilizoligubika Jiji la Dar ni kuwa Binti Kiziwi
amenyongwa nchini China baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na
madawa ya kulevya.
Kwa mujibu wa mitandao, Binti Kiziwi alinyongwa wiki mbili zilizopita.
Hata hivyo, mitandao hiyo haikusema kama mrembo huyo alinyongwa hadi
kufa au la! Sheria za hukumu hiyo, mwenye hatia anatakiwa kunyongwa hadi
kufa.
UKWELI WA BINTI KIZIWI NI HUU
Baada ya kusambaa kwa manenomaneno
hayo, Ijumaa Wikienda liliingia mtaani kuisaka familia ya Binti Kiziwi
lakini bila mafanikio.
Kwenye makazi ya mama yake, Buguruni, Dar,
majirani walisema mzazi huyo amehama baada ya kufunga ndoa siku chache
kabla ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
IJUMAA WIKIENDA LAZIDI KUCHIMBA
Ijumaa Wikienda lilizidi kuzama
ndani katika kuchimbua tetesi hizo ambapo lilifanikiwa kumpata ndugu wa
kiume wa Binti Kiziwi na kufanya naye mazungumzo kama ifuatavyo:
Wikienda: Samahani, nimeambiwa wewe ni ndugu wa Binti Kiziwi, ni kweli?
Ndugu: (huku akitaja uhusiano wao) Ni kweli, nikusaidie nini?
Wikienda: Kuna manenomaneno kwamba Binti Kiziwi amenyongwa nchini China
baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na madawa ya kulevya, ni kweli?
Ndugu: Sijui hizo habari watu wanazipatia wapi?! Watanzania wana maneno sana. Si kweli ndugu mwandishi.
Wikienda: Ukweli ni upi?
Ndugu: Kwanza kabisa Binti Kiziwi hakukamatiwa China, alikamatiwa Hong
Kong, kwa sheria za kule mtu akipatikana na hatia ya kukutwa na ‘unga’
anahukumiwa jela tu.
“Binti Kiziwi amehukumiwa miaka mitano jela Hong Kong, na si China. Watu wajue hilo na miaka mitano si mingi, atatoka.”
Wikienda: Nashukuru sana kwa ushirikiano ndugu yangu.
Ndugu: Asante, waambie Watanzania waache kuongeaongea sana.
source-GPL
No comments:
Post a Comment