MSHTUKO mkubwa ulijiri Jumamosi iliyopita, ikiwa ni baada ya kusambaa
kwa habari za kumwagiwa tindikali, mfanyabiashara mwenye ‘levo’ ya
ubilionea, Said Said Mohammed, 42, ambaye ndiye mmiliki na Mkurugenzi
Mkuu wa Home Shopping Centre.
Said ambaye kwa utambulisho mwingine
anajulikana kama Said Mohammed Saad, alimwagiwa tindikali Ijumaa
iliyopita, saa 2 usiku, lakini habari zake zikavuma Jumamosi, hivyo
kuibua taharuki ya aina yake.
Kuhusu nani alimmwagia tindikali hiyo,
sababu ya kutendwa unyama huo, yupi mhusika mkuu wa ukatili wenyewe na
malengo ya uharamia, kwa jumla, hayo ni maswali yanayoendelea kuitesa
familia yake, watu wa karibu pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania.
Taarifa za kipolisi zinathibitisha kwamba alimwagiwa tindikali akiwa
anazungumza na mfanyakazi wake wa duka lake lililopo kwenye Jengo la
Msasani City Mall kisha akakimbizwa Hospitali ya Ami Wellness Centre,
iliyopo Masaki, Dar es Salaam kabla ya kupelekwa Afrika Kusini kwa ndege
ya kukodi ndani ya kipindi kisichozidi dakika 60.
SAID NI NANI?
Ni Mtanzania mwenye asili ya Bara la Asia. Inadaiwa kwamba ndugu zake wengi wana asili ya nchi za Yemen na Saudi Arabia.
Ndiye mmiliki wa Kampuni ya Home Shopping Center. Kampuni hiyo ina
maduka mengi Dar es Salaam na katika mikoa kadhaa ambayo yanahusika
zaidi na uuzaji wa vitu vya nyumbani na ofisini.
Anatajwa kuwa tajiri mwenye uwezo zaidi katika jumuiya ya wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo, kifedha na ushawishi.
Inadaiwa kwamba wafanyabiashara wengi wenye maduka yao Kariakoo,
humtegemea yeye kuingiza mizigo nchini, kutokea nje ya nchi hususan
China.
Anamiliki nyumba kadhaa za ghorofa Kariakoo, yapo madai kwamba anamiliki nyumba sita.
Baadhi ya majengo ambayo anahusishwa nayo, la kwanza lina ghorofa saba,
lipo Mitaa ya Swahili na Msimbazi, la pili lina ghorofa sita, lipo
Kongo na Aggrey, tatu ni la ghorofa nne, lipo Barabara ya Uhuru na
kadhalika.
Said kupitia kampuni
yake ya Home Shopping Centre, aligeuka nyota ya jaha kwa familia 655,
zilizokumbwa na mafuriko eneo la Jangwani, Desemba 2011 kisha kuhamishia
Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa moyo wake
mwema, Said aliidhinisha kila familia ipewe seti kamili ya vyombo vya
nyumbani pamoja na taa zinazowaka kwa kutumia nishati ya mwanga wa jua.
Misaada hiyo, ilikabidhiwa na mkurugenzi mwingine wa Home Shopping
Centre, Ghalib Said Mohammed ambaye ni mdogo wa Said. Misaada hiyo,
ilipokelewa na Rais Jakaya Kikwete, Januari mwaka jana.
Said hakuishia hapo, baada ya misaada ya vyombo na taa za nishati ya
mwanga wa jua, alifanya jambo jema zaidi kwa kujenga shule ya msingi,
madarasa yote pamoja na ofisi za walimu, vilivyojengwa kwa ufadhili wa
Home Shopping Centre.
Machi mwaka huu, shule hiyo ilizinduliwa na
Rais Kikwete ambaye alikiri kwamba ujenzi wake utarahisisha upatikanaji
wa huduma za kijamii kwenye eneo hilo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam,
Yusuf Mrefu, alisema kuwa uchunguzi unaendelea kuhusiana na tukio la
Said kumwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu.
Mrefu alisema, Said
alikuwa akizungumza na mfanyakazi wake nje ya duka lake kwenye Jengo la
Msasani Mall kisha akatokea kijana mrefu mwembamba ambaye alimmwagia
kimiminika kinachosadikiwa kuwa ni tindikali.
Kamanda huyo wa polisi
aliongeza kwamba mfanyakazi huyo wa Said, Hassan Ahmad, naye
alijeruhiwa kidogo katika purukushani hiyo lakini alipopelekwa Hospitali
ya Ami Wellness Centre, alitibiwa na kuruhusiwa.
Iadaiwa kuwa Hassan, alipata majeraha baada ya kuanguka, wakati akimfukuza jamaa huyo ambaye alimmwagia tindikali Said.
Mmoja wa wauguzi katika Hospitali ya Ami Wellness, alimwambia mwandishi wetu kwamba baada ya Said
kufikishwa pale, ilichukua kama nusu saa, akachukuliwa kupelekwa Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tayari kwa safari ya kwenda
Afrika Kusini.
“Hali yake ilikuwa mbaya, lile jicho moja
limeathirika sana, kwa kweli sijui kama litaweza kuona tena. Ila moja
litakuwa salama, ukizingatia amepelekwa katika hospitali yenye ubora
zaidi. Yule mfanyakazi wake aliumia kidogo tu, alitibiwa na kuruhusiwa
siku ileile,” alisema muuguzi huyo.
Kuhusu jina la hospitali
aliyopelekwa, alisema: “Hakukuwa na utaratibu wa kuandika rufaa,
alichukuliwa tu kupelekwa Afrika Kusini na sasa naamini anaendelea na
matibabu vizuri. Ila inasikitisha sana, naamini wahusika walitaka
kumfanya awe kipofu.”
Kwa mujibu wa taswira ya
tukio lenyewe, kitendo alichofanyiwa ni umafia na mambo kadhaa yanafaa
kumulikwa kwa undani. Mambo hayo ni;
Said ana uadui na nani? Aliyemmwagia alijuaje kama yupo pale? Kwa nini tindikali machoni?
Ni wazi Said anao maadui ndiyo maana kitu kile kimetendeka. Bila shaka
aliyemmwagia aliambiwa na mtu, huyo anafaa kupatikana. Bila kupindisha
ukweli ni kwamba mmwagaji alikusudia kumfanya Said awe kipofu.
Polisi wanatakiwa kuchunguza nyendo za Said, kuona ana uhasama na akina
nani katika biashara au hata kwenye mambo ya kijamii. Kadhalika,
ichunguze mawasiliano ya watu wa karibu na Said, atajulikana mtoa
taarifa, hivyo kumpata mhusika wa ukatili pamoja sababu ya unyama
wenyewe.
SKENDO ZA SAID
Said ameshawahi kuripotiwa na
vyombo vya habari katika kashfa mbalimbali, gazeti moja liliwahi
kuandika matoleo kadhaa, likimtaja kama mfanyabiashara hatari kwa nchi
ya Tanzania.
Vilevile, alishawahi kuripotiwa kumfanyia unyama,
kijana mmoja raia wa Lebanon ambaye alidaiwa kuwa na uhusiano wa
kimapenzi na dada yake.
GPL
No comments:
Post a Comment