SIKU chache baada ya aliyekuwa mkali wa Hip Hop Bongo, Albert Kenneth
Mangweha ‘Ngwea’ kupumzishwa kaburini kufuatia kifo cha usingizini
nchini Afrika Kusini kilichotokea Mei 28, mwaka huu, mambo kibao
yanazidi kuibuka.
Habari zinadai kuwa familia ya marehemu Ngwea
imemkataa mtoto aliyeletwa na mama yake makaburini akidaiwa kuwa ni
mtoto wa Ngwea.
MTOTO WA NGWEA
Juni 6, mwaka huu wakati wa
mazishi, mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Paulina Jeremiah, mkazi
wa Kigamboni, Dodoma alitimba akiwa na mtoto huyo wa kike aitwaye Neema
Albert na kudai kuwa alimzaa na Ngwea mwaka 2001, wakati msanii huyo
akisoma Sekondari ya Mazengo.
Wakati akijieleza, ndugu wa Ngwea,
Anthony Mangweha alikuwa akimsikiliza ambapo aliwataja wanandugu wa
marehemu waliokuwa wakijua suala hilo.
Waliotajwa kujua kuwa mtoto
huyo alikuwa wa Ngwea ni Frank, Jotam na Amani ambao waliwahi kutumwa na
marehemu kwenda kumwangalia mkoani Dodoma.
Hata hivyo, ndugu huyo aliyekuwa akimsikiliza alimtaka mama Neema kupoa, hadi familia ikae kikao.
FAMILIA YAKAA KWA SAA 7, YATOA UAMUZI MZITO!
“Kweli
wikiendi iliyopita familia ilikaa kikao kwa zaidi ya saa 7, pamoja na
mambo mengine lakini wanadaiwa kufikia uamuzi mzito wa kumkataa mtoto
huyo hadi mama Neema apeleke vigezo vya uthibitisho,” kilisema chanzo
chetu ndani ya kikao hicho.
Akizungumzia suala hilo kwa sharti la
kutotajwa gazetini, mmoja wa dada zake Ngwea alisema: “Ni kweli yule
mtoto aliondoka na mama yake lakini kama akileta uthibitisho
tutampokea.”
MICHANGO YA RAMBIRAMBI YAHOJIWA
Habari
ziliendelea kudai kuwa katika kikao hicho, suala la michango ya
rambirambi lilihojiwa huku wanafamilia wakitaka kujua kilichopatikana,
kilichopo na namna zilivyotumika.
“Unajua kuna wajanja wengi ‘so’ familia ilikuwa na wasiwasi kuwa inawezekana kukawa na uchakachuaji,” kilidai chanzo chetu.
Ilisemekana
kuwa mmoja wa baba wadogo wa marehemu Ngwea alitoa ufafanuzi kwa
kumwaga data na kueleza namna zilivyotumika na kiasi kilichobaki ambacho
kiliwekwa benki.
MALI ZA NGWEA ZAZUA UTATA
Ilidaiwa kuwa
mengine yaliyojiri katika kikao hicho na kuzua utata ni pamoja na mali
alizoacha marehemu Ngwea na namna ya kuzikusanya na kuzisimamia.
“Ilisemekana
aliwahi kumiliki magari mawili kwa nyakati tofauti lakini aliyauza.
Vitu vyake alivyoviacha kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Sinza-Mori, Dar
vilitakiwa vijulikane ili visafirishwe hadi hapa kwa mama yake,”
kilisema chanzo.
Kuna madai kuwa kuna mtu ambaye Ngwea aliwahi
kumwambia kuwa alikuwa na kiwanja Goba, nje kidogo ya Jiji la Dar lakini
hakuna anayekijua.
Ngwea alifariki dunia Mei 28, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 30 katika kifo tata huko Sauzi.
M 2 THE P HAKUMBUKI KILICHOTOKEA
Wakati
huohuo, msanii aliyepata masaibu na Ngwea huko Sauzi lakini akapona,
Mgaza Pembe ‘M2 THE P’, wakati anatimua mjini hapa baada ya mazishi,
alipotakiwa kueleza kilichowapata hadi Ngwea akafariki dunia, alimwambia
mwanahabari wetu kuwa hakumbuki chochote kilichotokea.
Jamaa huyo
alidai kuwa bado anaumwa hadi sasa licha ya kuruhusiwa kutoka katika
Hospitali ya St. Hellen Joseph ya Afrika Kusini alikolazwa.
No comments:
Post a Comment