TUKIO la kuuawa kwa mfanyabiashara kijana mwenye mafanikio, Ayoub Mlay,
siyo tu linaacha simanzi kwa Watanzania bali pia ni fundisho kwa jamii
na serikali.
MLAY, alifariki dunia usiku wa Alhamisi iliyopita, Mei
16, mwaka huu baada ya kupigwa risasi kwenye Klabu ya Ambrosia, iliyopo
Kawe Beach jijini Dar es Salaam.
Simanzi inakuja kwa sababu Mlay, 38,
alikuwa mfanyabiashara kijana aliyeonesha mafanikio na kupiga hatua
kubwa, amefikwa na mauti akiwa bado na moto wa kusaka maendeleo zaidi
kwenye biashara zake na maisha kwa jumla.
Kwa Conrad ambaye ni kijana
mdogo pia, anaingia kwenye
msukosuko lakini nyuma yake kuna funzo la
umiliki na matumizi sahihi ya silaha za moto ambazo kwa sasa zimekuwa
kama ‘fasheni’ kwa vijana wengi wa mjini.
WOTE NI WATOTO WA ARUSHA
Mlay ni mfanyabiashara wa Arusha ingawa mara kwa mara hupatikana Dar es Salaam kutokana na mizunguko yake ya kibiashara.
Conrad, naye ni mwenyeji wa Arusha, ingawa kwa sasa makazi yake yapo Dar es Salaam.
Kuhusu
kazi ya Conrad, mmoja wa watu waliohojiwa na gazeti hili nje ya Klabu
ya Ambrosia, alisema: “Kwa kweli huwa tunamuona, wengi tunamuona ni
mtoto wa mjini tu, kwani hatujui anajishughulisha na nini.”
CHANZO CHA UGOMVI
Mtoa
habari wetu aliyeomba hifadhi ya jina lake gazetini, alisema kuwa Mlay
na Conrad ni watu waliokuwa wanafahamiana na kuna jambo walikuwa
wanazungumza.
“Siyo rahisi sana kujua walichokuwa wakizungumza ila
baadaye yalitokea mabishano. Walitaka mpaka kushikana ili kupigana, watu
wakawazuia. Inaonekana Conrad hakukubali, maana aliamua kutoka nje
mbio.
“Kwa haraka haikujulikana alifuata nini kule nje, tuliokuwepo
tuliamini ameamua kukimbia lakini kumbe alikuwa amefuata bastola.
Aliporudi, alikuwa na bastola mkononi, baada ya hapo hata hakutaka
kuzungumza maneno mengi, alimpiga Mlay risasi kisha akataka kutoweka,”
kilisema chanzo chetu.
WALINZI WALIVYOMDAKA
Chanzo chetu
kilibainisha kuwa wakati anapita na bastola kuingia ndani, walinzi
walimpisha kwa sababu ya kuhofia usalama wao lakini kipindi cha kutoka,
walijipanga kumdhibiti.
Kiliendelea kusema, Conrad akiwa anatoka,
walinzi walifanya kama wanampisha na baada ya kupita, walimbana mikono
na kumnyang’anya bastola kisha wakamfunga kamba kabla ya kupiga simu
kuita polisi.
Dakika kadhaa baada ya kupiga simu, polisi walifika na
kufanya mahojiano na watu waliokuwepo eneo la tukio, kabla ya kumchukua
mtuhumiwa na kumpeleka Kituo cha Polisi Kawe, Dar es Salaam.
Vilevile,
polisi walimchukua Mlay na kumuwahisha Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu,
Kinondoni, Dar es Salaam ili akapatiwe matibabu lakini baadaye
ilibainika alikuwa ameshakata roho.
ADAI KUHUSU MATUMIZI MABAYA YA SILAHA
Kwa
mujibu mtu aliyejitambulisha kwa jina la Matidau, Conrad alikuwa na
mazoea ya muda mrefu ya kuonesha bastola yake na kuwatishia watu
aliotofautiana nao.
“Tunamjua Conrad, kuna watu walishamwonya lakini
hakusikia, ikafikia wakati kwamba anapoanza ugomvi, basi tunaomjua
tunakaa mbali naye kwa sababu lolote linaweza kutokea.
“Kuna kipindi
alinyang’anywa bastola kwa sababu ya tabia yake ya kuioneshaonesha ovyo
pamoja na kutishia watu. Tukio hili la mauaji ya Mlay linatufanya
tujiulize hiyo bastola alirejeshewa katika mazingira gani au ni
nyingine?” kilihoji chanzo.
MINONG’ONO KUHUSU FEDHA
Kuhusu
kile ambacho Mlay na Conrad walibishana, kulikuwa na maneno ya pembeni
kutoka wa watu waliokuwepo eneo la tukio kwamba chanzo cha ugomvi ni
fedha.
“Unajua inapotokea matukio makubwa kama haya, watu wa eneo la
tukio wakati mwingine ndiyo huwa wa kwanza kupotosha. Kwa mfano, yapo
madai kuwa Mlay alimtuma kazi Conrad, sasa baadaye kukawa na mabishano
kuhusu malipo.
“Yote yatazungumzwa lakini jambo ni baya sana. Fikiria
kwamba Mlay ni mtu aliyekuwa ameajiri watu, ana familia na marafiki,
wote hao wataathirika kwa namna moja au nyingine kwa kumpoteza mtu
waliyempenda,” alisema mtoa habari wetu.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Dar es Salaam, ACP Charles
Kenyela alisema kuwa ni kweli tukio hilo lilitokea na akaongeza kuwa
Conrad alimfyatulia Mlay risasi ya kifua.
Kuhusu madai kwamba Conrad
ni mzoeafu wa tabia za kuchezea silaha na kutisha watu kiasi kwamba hata
jeshi lake lina taarifa na liliwahi kumnyang’anya kabla ya kumrudishia
kinyemela, Kenyela alijibu: “Hizo taarifa sina, ngoja nizifuatilie
kwanza, maana siwezi kuzungumza jambo nisilo na uhakika nalo.
“Nilicho na uhakika nacho ni hiki; kwamba mtuhumiwa tunamshikilia na tutamfikisha mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.”
KIFUATACHO
Bado
kuna maswali kuhusu tukio hili, timu nzima ya Kampeni ya Fichua Maovu
ya Global Publishers, imejipanga sawasawa kufuatilia kwa kina na mara
itakapokamilika, mambo yatakuwa hadharani
kupitia magazeti yake ambayo ni damu moja na hili; Risasi, Amani, Ijumaa na Ijumaa Wikienda.
Source:Global Publishers

No comments:
Post a Comment