Mtoto Junior Justine (3) aliyetelekezwa na mama yake mzazi.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea hivi karibuni katika kituo cha
mabasi yaendayo mikoani, Ubungo jijini Dar es Salaam ambapo mtoto huyo
aliokolewa na msamaria mwema.
INASIKITISHA SANA
Akisimulia mkasa mzima ulivyokuwa, shangazi wa
mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Monalisa, alisema wao kama
familia wameumizwa sana na kitendo kilichofanywa na Maya.
“Maya
amezaa na kaka yangu Justine anayeishi Marekani na amekuwa akimjali sana
kwa kumtumia fedha za matumizi mara kwa mara. Kisa ni kwamba kaka
alimwambia Maya ampeleke mtoto Bukoba (nyumbani kwa baba wa mtoto)
akasalimie, Maya akakubali lakini akamwambia atapitia kwanza Arusha
(nyumbani kwao) ndipo waende Bukoba.
“Justine akamuelewa lakini kumbe alidanganya, hakwenda Arusha na kuna
watu walimuona akiingia kwenye klabu moja hapahapa Dar es Salaam,
wakamjulisha kaka. Sasa alipompigia kumuuliza, akawa anajing’atang’ata,
siku iliyofuata akadamkia Ubungo ili kumsafirisha mtoto kwenda Bukoba
kwa mama yetu (bibi wa mtoto) lakini alitaka kumsafirisha kwa kumtumia
kondakta,” alisema Monalisa na kuongeza:
“Alikubaliana na kondakta
huyo kisha akamwachia namba ya simu ya mama na yake ili waweze
kuwasiliana na kumpokea mtoto huko Bukoba.
Kwa bahati mbaya siku ile
yule konda alikuwa hasafiri mpaka siku inayofuatia. Mtoto akaanza
kuhangaika stendi siku nzima bila uangalizi mzuri.
“Bahati nzuri
mama mmoja msamaria mwema akafuatilia na kuonana na huyo konda,
akamuomba namba za mama wa Bukoba kisha akawasiliana naye, kwa kuwa
alikuwa na safari ya kwenda huko siku iliyofuata, akaamua kuchukua
jukumu la kusafiri naye.”
Monalisa alikubali kutoa namba za simu za
msamaria aliyejitolea kusafiri na mtoto huyo, alipopigiwa alikiri lakini
aliomba sana asitajwe .
“Mimi kama mzazi iliniuma sana
kumuona mtoto mdogo anahangaika stendi bila uangalizi. Nilishangaa sana
kuona mzazi aliyeingia ‘leba’ anawezaje kumwacha mwanaye mdogo namna ile
asafiri mwenyewe?” alisema.
MSIKIE BABA WA MTOTO
Tulimvutia waya baba
mzazi wa mtoto huyo, Justine aishiye Marekani ambapo alisema: “Jambo
hilo limeniumiza sana. Kwa kweli kama ningekuwa huko nyumbani (Bongo)
ningehakikisha namfundisha adabu huyo mwanamke kupitia sheria.
“Nashukuru kusikia kwamba mwanangu alifikishwa salama Bukoba.”
MAMA WA MTOTO SASA
Mama wa mtoto huyo alipopigiwa simu alizua
kioja baada ya kukataa kwamba hajawahi kumuacha mtoto kwa konda Ubungo
na pia akadai eti hana mtoto na wala hajawahi kuzaa katika maisha yake
yote.
Wakati tukijiandaa kwenda mitamboni juzi Jumatatu, habari
zilizopenyeza katika chumba chetu cha habari zilisema kwamba mrembo huyo
alimpigia simu mama mkwe wake na kumchimba mkwara mzito.