14 September 2012

MAHAKAMA YAAMURU MBOWE AKAMATWE

MAHAKAMA ya Wilaya Hai, mkoani Kilimanjaro, imetoa hati ya kukamatwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, baada ya kushindwa kufika mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.
Hati ya kukamatwa kwa Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai, ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Denis Mbelembwa, baada ya mbunge huyo kutohudhuria mahakamani hapo bila taarifa yoyote.

Pamoja na kutolewa hati ya kukamatwa Mbowe, pia hakimu huyo alitoa hati ya kumkamata mdhamini wa Mbowe, Awadh Uronu, kwa kile kilichodaiwa kuwa amekiuka masharti ya udhamini.

Hakimu huyo alitoa hati hiyo, baada ya Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Inspekta Marwa Mwita, kuiambia Mahakama kuwa, kitendo cha Mbowe kutohudhuria mahakamani hapo amekiuka masharti ya dhamana.

Katika shauri hili, Mbowe anakabiliwa na mashitaka ya kufanya vurugu na kumjeruhi Msimamizi wa Uchaguzi, siku ya uchaguzi mkuu mwaka 2010.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Mbowe anadaiwa kufanya vurugu huzo Oktoba 31, katika kituo cha Uchaguzi kiitwacho Lambo.

Inadaiwa kwamba, mshitakiwa huyo alimshambulia msimamizi huyo, Nasri Othmani na kumsababishia maumivu makali mwilini.

Mbowe ameshitakiwa kutokana na kuvunja kifungu namba 240 sura 16 cha Sheria ya Makosa ya Jinai.

Pamoja na kutolewa hati ya kumkamata Mbowe na mdhamini wake, kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa Septemba 18, mwaka huu.
Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname