31 July 2012

Sababu za Azam kumuuza Ngassa kwa milioni 80/-

Uongozi wa klabu ya Azam ya jijini Dar es Salaam umesema kuwa umekasirishwa na kitendo cha kuibusu nembo ya klabu ya Yanga kilichoonyeshwa na mshambuliaji wake Mrisho Ngassa na kuongeza kwamba sasa uko tayari kumuuza mchezaji huyo kwa dola za Marekani
50,000 (Sh. milioni 80).


Hatua hiyo ya Azam imekuja kufuatia nyota huyo kuonyesha wazi mapenzi yake kwa klabu yake hiyo ya zamani, ambayo ni bingwa wa soka wa Afrika Mashariki na Kati.


Ngassa aliibusu nembo ya Yanga wakati akishangilia goli la pili alilofunga wakati timu yake ikicheza dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kushinda 2-1 katika mechi yao ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

Azam imeeleza katika mtandao wake wa facebook kuwa, kitendo hicho (cha Ngassa) hakikuwa sahihi na watakuwa tayari kumuuza mchezaji huyo kwa kiasi hicho cha fedha kwa klabu yoyote ya ndani na nje ya Tanzania.

Hata hivyo, hadi kufikia jana mchana, taarifa kutoka ndani ya Azam zimeeleza kuwa hakuna ofa yoyote waliyopokea kutoka Yanga, Simba au klabu nyingine, licha ya mshambuliaji huyo kutajwa hivi karibuni kuwa ni miongoni mwa nyota wanaotakiwa na timu hizo.

Imeelezwa kuwa Ngassa amekuwa akionekana mara kadhaa ndani ya jengo la Yanga ambako huwafuata wachezaji Jerryson Tegete na Hamisi Kiiza ambao ndio marafiki zake wa karibu.

"Hakuna chumba cha Ngassa kama inavyodaiwa, ila akija klabuni mara nyingi huwafuata Kiiza au Tegete na kwenda vyumbani kwao, vyumba vyote vina wachezaji ambao wanaichezea Yanga hivi sasa," alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.

Azam ambayo Jumamosi ilijiandikia rekodi kwa kufika fainali ya michuano iliyoshiriki kwa mara ya kwanza katika historia yake ya Kombe la Kagame, ilimaliza Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliomalizika ikiwa ya pili na hivyo mwakani itaiwakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Ngassa ambaye aliwahi kwenda nje ya nchi kufanya majaribio na klabu ya Seattle Sounds ya Marekani, aliliambia gazeti hili juzi kwamba anajituma kila anapokuwa uwanjani na anaheshimu kazi yake.

Nyota huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa (Taifa Stars) aliongeza kwamba anafahamu yuko Azam kikazi na ataendelea kuitumikia kwa sababu ilimsajili baada ya kuridhishwa na kiwango chake.

Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic, aliwahi kusema kwamba anamuhitaji Ngassa katika kikosi chake na amesikitishwa na uongozi kushindwa kumpata katika usajili wao msimu huu.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname