17 February 2012

Mbowe: Dk Slaa ruksa kugombea Arumeru

ALIYEPEPERUSHA BENDERA CHADEMA 2010 AREJEA KUTOKA MAREKANI, AUNGA MKONO
WAKATI Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akianza kugusa hisia za watu wanaomtaka agombee ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema iwapo mtendaji mkuu huyo wa chama ataamua kuwania kiti hicho, wataheshimu uamuzi wake.
Wakati Mbowe akitoa kauli hiyo, aliyepeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2010, Joshua Nasari na kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM, marehemu Jeremiah Sumari, naye amesema kama katibu mkuu wake ataamua kuwania kiti hicho, hatakuwa na pingamizi ikiwa
chama kitaamua kwani lengo ni kutwaa jimbo hilo.
Akizungumza na Mwananchi jana baada ya kuibuka mjadala kuhusu uwezekano wa Dk Slaa kuwania jimbo hilo, Mbowe alisema, “Katika suala la kugombea, utashi binafsi ni jambo la msingi…,kama Dk Slaa ataamua kugombea ubunge  Arumeru Mashariki, tutaheshimu uamuzi wake.”
Mbowe alisema katika uteuzi wa chama, kuna vigezo vinavyoangaliwa ikiwa ni pamoja na jinsi mtu anavyokubalika kwa wananchi anakogombea, sifa zake na utashi wake binafsi na kuongeza, “Hatuna uteule katika chama.”
Hata hivyo, Mbowe alisema Chadema hakiwezi kumlazimisha Dk Slaa akagombee jimbo hilo kama mwenyewe utashi haumtumi kufanya hivyo, na kwamba hana shaka na kukubalika kwa katibu mkuu huyo kutokana na imani aliyojijengea kwa umma wa Watanzania.
Mbowe alisema Dk Slaa amekuwa akiombwa kugombea ubunge katika maeneo mengi likiwamo Jimbo la Igunga, lakini chama kisingeweza kumlazimisha kwani jambo la kwanza ilibidi mwenyewe aonyeshe utashi binafsi wa kutaka kuwania kiti hicho.
“Dk Slaa aliwahi kuombwa akagombee Igunga, lakini hakwenda. Hii ni kwasababu anakubalika nchini karibu kote, hivyo kama atakuwa na utashi binafsi kwanza, nadhani taratibu za chama zitatumika tu kufikia uamuzi,” alifafanua.
Mwenyekiti huyo wa Chadema pia alitoa angalizo kwamba, wakati mwingine uamuzi wa chama kupata mgombea unaangalia jinsi mgombea alivyo na mtandao katika jimbo analotaka kugombea ili hata kama akichaguliwa aonekane ni mbunge wa eneo hilo.
“Ndiyo maana nasema kuna vigezo vingi tu, kwa mfano mtu anaweza kuwa mbunge mzuri bungeni, lakini je, ana connectivity (kinachomuunganisha) jimboni, kuangalia kama ana makazi na mtandao mwingine kwani asije akawa mbunge mzuri bungeni, lakini jimboni akiwa kama mgeni hivyo watu wakaona kama kimewapelekea pandikizi tu,”alifafanua Mbowe.
Tangu juzi kumekuwa na mjadala katika mitandao ya kijamii huku baadhi wakimtaka Dk Slaa akagombee ubunge Arumeru Mashariki kuziba pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marehebu Sumari, lakini wengine wanapinga na kumtaka aendelee kubaki na nafasi yake ya katibu mkuu wa chama kwa lengo la kukijenga.
Hata hivyo, Dk Slaa ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alishika nafasi ya pili akiwa nyuma ya Rais ya Jakaya Kikwete, juzi alinukuliwa na gazeti moja la kila siku (siyo Mwananchi) akisema, “Siwezi kulizungumzia jambo hilo, maana nilikwisha kusema muda mrefu kuwa sitaki tena ubunge na isitoshe mimi si mwenyeji wa Arumeru,”
Joshua Nasari
Kwa upande wake Nasari (26) ambaye ana mtaji mkubwa wa kura kufuatia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010 alitoa msimamo wake akisema  yupo tayari kufanya mazungumzo na viongozi wa juu ya chama chake juu ya kumpisha Dk Slaa kuwania ubunge katika jimbo hilo kama akihitaji.
Nasari ambaye amerejea hivi karibuni mjini Arusha akitokea nchini Marekani, leo anatarajiwa kuchukua fomu rasmi ili kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema.
 (mwananchi)

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname