Na Mwandishi Wetu
WAKATI
wafuasi wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (
Ukawa) wakiwa na shangwe kutokana na kumpata Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa kama mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba, ugumu wa kiongozi huyo kuingia ikulu umebainishwa, Uwazi lina
habari kamili.
Lowassa na mgombea mwenza Juma Duni Hajii.
aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza wa
serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, alijiunga na
Chadema mwishoni mwa Julai mwaka huu baada ya jina lake kukatwa wakati
wa mchakato wa kutafuta mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
nafasi ambayo ilitua kwa Dk. John Pombe Magufuli.
Ugumu
wa kwanza unaotajwa, ni uwezekano wa kutopigiwa kura na wafuasi wote wa
Chadema, ambao kuingia kwa kada huyo wa zamani wa CCM, kuliwagawa,
kwani wapo waliokubali kwa roho moja ujio wake na wengine ambao
hawakupendezwa kabisa na jambo hilo. Mgawanyo huo, unapunguza kura
ambazo angeweza kuzipata endapo wanachama hao wangekuwa kitu kimoja kama
awali.
Ingawa aliripotiwa kuwa na wafuasi wengi
akiwa CCM, ushahidi unaonesha kuwa siyo mashabiki wake wote
wamefurahishwa na hatua yake ya kuhamia upinzani, hivyo idadi kubwa ya
wapiga kura aliokuwa akiwategemea, wameamua kuachana naye na wao
kuendelea kubakia chama tawala.
Ugumu mwingine, unatokana na ukweli kuwa
licha ya Chadema kujizatiti hadi vijijini, lakini haina mtandao mpana
kama ilivyo kwa CCM, hivyo hata ile ‘amsha amsha’ inayoonekana mijini
hivi sasa, haiko vijijini, ambako chama tawala bado kina mizizi na kina
wapiga kura wengi maeneo hayo.
Jambo lingine linalotajwa kuwa ni gumu
kwa Lowassa kuingia ikulu, ni ukweli kuwa kujiweka kando kwa viongozi
wawili waliokuwa na mashabiki wengi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.
Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wa Cuf, Profesa Ibrahim Lipumba
kumewachanganya mno wafuasi wao na hivyo kuwa njia panda.
Ukimya wa Dk. Slaa, anayeaminika kufanya
kazi kubwa ya kuwashawishi watu kuipenda Chadema, umewafanya baadhi ya
wafuasi wake kutokuwa na mwelekeo, hivyo kuweka uwezekano mkubwa wa watu
hao ama kupiga kura kwa wagombea wa vyama vingine au wasipige kabisa,
kitu kitakachopunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya kura za Lowassa
kuelekea ikulu

No comments:
Post a Comment