13 August 2015

HIKI NDICHO Kilichofanyika mpaka Lowassa akatua CHADEMA na kufuta ndoto ya Dk. Slaa

 
USIKU wa Julai 10, 2015, Edward Lowassa, alipokea simu aliyoifahamu vema. Upande wa pili wa simu alizungumza mtu mwenye sauti nzito; Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). “ Mzee, nakukaribisha Chadema ili uongeze nguvu Ukawa”. Ndiyo ujumbe mfupi ambao Mbowe alimpa Lowassa siku hiyo.
Ni mazungumzo hayo ya Julai 10, ndiyo hatimaye yalimfikisha Waziri Mkuu huyo wa kwanza wa serikali ya Awamu ya Nne kwenye uamuzi wa kujiunga na Chadema mnamo Julai 28 mwaka huu, takribani wiki mbili baada ya jina lake kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha ndani ya CCM.
Nini kilifanyika hadi Lowassa akafikia uamuzi huo?
Hadi sasa, ni watu wachache sana wanafahamu kiundani ni vipi hasa Lowassa alifikia uamuzi huo wa kuhama Chama Cha Mapinduzi ambacho aliwahi kuapa huko nyuma kwamba hataweza kukihama. Hata hivyo, uchunguzi wa takribani wiki mbili wa gazeti hili, umebaini walau ni matukio gani yalitangulia tukio la Lowassa kuhamia Chadema na hatimaye kupitishwa kuwa mgombea pekee kutoka vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mmoja wa viongozi wa juu wa Ukawa aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema kabla Mbowe hajampigia simu Lowassa, kwanza alikuwa amewasiliana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad.


“ Maalim Seif ndiye wa kwanza kumshawishi Mbowe amtafute Lowassa endapo CCM itamkata kwenye kinyang’anyiro. Maalim Sif anafahamu Lowassa na Mbowe wanaheshimiana na hivyo ingekuwa rahisi kwao kuzungumza. Yeye Maalim Seif alikuwa na wadhifa kama wa Lowassa huku Bara (alikuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) na anajua kuwa mtu wa cheo kama cha Lowassa anapohamia upinzani, inakuwa na nguvu sana’’.
‘’Mwanzoni Mbowe alisita kukubaliana na pendekezo hilo la Seif kwa sababu ya historia ya nyuma ya Chadema na Lowassa. Halafu pia nadhani aliwaza atawaambiaje viongozi wenzake kuhusu jambo hilo? Mbowe alisita kwa kweli’’.
“Lakini Maalim Seif alimshawishi sana na mwishowe Mbowe akaelewa. Ndiyo maana, kwa kujua hilo, katika hatua za awali, hakuwashirikisha hata baadhi ya viongozi wa juu wa chama chake,” kilisema chanzo chetu hicho kutoka Ukawa’’.
Baada ya habari za jina la Lowassa kutokuwepo katika orodha ya majina matano yaliyopitishwa na Kamati Kuu kwenda kupigiwa kura kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ndipo Mbowe alipopiga simu yake hiyo ya kihistoria kwa Lowassa.
Akitaka kutotoa siri ya nini kinaendelea kati yake na Lowassa, Mbowe aliruhusu vikao vingine kuendelea kama kawaida na ndipo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, walipokutana na kukubaliana kuwa Slaa awe mgombea wa Ukawa.
Akijua nini kinaendelea nyuma ya pazia, Mbowe aliwataka wenzake ndani ya Ukawa kutoharakisha kumtangaza mgombea wao kwani “muda ulikuwa unaruhusu”. Mwenyekiti mwenza wa Ukawa kutoka chama cha National League for Democracy, Dk. Emmanuel Makaidi, alikieleza kipindi hicho cha kusubiri kutangaza mgombea kama kigumu.
“ Tulikuwa tukiambiwa tu kwamba kuna mtu mzito atajiunga na Ukawa. Tusubiri. Sasa mtu huyo nani tukawa hatuambiwi’’. “Kulikuwa na fununu tu nyingi kwamba ni Lowassa lakini hakuna aliyesema” alisema Makaidi katika mazungumzo yake na Raia Mwema.
Katika mazungumzo yake hayo na gazeti hili, Makaidi alisisitiza kwamba mtu pekee ndani ya Ukawa anayeweza kueleza kwa undani ni kwa vipi Lowassa alishawishiwa kujiunga na umoja huo ni Mbowe.
“Ukitaka kupata mkanda mzima wa tukio hilo, mtafute Freeman (Mbowe). Yeye ndiye aliyekuwa anajua kila kitu tangu mwanzo ingawa sasa sote tuko pamoja na tumekubaliana kwenye hilo,” alisema Makaidi.
Hali kwa Lowassa
Gazeti hili limeambiwa kwamba uamuzi wa Lowassa kuhamia Chadema na upinzani kwa ujumla, haukupokewa vema na kila mmoja katika familia yake. Hata hivyo, Raia Mwema limeambiwa na mmoja wa watu wa karibu na familia yake kwamba mwanasiasa huyo aliita familia yake kwa pamoja na kueleza kuhusu uamuzi wake huo.
“ Lowassa yuko karibu na familia yake. Wako pamoja, wanasali pamoja na aliwaeleza sababu za yeye kuchukua uamuzi huo. Si kwamba wote wamekubaliana naye kwenye uamuzi wake huo lakini walikubali kumuunga mkono. Ndipo hapo akaanza vikao rasmi na Mbowe’’.
Mbali na familia yake, Lowassa pia alipata upinzani mkali kutoka kwa swahiba wake wa kisiasa, Rostam Aziz, anayedaiwa kumshawishi abadili uamuzi wake huo hadi saa chache kabla ya mbunge huyo wa Monduli aliyemaliza muda wake kuhamia Chadema.
Kuonyesha usiri wa mazungumzo yake hayo, baadhi ya viongozi maarufu wa Chadema kama Slaa, Profesa Mwesiga Baregu, Tundu Lissu na John Mnyika hawakuhusishwa kwa chochote kwenye mazungumzo hayo. Vitabu na maandishi yanayofundisha kuhusu mazungumzo nyeti na ya siri, vinaeleza kuwa mafanikio ni makubwa wakati mazungumzo yanapofanywa na wachache na kwa siri; na inaonekana Mbowe na Slaa ni wanafunzi wazuri wa maandishi hayo.
Picha za Serena hotel
Usiku wa Julai 26 mwaka huu na asubuhi ya Julai 27, picha za Lowassa akiwa amehudhuria mkutano wa Kamati Kuu ya Chadema uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam zilisambaa katika vyombo mbalimbali vya habari. Picha zile ziliwashtua wafuatiliaji wote wa masuala ya siasa ndani na nje ya CCM na Chadema. Hadi siku moja kabla ya tukio hilo, viongozi wa juu wa chama tawala hawakuwa wakiamini kuwa taarifa za Lowassa kuhama zinaweza kutokea kweli.
Raia Mwema limeambiwa kuwa picha zile zilitoka kwa bahati mbaya kwani Chadema ilipanga kumtambulisha rasmi katika mkutano ambao ungehudhuriwa na viongozi wote wa Ukawa. Gazeti hili limeambiwa kuwa hiyo ndiyo sababu hata tukio lenyewe la Lowassa kutambulishwa kwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema lilifanyika usiku wa manane siku hiyo.
Mmoja wa aliyehudhuria mkutano huo alituma picha hizo kwa mmoja wa rafiki zake (labda kwa furaha au kwa mshtuko) kabla Mwenyekiti hajawaambia kuwa hawatakiwi kutuma picha hizo nje. Kilichobaki baada ya hapo ni historia.
Ni katika kikao hicho ndipo Dk. Slaa alipotoa hoja kwamba inabidi Lowassa aikane kwanza CCM hadharani na ajisafishe kabla ya kukubaliwa na Chadema. Hoja hizo zilipingwa na Mbowe aliyesema kwamba uwepo wa Lowassa unaihakikishia Ukawa ushindi na kwamba wana Chadema wanatakiwa kutazama hilo kuliko mambo yaliyopita huko nyuma. Slaa hakukubaliana na maelezo hayo ya Mwenyekiti wake na “amepumzika” kujihusisha na shughuli za siasa tangu wakati huo.
Lipumba, Maalim na Jussa
Kuna mkanganyiko kuhusu Profesa Lipumba. Kwanza Raia Mwema limeambiwa na vyanzo vyake kuwa nyuma ya uamuzi wa Maalim Seif kumshawishi Mbowe amtafute Lowassa ni Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa.
Jussa ambaye amewahi kuwa msaidizi binafsi wa Maalim Seif, anadaiwa ndiye aliyempa wazo hilo Seif na Makamu huyo wa Pili wa SMZ alilichukua moja kwa moja kwa sababu ya ukaribu wake na mwakilishi huyo. Lipumba tayari amewaambia watu wake wa karibu kuwa Maalim Seif ndiye aliyemshinikiza kuhudhuria vikao ambavyo vinaonekana kama ndivyo vilivyobariki ujio wa Lowassa Ukawa.
Muhimu zaidi kikiwa kile kilichomtangaza rasmi Lowassa kama mwana Ukawa mnamo Julai 28 mwaka katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam. Watu wa karibu na Lipumba wanadai tangu mwanzo hakuunga mkono ujio wa Lowassa Ukawa lakini kilichommaliza nguvu ni hatua ya kumpitisha kuwa mgombea wa Ukawa.
Kwa maoni ya Lipumba, “hakukuwa na tatizo kumkaribisha Lowassa kwenye Ukawa kama mwanachama wa kawaida lakini si kama mgombea”.
Uteuzi wa Lowassa kuwa mgombea wa Ukawa, ndiko hatimaye kulikomfanya Lipumba abwage manyanga, Raia Mwema limeambiwa.
CHANZO: Gazeti la RaiaMwema

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname