Hamfrey
Polepole na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa wamekabana
kwa hoja kali kuhusu uamuzi wa Chadema na Ukawa kwa ujumla kumpokea
Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea Urais.
Polepole na Msigwa walikutana jana katika kipindi cha ‘Mada Moto’
kinachorushwa na kituo cha runinga cha Chanel Ten kujadili mada
iliyotajwa kama ‘Lowassa Ndani ya CCM’.
Polepole alionesha msimamo wake wa kumkataa Edward Lowassa kuwa sio
kiongozi sahihi aliyepaswa kuungana na Ukawa katika safari yao ya kutaka
kuongoza dola na kupata katiba mpya ya wananchi kwa kuwa ana tuhuma
nzito zilizompa madoa.
Aliongeza kuwa dhana ya upinzani na mwenendo wa Ukawa ulipotea pale
walipomkaribisha Lowassa huku wakisahau kuwa ni miaka michache iliyopita
walizunguka nchi nzima kuwaaminisha watanzania kuwa ni fisadina kwamba
wana ushahidi wa kutosha.
Polepole ambaye alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iyoongozwa na Jaji Warioba, alisema kuwa Ukawa iliundwa kwa madhumuni
ya kutetea Katiba ya Wananchi na sio kwa lengo la kisiasa kama ilivyo
sasa.
Alisema kuwa Edward Lowassa hana msimamo thabiti kwenye maamuzi yake
kuhusu Katiba anayoitaka kwa kuwa aliwahi kumhoji awali akasema
anahitaji muundo wa serikali tatu lakini baadae alimfuata na kumueleza
kuwa amebadili anataka muundo wa serikali mbili.
“Lowassa niliongea naye wakati huo nakusanya maoni kuhusu katiba mpya,
mara ya kwanza alisema anataka serikali tatu na akaandika kwenye
kumbukumbu maalum za bunge. Lakini baadae alinifuata tena na kubadili
msimamo wake akitaka serikali mbili,” alisema Polepole.
Anasema kilichomshangaza zaidi kwa Lowassa ni pale alipopendekeza kuwa
anataka muundo wa serikali mbili na kwamba serikali hizi mbili ziwe na
uhusiano wa kijeshi pekee.
Akiendelea kutetea hoja yake ya kumpinga Lowassa, PolePole alisema kuwa
amewahi kufanya kazi na Lowassa na kwa undani kabisa aligundua kuwa ni
mbinafsi.
“Watanzania mnatakiwa kufahamu kuwa mnapokutana na Lowassa, Ninyi sio kitu bali kitu ni Lowassa,” alisema.
Mjadala huo ulitawaliwa na mivutano binafsi iliyowalazimisha kutoka nje
ya mada mara kadhaa hususan baada ya Mchungaji Msigwa kutoa tuhuma za
Polepole hadharani kisha akampa nafasi ya kujitetea.
Baada ya PolePole Kujitetea kufuatia tuhuma hizo, Mchungaji Msigwa
alimueleza kuwa alichokifanya ndio kinaitwa ‘natural justice’ ambayo
Edward Lowassa hakupewa wakati ule.
Akizijibu hoja za Polepole huku kukiwa na majibishano ya hapa na pale,
Mchungaji Msigwa alikiri kuwa yeye ni mmoja kati ya wanachama wa Ukawa
waliomsema sana Edward Lowassa na kumuita fisadi lakini sasa ameamua
kukaa kimya.
“It’s true tulisema. Hata mimi nilisema, it’s true I can’t deny it.
Lakini hata Joe Biden (Makomo wa pili wa Marekani) alikuwa anamsema
Obama kuwa ‘he does not fit for Commander in Chief, lakini
alipochaguliwa wakafanya kazi pamoja. Hatuwezi kusema kana kwamba
Lowassa ndiye muovu kuliko mtanzania yeyote hapa nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa kitu kikubwa alichojifunza kwa Lowassa na kumfanya
amheshimu sana, ni moyo wa uvumilivu na kukaa kimya hata pale alipokuwa
akitukanwa kila kona na kuitwa Fisadi. Alisema moyo huo wa uvumilivu
hata watumishi wengi wa Mungu hawana.
Alifafanua kuwa katika ulimwengu wa siasa ni kawaida kufanya kazi na
mwanasiasa ambaye awali ulikuwa ukimpinga sana kwa kuwa muda ukifika
akaamua kubadilika mambo hubadilika pia.
Msigwa alisema kuwa chama chao ni chama cha demokrasia na maendeleo na
kwamba hilo ndilo limewapelekea kumfungulia mlango Edward Lowassa baada
ya kumhoji na kumuelewa.
Alipinga hoja ya Polepole kuwa Lowassa ana mapesa mengi ambayo ameyapata
kwa njia zisizofahamika, Msingwa alisema kuwa maelezo hayo hutolewa
bila kuelezewa kwa undani kama ana pesa nyingi kuliko nani (serikalini).
“Unasema Lowassa ana mapesa mengi, ni kama vile unajua akaunti zote za
Lowassa zina shilingi ngapi. Na husema ana fedha nyingi kuliko nani?”
Aliwataka watanzania kutomchukulia Lowassa kama vile ndiye mtanzania
mwenye dhambi nyingi kuliko wote bali wajikite katika kuangalia nia yake
ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
Alisisitiza kuwa Chadema hawana muda wa kumsafisha Lowassa kwa kuwa
umati uliofurika kumsindikiza kuchukua fomu ya kugombea urais katika
ofisi za Tume ya Uchaguzi Mkuu (NEC) inaonesha jinsi ambavyo watanzania
wana Imani naye.
Alisema kuwa kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika hivi karibuni zinaonesha
kuwa ni asilimia 5 hadi 8 tu ya watanzania ambao wamejikita katika
kufahamu ufisadi wa wagombea na kwamba umma mkubwa unataka mabadiliko
kwa kuwa wamechoshwa na muundo.
Msigwa alimtaka PolePole kutomzungumzia Lowassa pekee kwa mtazamo hasi
bali azungumzie pia ubaya wa Magufuli ambaye anaunga mkono muundo wa
serikali mbili kinyume na ile anayoisapoti Polepole na Tume Ya
Mabadiliko Ya Katiba. Na kwamba yapo maovu mengi kwenye wizara ya ujenzi
inayoongozwa na Mafuli.
Akijibu hoja ya Msigwa, PolePole alisema kuwa yeye ni mmoja kati ya watu
walioishawishi CCM kukata majina ya wagombea wote wenye madoa katika
mchakato wa kura za maoni kumpata mgombea urais.
Alisisitiza kuwa ingawa CCM ni chama chake, hatampigia kampeni Magufuli
hadi pale ambapo rufaa zilizokatwa dhidi ya wagombea waliotangazwa kuwa
washindi wa kura za maoni ziangaliwe na wote wenye madoa waondolewe.
“Ili niwaunge mkono, CCM mnatakiwa kuwakata watu wote katika mchakato wa
kura za maoni wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali,” alisema Polepole
ambaye awali alitangaza kutembea nchi nzima kuhamasisha watu wasimchague
Lowassa.
PolePole alitoa ushauri pia kwa chama chake cha CCM ili kiwe tofauti na makosa yaliyofanywa na wahasimu wao wa kisiasa, Ukawa.
“Viongozi wa CCM, kama Ukawa wamewachukua watuhumiwa wamewakubali. Nyie
onesheni uongozi na utofauti mhakikishe mnawakata wagombea wote
wanaotuhumiwa. Onesheni kwamba watuhumiwa hawana nafasi kwenu
No comments:
Post a Comment