06 January 2015

Simba yaikwepa Yanga, yamchenjia Okwi fasta

SIMBA imefanikiwa kutinga robo fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga JKU bao 1-0 jana Jumatatu usiku kwenye Uwanja wa Amaan, lakini mambo ni yamebadilika ndani ya timu hiyo na Kocha Goran Kopunovic hataki mchezo.
Bao la Simba katika mchezo huo lilifungwa na kiungo mshambuliaji Ramadhan Singano katika dakika ya 12 baada ya kupokea pasi ya Awadh Juma. Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe pointi sita na kuongoza Kundi C lenye timu za JKU, Mtibwa Sugar na Mafunzo.

Simba inaweza kukutana na timu itakayoshika nafasi ya tatu yenye pointi nyingi ambayo inaweza kuwa Polisi au Taifa Jang’ombe za Kundi A au KMKM ya Kundi B mchezo utakaochezwa kesho Jumatano.

Matokeo hayo pia yameifanya Simba kuchomoka mikoni mwa Yanga kwani ingepoteza ama kutoka sare mchezo huo ingeweza ingekutana na Yanga robo fainali ambayo tayari imeshatinga katika hatua hiyo baada ya kushinda mechi zake mbili za awali.

Timu nyingine iliyotinga robo fainali ni Mtibwa iliyomaliza nafasi ya pili Kundi C ikiwa na pointi tano baada ya jana mchana kutoka suluhu na Mafunzo. Mtibwa sasa itacheza robo fainali na mshindi wa pili wa Kundi B lenye timu za Azam FC, KMKM, KCCA na Mtende ambazo leo zinacheza mechi zao za mwisho.

Mambo yambadilikia Okwi

Mambo sasa yamebadilika ndani ya Simba baada ya kocha Kopunovic kuueleza wazi uongozi kama ukiendelea kubembeleza wachezaji wake na kuwapa ruhusu zisizo na maana, hakuna itakachoambulia katika Kombe la Mapinduzi na Ligi Kuu Bara.

Muda mfupi baada ya kuanza kazi katika mazoezi ya timu hiyo Uwanja wa Ngome, Kopunovic alionyesha kukerwa na utoro wa wachezaji wawili Joseph Owino na Emmanuel Okwi.

Tofauti na wenzake ambao wana na madai ya haki zao za mishahara na fedha za usajili, Okwi aliomba ruhusa ili akamalizia fungate kwao Uganda baada ya kufunga ndoa hivi karibuni. Tayari Simon ameshatua Zanzibar jana Jumatatu.

Katibu wa Simba, Steven Ally aliliambia Mwanaspoti wamepanga kuwaweka kitimoto wachezaji hao kutokana na kitendo cha kuchelewa kuwasili Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi.

“Kweli Okwi tulimpa ruhusa lakini muda wake wa kurudi umeshafika na bado hajarejea.

“Kwa pamoja na kocha tumekubaliana wachezaji wote watakapofika Zanzibar akiwemo Okwi, wajieleze kwa maandishi kwa uongozi na kama sababu watakazotoa hazitakuwa na maana tutawachukulia hatua kwa maana wanaiyumbisha timu,” alisema.
Tayari Kopunovic ameshapewa habari zote kuhusu wachezaji wa kigeni wa Simba ambao wote wanatokea Uganda kuhusu tabia yao ya kuchelewa kurejea katika timu kila wanapopewa ruhusa ya muda mfupi. “Nidhamu ya nje na ndani ya uwanja ndiyo kitu kinachotakiwa kufanywa na kila mtu, sasa mchezaji wa kulipwa unachelewaje katika timu? Nitashughulika nao ili tuwe na timu yenye nidhamu itakayopata matokeo mazuri,” alisema Kopunovic

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname